Saturday, April 30, 2011

MZEE KARUME ALIYAKIMBIYA MAPINDUZI YA ZANZIBAR


Karume aliyakimbia mapinduzi-II
NIMEPOKEA maswali mengi na hoja mbalimbali kutoka kwa wasomaji wa gazeti hili kutokana na makala yangu iliyochapishwa katika toleo la 30 Aprili 2008 iliyobeba kichwa cha habari kisemacho: “Karume na zimwi la Mapinduzi.”
Karibu hoja zote na maswali zililenga kutaka ufafanuzi juu ya kutaka kufahamu kama kweli muasisi wa taifa la Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume, hakushiriki katika mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.
Wengi waliuliza, “Kama Karume hakushiriki, kwa nini historia inapotoshwa?”
Katika makala yangu nilieleza kwa ufupi kwamba inawezekana kabisa wazo la mapinduzi halikuwamo akilini mwa Karume.

Nilisema Karume ambaye tangu mwanzo alipendelea kuona Serikali ya mseto kati ya vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na chama chake- Shirazi Party (ASP), kama njia pekee ya kuleta umoja wa kitaifa.
Ingawa kuna taarifa kwamba Waziri Mkuu wa wakati huo, Mohamed Shamte, alikataa ombi la Karume, upo ushahidi kuwa serikali hiyo iliundwa mwaka 1961.
Katika serikali hiyo ya mpito, Karume alipewa na alikubali kupokea nafasi ya uwaziri wa Siha (Afya).
Hii ni ishara tosha kwamba chama cha ASP kiliutambua ushindi wa serikali ya ZNP na ZPPP; hoja inayojitokeza sasa kwamba Zanzibar ilipata uhuru 12 Januari 1964, badala ya 10 Desemba 1963 ni dhaifu na isiyo na mashiko.
Kuna madai pia kwamba Karume hakuwahi kuwa rais wa Zanzibar. hii ni kwa sababu rais huchaguliwa chini ya Katiba; mtu anayeongoza Mapinduzi huitwa “Kiongozi wa Mapinduzi.”
Vilevile, Karume hakuwahi kuchaguliwa hata mara moja na wananchi wa Zanzibar. Pia chini yake, Zanzibar haikuwahi kuwa na katiba.

Kuhusu mapinduzi, Karume mwenyewe aliwahi kukiri kwamba aliondoka Zanzibar mara tu harakati za mapinduzi zilipoanza.
Hatua hiyo inadhihirisha kwamba Karume aliyakimbia mapinduzi hayo. Ni kutokana na kutojua mapema kilichokuwa kikiendelea.
Hizi si taarifa ya uzushi. Ni taarifa sahihi na zinazothibitishwa na mtandao wa Wikipedia Encyclopedia.
Kwa mujibu wa mtandao huo, “Abeid Karume hakuwa Zanzibar usiku ule Mapinduzi yalipofanyika.”
Wengi wanasema Mapinduzi haya yalipangwa na Wakulima, Wakwezi na Wavuvi. Hapana! Mapinduzi yalipangwa na watu wenye kuelewa mambo na wenye ujuzi wa kutosha wa kutumia silaha.
Hawa ni baadhi ya polisi wasio Wazanzibari walioachishwa kazi baada ya uhuru wa Desemba 1963 na kubakia Zanzibar wakiumia kimaisha bila kazi.
Maana kama mapinduzi yalipangwa na wakulima, wavuni na wakwezi, kundi hili lilipata wapi uzoefu wa silaha na mbinu za kivita hata kuteka vituo vya usalama na kupora silaha?
Waliopanga kufanya mapinduzi wanafahamika. Hawa hawakuwa Wazanzibari asilia. Ni pamoja na Field Marshal (John Okello (Mganda) na msaidizi wake, Absalom Anwi Ingen (Mjaluo kutoka Kenya).

Wengine ni Saidi Washoto (Tanganyika) sasa Tanzania Bara, Mohamed Kaujore (Mmakonde wa Msumbiji) na Hamisi Darwesh (Tanganyika).
Walikuwapo pia akina Abdallah Mfaranyaki (Tanganyika), Saidi Natepe (Tanganyika), Seif Bakari (Tanganyika) na Edington Kisasi (Mchaga wa Kilimanjaro-Tanganyika).
Vyombo vya habari navyo vinatoa ushuhuda juu ya nani aliongoza Mapinduzi. Gazeti la serikali ya Tanganyika (The Standard) la 13 Januari 1964, liliandika katika ukurasa wake wa mbele kwamba:
“Wapigania Uhuru waliokuwa na silaha wamekitwaa Kisiwa cha Zanzibar. Wamekamata majengo yote muhimu ya Serikali kwa muda usiozidi saa 24. Usiku Kiongozi wa Mapinduzi alitangaza muundo wa Serikali mpya ya Jamhuri ya Zanzibar na Pemba …”.
Kiongozi huyo alikuwa Okello, ambaye katika tangazo lake la Mapinduzi alipanga Baraza lake la Mawaziri.

