Monday, April 25, 2011

SMZ YAGOMA KUILIPA .............TANESCO





Waziri wa Ardhi, Maji, Makazi na Nishati wa Zanzibar, Ali Juma Shamhuna na Mwakilishi wa Jimbo la Donge Kaskazini Unguja aliwaeleza wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba kamwe SMZ haitolipa fedha kwa Shirika la Umeme Tanzani (TANESCO)

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekataa kulipa deni la umeme la shilingi bilioni 40 kwa TANESCO baada ya kupandishiwa kiwango cha malipo.
 Waziri wa Ardhi, Maji, Makazi na Nishati wa Zanzibar, Ali Juma Shamhuna amesema baada ya kiwango serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatakiwa kulipa kwa asilimia 168 badala ya asilimia 21  kwa uniti.
Shamhuna alikuwa akichangia katika majumuisho ya mjadala juu ripoti ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambapo Shamuhuna  alisema, “hatukubali kulipa deni la shilingi bilioni 40 kwa kiwango cha asilimia 168 asiliani.”
Shirika la Tanesco ilipandisha viwango vya malipo kwa wateja wake tokea mwaka jana kwa asilimia 21, kwa upande wa Tanzania bara ambapo kwa Zanzibar shirika hilo la umeme ukapandishwa kwa asilimia 168 na kusababisha malalamiko makubwa upande wa Zanzibar.
Shamhuna alisema kuendelea kwa Tanesco kudai deni hilo kunakwenda kinyume na agizo la Rais Jakaya Kikwete kwamba pande zote mbili za Muungano zilipe viwango sawa vya asilimia 21 kulipa umeme na sio Zanzibar peke yao kupandishiwa bei jambo mbalo alisema sio sahihi.
Waziri huyo ambaye alikuwa akichangia na kupigiwa makofi na wajumbe wengine alisema ili kuepukana na utegemezi wa umeme kutoka Tanesco ambao unaigharimu SMZ fedha nyingi, serikali umeanza kuchukua hatua za kuzungumza na wawekezaji wazoefu ili kuzalisha umeme kutokana na jua na gesi utakaojitegemea.
Shamhuna aliwamabia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba mradi kama huu umefanikiwa Dubai na Malaysia unaweza kuzalisha kati ya Megawati 50 na 100 ambao unatosheleza mahitaji ya sasa ya Zanzibar ya Megawati 50.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu madai ya baadhi ya Wajumbe wa baraza la Wawakilishi la kutaka Zanzibar izalishe umeme kwa kutumia mawimbi ya bahari, Shamhuna alisema utafiti unaonyesha kuwa ni mradi mkubwa wenye gharama kubwa na pia haujafanikiwa katika nchi nyingi duniani.
wakichangia mjadala huo wajumbe wengine wa baraza hilo wamesema suala hilo linahitaji kuangalia vyema na serikali ya muungano kwani haiwezekani serikali hiyo kukaa kimya na baadhi yao kutaka fedha hizo kutolipwa kwani haitowezekana kungangania fedha hizo.
Katika hatua nyengine wajumbe wa baraza la wawakilishi wamehoji juu ya majenereta 32 yaliyonunuliwa mwaka jana na kugharimu shilingi 17 billioni ili kukabiliana na tatizo la umeme Zanzibar kutotumika wakati huu ambao kuna matatizo ya umeme.
Wajumbe hao wamesema kuna taarifa kwamba majenereta hayo ni mabovu na wengine kutoa kauli za kutofanya kazi kutokana na kukosekana kwa mafuta maalumu ya kuendeshea majenereta hayo jambo ambalo lilihitaji majibu kutoka serikalini.
Shamuhuna aliwaambiwa wajumbe hao kwamba majereta yote 32 ni mazima, lakini yameshindwa kufanyakazi kutokana na ukosefu wa fedha za kununua mafuta za kuyaendesha jambo ambalo linahitaji kupatikana fedha za kutosha.
Baraza la wawakilishi limefungwa hapo jana hadi juni 15 ambapo kikao kitakachofuata kitakuwa ni cha kujadili bajeti, jumla ya maswali 88 kati ya 147, yaliulizwa na kujibiwa na miswaada minne ya sheria kupitishwa katika kikao hicho.

No comments:

Post a Comment