Sunday, May 1, 2011

SEREKALI ZA MSETO HAZIKUANZA SASA ZANZIBAR

napongeza sana aliye andika habari au stori hii ili tu kunavipengele ambavyo hukutaka kuvitaja kwahiyo mimi nimevitaja ili kuweka wazi kila moja anufaike na historia ya zanzibar nchi ya amani na upendo
mungu ibariki zanzibar yetu daima
          
USIKU wa  kuamkia Januari 12, 1964 kundi la watu 300 walikitwaa kisiwa cha Unguja wakiongozwa na mtu asiyekuwa maarufu kipindi hicho, aliyekuwa akiitwa John Okello, Okello alikuwa akiishi Pemba ambako alitokea Uganda miaka michache tu.

Ndani ya Zanzibar Okello alipata umaarufu kwa vijana majabari, wengi wao wakiwa ni makuli na wachukuzi wa meli zilizoingia na kutoka bandarini Zanzibar.  Walikuwa wakikutana naye kufanya vikao vya siri.

Okello aliwapa matumaini ya mabadiliko wafuasi wake hawa, ambao walikuwa wakifanya kazi pamoja kwa muda mrefu, mara nyingine katika mazingira ya hatari, na tayari kufuata amri za kiongozi yeyote ambaye ataweza kuwalipa.

Machafuko ya kisiasa yalikuwa yakiongezeka ndani ya unguja na Pemba tangu kifo cha Sultani Khalifa mwaka 1960.
Sultani Khalifa alitawala Zanzibar kwa karibu ya miaka 50, tangu mwaka 1911. Baada ya udanganyifu mkubwa kwa majimbo ya uchaguzi na mseto katika chaguzi kuu mbili za mwaka 1961, vyama vikuu vya ASP na ZNP vilishindwa kujipatia wingi wa kura kwa kila kimoja.

Lakini katika uchaguzi wa mwisho wa 1963, ZNP na ZPPP viliunganisha nguvu na kukishinda ASP kwa viti vya Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) na kuunda Serikali ya Mseto kwa sasa tunasema GNU AU SUK  ya ZNPP/ZPPP, chini ya Waziri Mkuu wa Kwanza, Mohamed Shamte.

ZPPP ni chama kilichoundwa mwaka 1960 baada ya mtafaruku wa kiuongozi ndani ya ASP na kusababisha kundi moja, likiongozwa na Mohamed Shamte kutoka Pemba, kujiengua.

Waingereza waliondosha majeshi yao hapo nchini zanzibar kikiwemo kikosi maalumu cha Kiarishi ambacho kilikuwa kimewekwa karibu na uwanja wa gofu na mpaka wa mji mkongwe mapema mwaka 1963. Wakati mfalme mpya, Jemshid  akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar tarehe 10 Desemba 1963,mfalme mpya alitaka Gavana wa kiingereza kuondoka zanzibar na kuwa mwisho wa ukoloni zanzibar.

Taifa hilo la Zanzibar baada ya uhuru lilikuwa mwanachana kamili wa Jumuiya ya madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.

Wakati huo Zanzibar ilikuwa ikichemka kisiasa. Watu kwa makundi walikuwa wakijadiliana kuhusu haki dhidi ya  fursa, wageni dhidi ya wenyeji, ubepari dhidi ya ujamaa, wafanyabiashara dhidi ya wamiliki ardhi, zanzibar thaidi ya tanganyika watu ambao ni watanganyika waliokuwa wakifanya kazi wakati wa karafu walitaka haki zao pia sawa na wazanzibar , Waasia dhidi  ya pazia la nyuma  la vita baridi na harakati za utaifa na kuondosha ukoloni ambazo zilikuwapo kipindi hiki ndani ya Afrika.

John Okello hakuwa na jawabu ya mambo haya nyeti, lakini alikuwa na kipawa cha kutambua kwamba vikundi hivi vinavyoshindana vinatoa nafasi nzuri kwa mtu wa harakati kama yeye Okello.

Januari 12, 1964 akiwa anaungwa mkono na asilimia kubwa ya watu waliokuwa wakitokeya tanganyika na kuweka makazi yao hapa zanzibar na wengi wao wakifanya kazi za kuchuma karafu na kathalika, Okello na kikosi chake waliipindua Serikali ya Mohamed Shamte.

Inaelezwa kuwa takriban watu 10,000 waliuawa, licha ya kwamba kikosi cha Okello kilikuwa na silaha duni. Okello na kikosi chake walilishangaza Jeshi la Polisi Zanzibar na kuchukua ofisi zao.

Kwenye hotuba yake iliyotangazwa kwa njia ya redio, Okello alitangaza kuwa yeye ni ‘Field Marshal’ wa unguja na Pemba’ na alimwamuru Sultan aue familia yake na kisha ajiue mwenyewe, la sivyo Okello ataifanya kazi hiyo mwenyewe.

Kutokana na kufanikiwa kwa Mapinduzi hayo, Okello alitangaza Baraza la Mapinduzi na Sheikh Abeid Amani Karume kuwa Rais. Kiongozi wa Chama cha Umma, Abdulrahman Mohamed Babu, akawa Waziri Mkuu. Baadaye alikuja kuwa Makamu wa Rais.

Sheikh Karume na Babu hawakuwa wamejulishwa kuhusu mapinduzi hayo ya kijeshi kwani wote walikuwa Tanganyika, lakini walirudi Zanzibar walikokaribishwa na Okello.