Field Marshal John Okello (Waziri wa Ulinzi na Utangazaji na Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi); Sheikh Abeid Amani Karume (Rais wa Serikali ya Mapinduzi) na Kassim Hanga, Makamu wa Rais.
Mawaziri wake walikuwa ni Abdurahman Babu (Ulinzi na Mambo ya Nje), Aboud Jumbe (Afya na Huduma za Jamii) na Othman Sharrif (Elimu).
Okello aliwateua pia Hasnu Mukame kuongoza Wizara ya Kilimo na Idris Abdul-wakili kuongoza Wizara ya Biashara.
Haukupita muda Okello akamtaja Hasnu Makame kuwa Waziri wa Fedha na Salehe Sadallah (Kilimo).
Okello alimaliza kwa kusema, ”Serikali sasa inaendeshwa nasi –Jeshi. Ni juu ya kila raia, mweusi, maji ya kunde au mweupe kutii amri……”.

Gazeti hilo “The Standard,” lilizidi kuthibitisha kuwa Field Marshal amefanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari katika ofisi za kurushia matangazo.
Gazeti lilisema, “lundo la bastola lilikuwa mbele ya meza yake. Walinzi wenye silaha mbalimbali walisimama kumzunguka kwa utii na nidhamu….”
“…ni yeye aliyepanga kuiangusha Serikali ya Zanzibar akisaidiwa na Kamati Kuu yake ya watu waliopewa siku 14 tu za mafunzo msituni.”
Ali Muhsin Ali Barwan, aliyekuwepo Zanzibar siku ya Mapinduzi anaeleza katika Kitabu chake “Conflicts and Harmony in Zanzibar,” kwamba “…John Okello, askari mamluki, aliongoza mauaji ya kinyama …. Watu 12,000 walichinjwa…”

Nalo gazeti la The Spectator la nchini Uingereza katika toleo lake la 7 Februari 1964, chini ya makala iliyosema “Gidion’s Voice” pamoja na lile la 12 Februari 1964 “How it Happened”, linaeleza kuwa ni John Gidion Okello aliyeongoza mapinduzi.
Gazeti linafika mbali zaidi na kusema, “ni yeye aliyewavuta wote waliokuja kushirikiana naye katika kutekeleza mapinduzi hayo.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haroub Othman (Mzanzibar), katika kitabu kiitwacho, “Mwalimu The Enfluence of Nyerere-Uk 172,” anathibitisha kuwa uhuru wa Zanzibar ulipatikana 10 Desemba 1963.
Anasema Sultan alikuwa Mkuu wa Nchi, na kupewa mamlaka ya kuteuwa mrithi wake. Serikali hiyo ilipinduliwa ndani ya majuma matano tu na “Masiha mjinga,” ambaye ni kiongozi wa wanaharakati John Okello.
Okello alisimika Baraza la Mapinduzi ndani ya kipindi kifupi chini uongozi wa Karume.
Hata Amiri Mohamed anakiri katika kitabu chake “A Guide to a History of Zanzibar” kwamba Okello ndiye aliyetawala Uwanja wa Mapinduzi kwa miezi miwili mfululizo kuanzia 12 Januari 1964 hadi alipokamatwa na kufukuzwa nchini akiwa ziarani Tanganyika. Aliambiwa ni mhamiaji asiyetakiwa visiwani humo.
Anasema ya kuwa Okello akiwa na wapiganaji wapatao 400 aliongoza mashambulizi na baada ya kukamilisha kazi aliendelea kutoa maagizo kupitia kituo cha radio.
Anasema, “ukweli wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanaona kuwa Okello ndiye alikuwa rais wa kwanza halali wa Serikali mpya ya Mapinduzi yenye Baraza kamili la Mawaziri.
Hakuna mahali popote wala kumbukumbu za historia, kuonyesha kwamba Abeid Amani Karume aliwahi, katika hatua yeyote ile, kupanga, kuongoza au kushiriki katika Mapinduzi hayo ya 12 Januari 1964.


Sasa kama ni hivyo, kwa nini historia ilipotoshwa na ushiriki wa Okello kutopewa uzito unaostahili?
Jibu linatolewa na Michael F. Lofchie, katika Kitabu chake Was Okello’s Revolution a Consiracy kuanzia uk 36 hadi 42. Anasema, “Okello alifanya Mapinduzi ya Zanzibar…..Njama za kumwondoa Zanzibar ni za kuficha ukweli unaochukiza….”
Kutokana na hali hiyo, majigambo, hila na hadaa za rais wa sasa wa Zanzibar, kwamba baba yake (Abeid Amani Karume), ndiye aliyeendesha mapinduzi hayo, hayana msingi na kuendeleza kuyasikiliza, ni kufinyanga historia.


mwenye shati jeusi aliye ktk na kofia
ndiye
JOHN OKELLO
na kundi lake lililo ipinduwa serekali ya kwanza ya
ZANZIBAR
YA
1963
BAADA YA ZANZIBAR KUPATA UHURU WAKE.

No comments:

Post a Comment