Sunday, May 1, 2011

WAZANZIBAR TUSIKUBALI SEREKALI TATU WALA NNE JAMBO MOJA TU WAZANZIBAR WAPEWE NCHI YAO WAJITAWALE WENYEWE.

TATIZO kubwa la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kwamba hauna watetezi.
Ni rahisi kumtetea fisadi kuliko kuutetea Muungano. Watu wa Zanzibar wanasema wamechoshwa na watu wa Bara wanasema wamechoka. Viongozi waliopewa uongozi wa Taifa hawana msimamo unaojulikana zaidi ya kuzungumzia “kero kero kero” na kwa miaka 47 sasa wamebakia kuongeza matatizo zaidi wakifikiria wanapunguza kero.
Muungano hauna watetezi si kwa sababu hauteteeki bali ni kwa sababu ni vigumu kuutetea hasa kama hakuna watetezi. Juhudi zote ambazo mtu yeyote anaweza kuziona kwa uwazi ni kuwa tunaelekea kuuvunja Muungano na niwe wa kwanza kusema wazi kuwa kama hakuna watetezi wa Muungano hatuna budi kuuacha uvunjike ili hatimaye Muungano bora uweze kuja.
Hatuwezi kuendelea hivi tulivyo sasa kwani msukumo wa mabadiliko umefikia mahali ambapo hakuna jinsi yoyote nyingine isipokuwa kuweka utaratibu wa wazi, wa makusudi na usio na mawaa ambao utasimamia mchakato wa kuvunja Muungano wetu. Naam, nimelisema lile ambalo wengine wanalifikiria.
Hatutaki Serikali Tatu
Msiniulize mimi na nani. Lakini ukweli ni kwamba wanaozungumzia suala la serikali tatu wanajaribu tu kutafuta njia ya mkato ya kutatua tatizo la Muungano wa sasa. Kwa hiyo hawa baada ya kufikiria sana wakaona kuwa na serikali tatu kutatatua tatizo la serikali mbili.
Yaani, kuna watu wanafikiri kabisa kuwa tukiongeza serikali ya tatu (wenyewe wanaiita ya Shirikisho) basi tutapunguza tatizo la kuwa na serikali mbili yaani za “Muungano” kana kwamba kuitwa “Shirikisho” kunatosha kuondoa matatizo ya “Muungano”.
Aidha sisi ni watu tusiofikiri sana au ambao tumezoea kujiongezea matatizo zaidi tukiamini tunapunguza. Fikiria badala ya kujitahidi kuondokana na misongamano ya wagonjwa kwenye wadi zetu za wazazi tunataka kujenga mabarabara ya juu kwa juu!
Badala ya kuboresha shule zetu nyingi na kuzileta kuwa za kisasa tumeenda na kuongeza matatizo zaidi kwa shule lukuki huku tukijivunia tuna “Sekondari za Kata” ambazo sijui kama kuna waziri, naibu waziri au mbunge hata mmoja ambaye mtoto wake anasoma huko! Tuna uwezo mkubwa zaidi wa kujiongezea matatizo – na hili limefikia hadi kwenye suala la Muungano.
Mwalimu Julius Nyerere alilisema hili vizuri sana kwenye “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania” alipojaribu kuhoji hili suala la serikali tatu lina mantiki gani hasa? Alisema hivi katika kitabu hicho ambacho kinatakiwa kisomwe na kila mtu anayetaka kutoa mawazo yake juu ya mfumo wa Muungano tunapoelekea Katiba Mpya.
Alisema Mwalimu: “Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zan­zibar na ukubwa wa Tanganyika. Zan­zibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tutuhumiwe, hata kwa makosa, kwanba tunaanzisha ubeberu mpya!
“Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzi­bar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tan­ganyika ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tan­ganyika ingeendesha Serikali yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.”
Nyerere alionyesha kuwa kuunda serikali tatu kungeongeza matatizo zaidi. Na akaendelea hapo hapo na kusema “Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tan­ganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tan­ganyika.”
Ndugu zangu, ndio maana hata mimi siamini katika serikali tatu. Tunaweza kuwa na mfumo wa Upili (dual government system) kama uliopo Marekani, lakini hatuwezi kuwa na mfumo wa serikali tatu na tukafikiria tumepunguza matatizo.