Lakini pamoja na shughuli yote aliyoifanya si Karume wala Babu waliomhitaji tena Okell,o aliondoka kuelekea Tanganyika na kuanzia wakati huo alizuiwa kurudi Zanzibar na alipigwa marufuku pia asionekane Tanganyika na Kenya.

Baada ya Okello kupigwa marufuku Zanzibar na Tanganyika, aliishi maisha ya kuhama hama kutoka nchi moja hadi nyingine. Aliishi Kenya na baadaye Congo Kinshasa na Uganda. Aliwahi kufungwa mara kadhaa na mara ya mwisho alionekana akiwa na kiongozi wa Uganda mwaka 1971 na baadaye alipotea.

Inadhaniwa kuwa Iddi Amin alimwona Okello kuwa ni tishio kwake na mara nyingine inaelezwa kuwa baada ya Amin kujipandisha cheo na kuwa Filed Marshal, inaelezwa kuwa Okello alisema kwa dhihaka, “Uganda hivi sasa ina Field Marshal wawili.
Hata hivyo inaelezwa kuwa Idd Amini alipanga mipango ya mauaji dhidi ya Okello, lakini pamoja na hali hiyo kifo chake kimebakia kuwa ni cha utata.

Okello ni nani?
John Gideon Okello alizaliwa mwaka 1937 wilayani Lango, Uganda. Ni mwanamapinduzi asiye na kifani barani Afrika.
Alianza kuishi maisha ya uyatima akiwa na miaka 11. Alipofikisha umri wa miaka 15 aliondoka nyumbani kwao na kwenda kutafuta ajira katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki.

Kuanzia mwaka 1944 alifanya kazi nyingi ikiwa ni pamoja na ukarani, mtunza bustani na shughuli mbalimbali. Alijifunza kufanya biashara ya kuuza matofali na baadaye alimudu kufanya kazi ya uashi, lakini alikamatwa mjini Nairobi, kutokana na sababu ambazo hazikuelezwa. Alifungwa miaka miwili gerezani. Kifungoni ndicho kilichomfanya awe na fikra za kimapinduzi.

Mara nyingi umekuwapo uvumi kuwa huenda Okello alikuwa amepata mafunzo yake nchini Cuba, lakini jambo hili halikuwahi kuthibitishwa na Okello mwenyewe.

Baada ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zanzibar iliendelea kutawaliwa na Abeid Karume na chama chake cha ASP.
Haikuchukua muda mrefu kwani April 26 mwaka huo huo, Karume na Mwalimu Nyerere waliunganisha Zanzibar na Tanganyika zikawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo utawala wake unaelezwa kuwa wa kibabe na wa kikatili kwa wote walioonyesha nia ya kupingana naye. Katika kipindi cha miaka minane aliyokaa madarakani, Zanzibar haikuwa na Katiba wala chama cha ASP hakikuwahi kufanya mkutano mkuu. Hata kifo chake cha mwaka 1972 kinaelezwa kutokana na watu ambao hawakuridhishwa na utawala wake.

Mrithi wa Karume, Aboud Jumbe ndiye aliyeleta mabadiliko ndani ya ASP na serikali yake. Kwanza alifungua milango ya kuundwa kwa Katiba ya Zanzibar, akaruhusu kuwepo kwa mikutano ya ASP na kutoa fursa kwa Wanzanzibari kwenda kusoma masomo ya juu nje ya Zanzibar.

Jumbe alishiriki kuziunganisha TANU na ASP na kuunda CCM mwaka 1997.
Hata hivyo Jumbe naye hakudumu madarakani, kwani mwaka 1984 alienguliwa na Kamati Kuu ya CCM baada ya kutofautiana na Mwalimu Nyerere hasa katika masuala ya Muungano.
Mivutano zaidi iliendelea ndani ya CCM Zanzibar ambapo ilifika mahali baadhi ya makada wa chama hicho walifukuzwa akiwamo Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake.

Kufukuzwa kwao kuliunda tabaka ambalo baadaye lilikuja kuunda chama cha upinzani chenye nguvu visiwani humo yaani CUF baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa mwaka 1992.

Tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995, 2000 na 2005, chama hicho kimeonyesha upinzani dhidi ya CCM visiwani humo. Chama hicho kimekuwa kikidai kudhulumiwa ushindi wake hata kufikia kususia vikao vya Baraza la Wawakilishi na kuandamana kupinga wizi wa kura.

Kulifanyika juhudi mbalimbali za kukipatanisha chama hicho na CCM kwa majadiliano ya mwafaka lakini nayo hayakufanikiwa.
Maridhiano
Lakini mwaka 2010, aliyekuwa Rais wa Zanzibar Amani Karume alimwita Katibu Mkuu wa CUF Ikulu ya Zanzibar na kujadiliana namna ya kuumaliza mgogoro huo na kutafuta maridhiano.

Baada ya majadiliano hayo, Katiba ya Zanzibar ilifanyiwa marekebisho na kuunda mfumo wa serikali shirikishi.
Ndipo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Dk Mohamed Ali Shein wa CCM alichaguliwa kuwa Rais na Seif Sharif Hamad wa CUF aliyeshika nafasi ya pili akapewa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi ya Makamu wa Pili akapewa Balozi Seif Idd wa CCM.

Huo ndiyo umekuwa mwanzo wa visiwa hivyo kuwa na mwafaka wa kisiasa baada ya makundi mbalimbali ya wanasiasa visiwani humo kusigana kwa muda mrefu.
Imeandaliwa na Elias Msuya kwa msaada wa mtandao

No comments:

Post a Comment