Monday, April 25, 2011

TUTAISHITAKI SEREKALI YA ZANZIBAR




Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib katikati Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa NCCR-Mageuzi, Ali Omar Juma na Mwenyekiti wa AFP, Said Soud Said wakizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa MAELEZO leo asubuhi kuelezea azma yao ya kutaka kwenda mahamani dhidi ya kitendo cha serikali kujiamuliwa na kuchukua mali za umma bila ya kufuata taratibu kisheria.
VYAMA vitatu vya siasa hapa Zanzibar vimekusudia kuishitaki Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutokana na mtindo wake wa kuuza majengo ya serikali au kuitisha maandamano makubwa ya wananchi kupinga uamuzi huo.
Mkurugenzi wa ya Nje wa Chama cha NCCR Mageuzi, Ali Omar Juma amesema wataipeleka mahakamani serikali kwa kuuza majengo yaliyokuwa yakitumika na afisi ya mrajis mkuu wa nyaraka Zanzibar.
Kauli hiyo alitowa wakati akizungumza na wandishi wa habari katika ukumbi wa habari maelezo Rahaleo Mjini Zanzibar, Omar alisema Baraza la Wawakilishi limeshindwa kutoa kauli yeyote pale inapotokea kuvunjwa kwa sheria ambazo ndizo muongozo mkuu wa kulinda mali za umma zisiporwe.
“Tunaishauri serikali yetu kuzingatia matakwa ya umma katika kuyarejesha majengo hayo mikononi mwa wananchi na iwapo itashindikana kupatikana ufumbuzi wa majego hayo, tunakusudia kuwaongoza wazanzibari kuitisha maandamano ya amani yenye misingi ya kisheria na kufuatiwa na kufungua kesi ya madai mahakamani dhidi ya serikali ya mapinduzi zanzibar na kampuni ya Zamani Zanzibar Kempinski” walisema viongozi hao watatu katika mkutano wao.
Omar alisema mwenendo mzima wa uuzaji wa majengo hayo haukukidhi matakwa ya kisheria na kamwe jambo hilo halikuwahi kutangazwa na bodi yenye mamlaka kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma wa Wazanzibari hali iliyopelekea wananchi kutofahamu jambo lolote juu ya mustakabali wa rasilimali zao.
Kutokana na uuzwaji wa najengo hayo ya umma ni dhahiri kuwa taratibu na sheria hazikuzingatiwa katika kufikia mkataba wa mauzo wa majengo pacha yaliyopo Mambo Msige.
“Majengo ambayo tunayoyazungumzia ni majengo ya umma ambayo yalitumiwa na kuendesha shughuli mbali mbali za serikali na kutumika kuwa ni afisi za umma ambayo mshangao wetu majengo hayo yameuziwa kwa kampuni binafsi iitwayo Zamani Zanzibar Kempinski” alisema Omar.
Alisema kimsingi mkataba ulitaka awasilishwe chemba ya wanasheria katika afisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kutimiza matakwa ya kisheria na baadae kutolewa taarifa rasmi katika vyombo vya umma kama inavyotajwa katika kifungu cha 29 (8).
Alisema majengo ambayo yalikuwa na afisi ya serikali na yakitumiwa na Afisi ya Mrajis Mkuu wa nyaraka Zanzibar,Afisi ya Wakfu na Mali ya Amana, Afisi ya Shirika la Meli, Afisi ya Mrajis Msajili wa Makampuni, Jengo la Starehe Club pamoja na eneo la wazi lililopimwa kisheria, majengo hayo ya umma yaliyopo mtaa wa Mambo Msige Wilaya ya Mjini Zanzibar.
“Vyama vyetu vimeshutuswa na uuzaji wa majengo pacha ya serikali ukizingatia kuwa majengo hayo yalipatikana baada ya kutaifishwa na serikali chini ya sheria the confiscation of immovable properties decree no 9 of 1964” imesema wamesema viongozi hayo.
Wananachi wa Zanzibar wanapenda kuelewa sababu zilizofikiwa hadi kuuzwa kwa majaengo hayo wakati yanafaa kutumika kwa shughuli za utawala wa Serikali pamoja na mambo mengine muhimu.
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali alishindwa kutoa taarifa kwa umma hata baada ya mkataba wa mauzo kuandikiwa baina ya Serikali na mwekezaji hali ambayo inatia mashaka zaidi kuona kuwa mkataba huo hauna maslahi kwa umma na kwa wazanzibari.
Hata hivyo viongozi hao wa vyama vitatu Ali Omar Juma NCCR, Juma Ali Khatibu TADEA na Said Soud Said AFP wameishauri Serikali chini ya kifungu cha 41(2)(a)(b)(3)(a) kusimamisha ujenzi unaoendelea kufanywa na Kampuni ya mwekezaji Zamani Kempinski.
Vyama hivyo wameishauri Serikali ihusike kutangaza rasmi kuvunja mkataba uliofikiwa juu ya uuzwaji wa majengo hayo pamoja na eneo la wazi kwa vile yamesababisha hasara kubwa kwa umma.
Majengo hayo ya umma yametoa huduma na mchango mkubwa sana katika ustawi wa Zanzibar ambapo Wazanzibari wote wanafahamu na kuamini kuwa majengo hayo ni uti wa mgongo wa taifa pamoja na kuigizwa katika ramani ya dunia na historia ya urithi wa kimataifa.
Aidha wazanzibari wameridhika namna wanavyopata huduma za vyeti vya kuzaliwa na huduma nyengine muhimu na kwa vyovyote uuzwaji wa majengo hayo ulitakiwa uratibiwe na kupata baraka za umma.
“Hali hiyo imesababisha wananchi kujenga khofu ya kuona kuwa sheria hazikuzingatiwa katika uundwaji wa mkataba wa mauzo ya majengo hayo pamoja na eneo la wazi hapo Forodhani, unaashiriria kuwepo mazingira ya udanganyifu na rushwa na hayo yamekatazwa na sheria ya mauzo ya umma katika part V kifungu cha 41 (1)” alisema kiongozi huyo ambaye aliongea kwa niaba ya wenzake.
Vyama hivyo vimewaomba wajumbe wa baraza la wawakilishi kuandaa hoja binafsi na kuiwasilisha katika baraza la kutunga sheria ili indwe tume huru ya uchunguzi itakayopewa jukumu la kuchunguza mkataba tata (ambigious contract) baina ya serikali na mwekezaji.
Wamesema tume hiyo iwe huru kufanya shughuli zake na ipewe wajibu wa kuchunguza kwa kipindi cha miezi mitatu, na ripoti ua uchunguzi iwasilishwe katika kikao cha baraza la wawakilishi septemba 2011 na tume hiyo iundwe pamoja na kuwashirikisha wanasheria kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali pamoja na taasisi mbali mbali na wananchi wahusike katika uchunguzi huo.
“Tunaamini baraza la wawakilishi lina wajibu mkubwa kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ibara ya 78(3) na ibara 88(a) (b)(c) ambapo wawakilishi wana wajibu wa kuandaa ripoti ambayo itakuwa ni muongozo na sheria kwa umma kwa ajili ya kupata ukweli wa jambo hilo.

No comments:

Post a Comment