Hivyo, kufikiria kuwa tukiwa na serikali tatu basi mambo yatakuwa mazuri zaidi ni kudanganyana tu. Sababu zilizotufanya tukatae serikali tatu mwaka 1964 bado zipo na zina nguvu nadhani sasa hivi kuliko wakati ule.
Kuelekea nchi mbili huru au kuelekea nchi moja yenye serikali mbili au zenye mfumo wa upili au kuelekea nchi moja yenye mifumo miwili?
Hatuwezi kuendelea tulivyo sasa. Mfumo uliopo sasa hivi hauwezi kabisa kutatua matatizo ya msingi ambayo yamedumu kwa muda mrefu ambayo tumeyaita kuwa ni “kero”. Ndugu zangu kilichopo sasa hivi katika Muungano si “kero” bali ni matatizo – matatizo ambayo yanatishia uhai wa Muungano wetu.
Kuna njia nne ambazo tunaweza kuzielekea – njia ya serikali tatu kwangu haipo wala siifikirii.
*Kuelekea nchi mbili huru – Hii itakuwa ni njia ya kurudisha uwezo kamili wa kujitawala wa nchi za Tanganyika na Zanzibar.
Maana yake ni kurudisha kilichokuwapo kabla ya Aprili 26, 1964. Binafsi ninaamini ni njia bora zaidi ambayo inaweza ikazaa muungano bora zaidi. Ukifikiria sana utaona kuwa kurudisha nchi hizi mbili si jambo gumu sana sasa hivi kwani tayari kuna vyombo na mifumo ya utawala ambayo imekuwapo kwa muda.
Kazi kubwa hata hivyo nadhani itakuwa kwenye kuamua mambo mbalimbali kama nani anapata nini na kwanini. Mara zote sehemu moja ya nchi inapotaka kujitoa basi ugumu mkubwa zaidi hauko katika kuunda vyombo mbalimbali bali katika masuala makubwa mawili: a. inapata kitu gani kutoka kwa ile nchi nyingine na pili, inahusiana vipi na hiyo nchi nyingine. Hili nitaliangalia siku nyingine kwani binafsi naona ndiyo njia pekee ya kuiokoa Tanzania.
*Kuelekea nchi moja yenye serikali mbili – mfumo huu ndio uliopo sasa. Pamoja na maneno kuwa “Zanzibar ni nchi” ukweli uko wazi kuna nchi moja tu inaitwa Tanzania. Katiba ya Muungano inasema hivyo na kuwa kuna serikali mbili yaani ya Zanzibar na ya Muungano. Kuudumisha huu ulivyo sasa ni kuendelea na matatizo. Kwa hiyo sitajadili sana hili.
*Kuelekea nchi moja yenye mfumo wa Upili (dual government system); mfumo huu unaweka madaraka ya juu ya utawala (sovereignty) kwenye serikali kuu na chini yake kuna serikali nyingine za majimbo ambazo zinahusiana na serikali kuu katika mfumo unaoleweka na kuongozwa na Katiba ya Taifa.
Mfumo huu ndio ulioko Marekani, kwa mfano, ambapo huwezi kusema ni nchi yenye serikali 50 ati kwa vile kila jimbo lina serikali yake vile vile. La hasha bali kuna mfumo wa Federal Government (Serikali ya Shirikisho) na Serikali ya Jimbo (State Government). Na ndani yake pia kuna mifumo mingine ya serikali za Makabila ya Wazawa ambayo nayo yanahusiana na Serikali Kuu kama ilivyo serikali ya Jimbo japo utaona kuwa baadhi ya makabila hayo nayo yamo kijiografia ndani ya majimbo fulani fulani. Uzuri wa mfumo huu kwetu ni kuwa utasaidia sana katika kuiunganisha Afrika ya Mashariki.
*Kuelekea nchi moja yenye mifumo miwili. Kama Tanzania haitataka kuungana na nchi nyingine za Afrika na inataka kutatua matatizo yake ya Muungano yawezekana mfumo huu ambapo kuna serikali moja ya kitaifa na chini yake kuna mifumo miwili ambayo inauhuru mkubwa kwa Zanzibar kuliko hata ilivyo sasa.
