Thursday, May 19, 2011

SHEIN ASEMA. SITOSITA KUMFUKUZA MTU....?

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na Viongozi wa Serikali na watendaji wakati wa mkutano wa majumuisho ya Ziara kwa Mkoa wa Mjini Magharibi,katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbweni.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, amesema hatoacha kuwachukulia hatua ya kuwatimua kazi maafisa na watendaji wa serikali wanaozembea kazi zao na kushindwa kutekeleza majukumu waliopewa.
Dk Shein amesema kabla hajaanza kazi ya kuwatimua wale wote wanaojihisi hawawezi kutkeleza majukumu yao waanze kujiondoa haraka kabla hajachukua hatua yeye ya kuwaondoa kwa kuwa wanashindwa kuwatumia wananchi jambo ambalo ni wajibu wao.
“Nasema kwa dhati ya moyo wangu kwamba aliyekuwa hawezi aondoke mwenyewe aje aninong’oneze nimuondowe nimuweke mwengine kwani haiwezekani mtu anaingia kazini saa tatu kisa anakaa anapiga barza, kisha kidogo anaaga anaenda sokoni akirudi tena anaaga anakwenda nyumbani hivi sivyo na haiwezekani kulea maafisa wa namna hii ” alisema Dk Shein.
Kauli ya Dk Shein mekuja siku chache baada ya kuhitimisha semina elekezi kwa viongozi wa taasisi mbali mbali za serikali ambapo walipewa mafunzo ya uwajibikaji kwa siku tatu mfululizo kwa lengo la kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Dk .Shein, alitoa kauli hiyo jana katika kikao cha majumuisho ya ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Mjini Magharibi, mapema wiki hii, kwa kukagua shughuli za maendeleo za Mkoa huo katika Sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na shughuli za kijamii.
Kikao hicho kiliwashirikisha watendaji wakuu wa serikali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Masheha, na baadi ya watendaji katika taasisi mbali mbali za serikali na Vyama.
Alisema anachohitaji kukiona katika serikali anayoiongoza ni kwa watendaji wa taasisi zote wakiwemo masheha wanatoa huduma bora kwa wananchi na yeyote ambaye atashindwa kuwahudumia wananchi basi anaweza kujiondoa kabisa kabla ya kuondolewa kwani huko ndio kuwajibika katika serikali.
Aidha Dk Shein katika ziara yake hiyo ambayo ametembelea sehemu mbali mbali za Mji wa Zanzibar ameelezea kusikitishwa kwake na mji huo ambao ni mchafu na hauna mvuto kwa watu wanaokuja kutembea Zanzibar ambapo inaipa sifa wananchi wa ndani na wageni wanaokuja kutembelea visiwa hivi.
Alisema uchafu ulivyokithiri katika maeneo ya Mji wa Zanzibar kama kwamba mji hauna wenyeweau hauna kiongozi wa kuongoza jambo ambalo wamewataka viongozi waliopewa jukumu hilo kutekelez amajukumu yao haraka.
“Imenisikitisha sana hali ya Mji wa Zanzibar ni mchafu sana imekuwa nchi kama haina kiongozi aliyepewa jukumu kuliongoza Baraza la Manispaa kutokana na taka kuzagaa kila pembe, wanyama wanaachiwa wanatembea ovyo katika mji ni jambo baya sana na linatia aibu kwa wenyewe na wageni” alisema Dk Shein.
Dk Shein alisema imekuwa ikiionesha picha ya Mji wa Zanzibar kama kwamba hauna mwenyewe na ni vyema waliopewa majukumu kusimamia shughuli za usafi na kuutengeneza ili uonekane msafi na wenye kuvutia la sio hivyo basi wahusika watakuwa wameshindwa kazi na wanapaswa kukaa pembeni na kuwaachia wengine wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Amewaambia maafisa hao kwamba kamwe hatukuwa na muhali katika suala hilo kwa maafisa na watendaji wote wa serikali hivyo watendaji waanze kuliona hilo mapema kabla hatua za lazima hazijachukuliwa nay eye mwenyewe kwa kuwateuwa watu wapya vijana na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa ari na nguvu zaidi.
“Nasema mapema katu sitokuwa na muhali na mtu kwani uwezo wa kumtafuta mwengine na kumrithisha kazi hizo bado ninao na haiwezekani nikawa nasema ama kusisitiza jambo hilo hilo hilo kila siku bila ya kufanyiwa kazi” alisema huku akioesha kukasirishwa na hali hiyo..
Alisema katika Utafiti uliofanywa juu ya utendaji wa kazi kwa Wananchi wa Zanzibar umeonesha kuwa wafanyakazi wa serikali wanafanya kazi masaa matatu badala ya manane ambayo walitakiwa kuwajibika kisheria jambo ambalo hatuweza kulivumilia chini ya utawala wake.
Watendaji hao licha ya kufanya kazi muda wa masaa matatu wamekuwa wakipokea mishahara yao kamili bila ya kukatwa zile siku ambazo hawafanyi kazi walizopangiwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na serikali.
Watendaji hao wameelezwa kwamba jambo ambalo linatakiwa ni kuwatumia wananchi na kushughulikia majukumu yao waliopewa kikamilifu na sio kuzembea kwani kupewa jukumu kama kiongozi ni suala ambalo linahitaji kufanyiwa kazi na sio kujifakharisha kwamba wamekuwa mabosi tu.
“Suala la kuwa tumekuchagueni kuwa mabosi na mkaazi kujikweza kwa kuitwa mabosi tu bila ya kutoa huduma na kufanya kazi kwa umakini na kutekelez amajukumu nadhani hiyo sio dhamira ya kupewa uongozi, uongozi ni kuwajibika sijakupeni nafasi muwe mabosi tu maana mabosi wasiokuwa na tija yoyote hawana maaana” aliongeza Dk Shein huwa watendaji hao wakiwa kimya kumsikiliza.