Mfano mzuri ni kama nchi za Canada na jimbo lake la Quebec au hata China na Hong Kong. Japo kuna historia tofauti kati ya sehemu hizo kimsingi serikali kuu za nchi hizo zimekubali madai na utofauti wa majimbo hayo kiasi cha kuruhusu mifumo miwili kabisa tofauti japo baadhi ya mambo ya msingi yameachwa kwenye serikali kuu.
Hili sijui litafanyika vipi kwa Tanzania kwani msingi wake mkubwa ni Zanzibar kukubali isiwe nchi huru na kuachilia mambo kadhaa kwa serikali kuu lakini ikabakia na utambulisho wake.
Hata hivyo kuna njia moja ya tano ambayo Nyerere aliizungumzia na ambayo kimsingi ingekuwa ni njia bora zaidi lakini tatizo lake ni kuwa lingefanya kile ambacho Nyerere alikihofia mwaka 1964 yaani kuunda Nchi moja na taifa moja. Kuelekea nchi moja ni jambo gumu na lisilowezekana.
Tatizo lilipo hata hivyo ni jinsi gani tunataka kuuvunja huu Muungano? Kuna njia moja ya uhakika nayo ni kuitishwa kwa kura ya maoni. Binafsi siamini kama Tanzania Bara wana tatizo hilo la Muungano kwani hawatishiwi lolote na uwepo wa Zanzibar ndani ya Muungano kinyume na watu wengine wanavyoweza kufikiria.
Tanzania Bara wanaweza kuishi na uamuzi wowote ule ambao Zanzibar itachukua na nina uhakika hata ikitaka inaweza kulipia mambo fulani fulani ya Zanzibar ili kuipa mwanzo mzuri wa kuwa taifa huru.
Hivyo, kabla hatujaweza kuandika Katiba Mpya ni lazima tutatue tatizo la Muungano. Mfumo wa Muungano si sehemu ya mijadala ya Katiba Mpya bali maamuzi ya wananchi wa Zanzibar ndiyo yatakayoamua nini kiwemo kwenye Katiba hiyo Mpya.
Hivyo, naamini wakati umefika kwa Wazanzibar kutangaza wazi na wachukue azimio kupitia Baraza la Wawakilishi au hata kwa kuanza maandamano ya kuishinikiza serikali yao kutangaza nia ya kuwa nchi huru. Nina uhakika watasikilizwa.
Na muda ukifika (natumaini kabla ya 2015) wanachi wa Zanzibar waulizwe swali moja tu nalo ni “Je Zanzibar ibakie kwenye Muungano wa Tanzania au ijitoe ifikapo mwaka x?”
Wakisema ijitoea uamuzi wao uheshimiwe, taratibu zianze kupangwa za jinsi Zanzibar itakavyotoka kwenye Muungano. Watakaoshangilia washangilie na watakaolia walie. Zanzibar iliwahi kuwa nchi na imewahi kuwa himaya na ina historia kubwa tu ya utawala.
Wakisema wabakie taratibu zianze kufanyika za namna gani kuunda Muungano huu ili kuondoa kelele za pande zote mbili ili tusije kuwaachia watoto wetu kazi nyingine ya kujaribu kuuokoa Muungano.
Yote haya yatafanyika kwa sababu Muungano wa sasa hauna watetezi. Huwezi kutoa utetezi wa vitisho au wa Kikatiba. Ni lazima uwe utetezi wa kiakili wenye kushawishi hisia vile vile.
Mwanasheria Mkuu wa Tanzania hawezi kutetea Muungano kwa kusema “Katiba inasema hivyo”. Huwezi kutetea Muungano kwa kusema “kuuvunja ni uhaini”.
Naelewa kuna sheria ambazo zinafanya kuzungumzia suala la Muungano au hata kutaka kuvunjika kuwa ni kosa kubwa. Lakini wakati umefika kwamba baada ya miaka 47 ya Muungano aidha kizazi kilichotuletea matatizo kikae pembeni ili kizazi kipya cha Watanzania kiamue kuuokoa Muungano wao au kizazi hicho kiamue kuanza moja kujenga msingi ulio mzuri zaidi wa mahusiano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara – mimi si Muumini wa Tanganyika. Jambo moja nina uhakika nalo ni kuwa hatuwezi kuendelea tulivyo kila moja abaki na nchi yake tuwe marafiki tu basi na kama hawataki basi lakini tusilazimishane.

No comments:

Post a Comment