Dk. Shein, alisema ikiwa watendaji hao watashindwa kuwajibika watambue kuwa ipo hatari kwa serikali kuchekwa na mataifa mengine pamoja na wahisani wanaotowa fedha zao kwa ajili ya kuipatia Zanzibar ili ibadili Mji wake.
Hivi karibuni Zanzibar imepewa mkopo na Benki ya Dunia wa dola za kimarekani milioni 38 ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 56 za kitanzania kwa ajili ya kuubadili Mji wa Zanzibar Chini ya mradi utaosimamiwa na Baraza la Manispaa.
Dk Shein alisema fedha hizo walizopewa zinahitaji kuonekana matunda yake lakini watendaji waliopewa kazi hiyo watashindwa kuifanya kazi hiyo wajue kuwa wataitia aibu serikali na hatimae kuonekana serikali ya umoja wa kitaifa haijaleta matumaoni yoyote kwa wananchi.
Chini ya serikali ya umoja wa kitaifa Dk Shein alisema kamwe hawezi kakaribisha masimango na kicheko kutoka kwa mataifa ya nje wala hatuvumilia kuona Zanzibar inarudi nyuma katika maendeleo kwani haiwezekani serikali ikawa inalipa madeni ya mikopo lakini huku kukiwa hakuna kilichofanyika kutokana na watendaji wasiotaka kubadilika.
Alisema Zanzibar wanaopewa majukumu wanalazimika kutambua Zanzibar sio ya mtu mmoja ambaye amepewa jukumu la kuiongoza taasisi bali wajue kuwa wanawawajibikia watu milioni 1.5 ambao waliichagua serikali yao kuwaongoza.
“Msisubiri kuitwa kuulizwa kazi zenu mnavyozifanya lazima muwe tayari kujituma wenyewe kwa kushirikiana mbadilike kwa kufanyakazi kwa bidii tunataka maendeleo sio kukaa bila ya kuandaa mipango ya maendeleo” alisema Dk. Shein.
Alisema katika serikali yake hivi sasa kuna baadhi ya viongozi tayari wameonekana kutekeleza majukumu yao vizuri lakini wengine bado na ni lazima kuona sasa wanabadilika ili waende pamoja na serikali yao.
Alisema maelezo yake hayo hayana lengo na kumtisha mtu kwani haiwezekani kuona watu wanaitwa waheshimiwa lakini upande mwengine wanashindwa kuwa na heshima mbele ya jamii na ni lazima hivi sasa waanze kujiheshimu ili waheshimiwe na taifa zima.
Dk .Shein, alisema ikiwa watashindwa kujenga tabia hiyo hasa kwa viongozi katika majimbo wakiwemo wawakilishi na wabunge kutambua wapo katika hatari kubwa ya kuachwa na wananchi katika uchaguzi ujao hivyo aliwataka uwajibikaji ufanyike.
“Viongozi wachukuwe jukumu lao wanapokwenda majimbo yao wachangieni wananchi sio kujidai hawana, hawana tuu basi muwe hamna hata za kujidai Wawakilishi, Wabunge wananchi wanataka kuwaona jidaini hivyo hivyo kwa hicho kidogo sio tunaishi kwa jeuri kwani siku zinayoyoma na uchaguzi unakaribia mtakuja kuangushwa na ubakhili wenu” alisema Dk Shein.
Katika ziara yake ilioanza wiki hii ambapo alitembelea maeneo kadhaa ya Mji wa Zanzibar na kujionea hali halisi ya shughuli za sekta alizozitembelea alisema kwa kiasi kikubwa zimeonesha kuwapo kwa hali nzuri hasa katika eneo la kilimo kutokana na kuanza kujiandaa na kilimo cha kisasa.
Alisema serikali itahakikisha inakabiliana na changamoto zote zilizojitokeza katika sekta hiyo ikiwa pamoja na kuliangalia suala la kuwapatia ruzuku wakulima kama baadhi ya mataifa ya ulaya na Tanzania bara wanavyofanya kwani tayari mazingatia hayo yamo katika Bajeti ya Zanzibar ijayo.
Aidha aliahidi serikali yake kusimamia zaidi kituo cha utafiti cha kilimo kinaimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa huku kikikuziwa mitaala yake kufikia ngazi ya shahada na kuwapongeza kwa kupata mbegu mpya ya mpunga ambayo itaweza kuongeza kiwango cha chakula nchini.
Hata hivyo Dk. Shein, ameagiza watendaji katika shirika la Umeme kuona wanavipatia huduma ya umeme kwa haraka vituo vya kilimo kwa ajili ya kusukumia huduma za maji na kuonya watendaji hao kuacha kutumia vyeo vyao kwa kujiona kama wao ndio wao na kufanya kazi kwa mitazamo yao binafsi.
“Tatizo la watendaji wetu wanataka waonekane yeye ndio mwenyewe tu hapo alipo hivyo sivyo mnaharibu kwani hili mkilifanya halimnufaishi mtu mmoja ni la wengi kaeni pamoja mlete mabadiliko ya kilimo kwani umeme ukifika wengi watafaidika na kilimo kitaimarika” alisema Dk Shein.
Kuhusu sekta ya Afya Dk Shein, alisema maendeleo yake yameonesha mafanikio ya msingi katika ujenzi wa majengo ya vituo vya daraja la pili na kuitaka Wizara hiyo kuona inajiandaa kuweka utaratibu wa kuchangia gharama za ujenzi katika hatua ya kumalizia baada ya wananchi kujitolea kama inavyotekelezwa katika sekta ya elimu.
Upande wa Elimu Dk Shein alisema serikali imeridhishwa na hatua ya ujenzi wa mradi wa skuli ya Wilaya kwani utawezesha kutimiza lengo la serikali katika kuinua sekta hiyo kutokana na skuli hizo kujengwa kila Wilaya.
Dk. Shein alikamisha ziara yake jana ambapo awali alitembelea kituo cha Afya cha Mpendae, Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani, Skuli ya Chekechea ya Meya, Uwanja wa Mnazi mmoja, Bwawa la Hoteli ya Bwawani, Bonde la Mpunga Mtwango na Bumbwisudi, Hospitali ya Mbuzini, Kukagua uwanja wa Timu ya Bweleo na Skuli ya Maandalizi ya Bweleo.


Mimi nafikiri kama shein haelewi au labda hajuwi au labda anajuwa ila anataka kufurahisha wananchi maana anajuwa ashawauthi pale alipouza jengo la mambo msige. kisha akasema mtu akiuza chake hulizwa sasa labda anajaribu kujiweka msafi kabisa kabla wananchi hawajamaliza ila mimi nataka kukuliza hapo juu umesema kama hawafanyi kazi zao vizuri kuna vijana tele ambao watafanya kazi kwa ari sasa ulipochanguliwa kuwa raisi kwanini hukuwachanguwa hao vijana...? ili znz iweze kujijenga mbona ukanza na kuapisha watu wale wale waliyokuwepo toka mzee karume mpaka leo na hawana moja wanalolofanya. je unafikiri hiyo hutuba yako ya nusu saa au saa moja kweli itawamsha hao na wao washazoweya kutwepereka hiyo manispa unaipa mamillioni kwa mamillioni toka anzi za comando waliletewa malori ya kubeba taaka za mji mzima na taka zilikuwa zikika hapo michezani mpaka mafunza na panya wakafanya ndio nyumba yao na yale malori hatukujuwa mwisho wake shein shein karibu znz hilo tu ndio nitakalo kuambiya karibu znz hawa dawa yao ni moja tu. waulize miaka yote uliyo changuliwa umefanya nini kwa wananchi hawana jawabu timuwa weka kijana shupavu ndio utawaweza lakini unasema kama hamukufanya kazi vizuri nitawatimuwa utafikiri mwalimu mkuu na wanafunzi wake shuleni ukirudi ofisini wao wanaendeleya kucheza ndivyo ilivyo na kama huamini sawa miaka mitano itakwisha na hakuna moja litakalofanywa.

No comments:

Post a Comment