Wednesday, July 13, 2011

ALI JUMA SHAMUHUNA MTETEZI WA WAZENJI KTK MAFUTA NA GASI ASILI


WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi jana wameipitisha kwa tabu hutuba ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati baada ya wajumbe wengi kutaka ufafanuzi wa kina na kauli ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya hatma ya mafuta na gesi asilia kutolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Akifanya majumuisho yaliomchukua muda mrefu Waziri wa wizara hiyo, Ali Juma Shamuhuna aliwaambia wajumbe hao kwamba suala la mafuta na gesi asilia limeshamalizwa katika ngazi za maamuzi kwa kuwa msimamo wa serikali upo pale pale kwamba suala hilo ni la wazanzibari wenyewe na kilichobaki ni kusubiri hatua zinazoendelea za kutayarisha sheria.Shamhuna alisema suala la mafuta limeshatolewa maamuzi tokea vikao vya baraza la wawakilishi vilivyopita na tayari baraza la mapinduzi limeshalijadili kwa kina suala hilo, hasa kwa kuzingatia sala hilo linawagusa wazanzibari wote kiuchumi, huku mipango ya kuhakikisha linaondolewa katika orodha ya mambo ya muungano.Alisema moja kati ya mgogoro uliomo katika katiba ya Tanzania ni suala la mafuta, ambapo lazima ushirikiano upatikane na kuepuka baadhi ya wengine kuonekana wasaliti kwani katika masuala kama hayo wapo ambao hujitokeza kuanza kuwa na misimamo tofauti.
“Napenda kuahidi, katu sitorudi nyuma katika suala la mafuta kama lilivyoamuliwa katika baraza hili, nakupongezeni sana kwa kuguswa na suala hili, meseji zenu zimefika kunakohusika na wamezisikia wenzetu”. Alisema ShamhunaAidha alisema Katiba ya Zanzibar na ya Muungano zote zina matatizo na ndio chanzo cha mgogoro unaoendelea juu ya umiliki wa mafuta na gesi hivi sasa lakini aliwataka wananchi wote kuwa kitu kimoja ili kusmama na kauli moja kama wazanzibari wapate kufanikiwa wakati utakapofika wa kutoa maoni wakati wa mchakato wa katiba mpya ya Tanzania.Waziri huyo amesema wakati umefika kwa Tanzania bara kuwaachia wananchi wa Zanzibar haki ya umiliki wa raslimali zao huku akisisitiza kwamba suala la umiliki wa mafuta katika bahari kuu ya Zanzibar lipo chini ya Serikali ya Mapinduzi na haoni sababu kwanini linajadiliwa barazani wakati maamuzi yameshatolewa katika vikao vilivyopita.“Mheshimiwa Spika vikao vilivyopita suala hili tayari tulikuwa tumeshalijadili na maoni ya wananchi kupitia wawakilishi wao serikali imeyafanyia kazi lakini kubwa ni kwamba uamuzi wa kuondoa mafuta katika orodha ya mambo ya Muungano umekwisha,” alisema Shamuhuna.Licha ya Waziri Shamuhuna kueleza kwa ufasaha suala hilo lakini bado wajumbe hao walishindwa kuridhika na ufafanuzi wake jambo ambalo lililowalazimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Othman Masoud na waziri wa Katiba na Sheria Abukakari Khamis Bakari, kusimama mara kwa mara kujibu hoja za wajumbe hao zinazohusu sheria hasa kwenye kipengele cha mafuta na gesi asilia.
Jukumu alilonalo Shamuhuna kwa sasa ni kuliondoa suala hilo katika orodha ya mambo ya muungano ambapo kwa mujibu wa katiba iliyopo imekuwa kipingamizi kikubwa cha uchimbaji mafuta.
Alisema kwa uamuzi wa baraza hilo, kinachotakiwa kufanywa na Serikali ya Muungano kupeleka muswada wa sheria ya kuondoa suala hilo katika mambo ya Muungano.Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wanahoji umiliki wa mafuta na gesi kuwa chini ya mambo ya Muungano, wakati rasilimali hiyo ni mali ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria iitwayo Mining Decree ya mwaka 1951.Shamuhuna aliwahakikishi wajumbe wa baraza hilo kwamba chini ya uongozi wake ambaye anasimamia wizara hiyo ngumu atahakikisha kupitisha uamuzi wa kuondoa mafuta katika orodha ya mambo ya Muungano mwaka 2009, atasimamia kidete kuhakikisha sekta hiyo inabaki chini ya umiliki wa Zanzibar.“Mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano yatumiwe kikamilifu na yawe ajenda namba moja katika kuhakikisha wananchi wanatoa mawazo ya kuling’oa suala hili la mafuta” alisema Waziri huyo ambaye anaonekana ni jasiri kama alivyosifiwa na baadhi ya wajumbe wenzake.Alisema kuundwa kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na nchi mbili, kumesababisha Katiba ya Zanzibar na ya Muungano, zote kuwa na matatizo katika mambo mengi, yakiwemo ya uchumi na kisiasa.“Katiba ya Zanzibar na ya Muungano, ulioundwa baada ya nchi mbili kuungana, zote zina matatizo, lakini wenzetu hawataki kuyaondoa lakini nakuhakikishieni wajumbe wa baraza hili tukufu kwamba wenzetu ni wakaidi lakini hili tutahakikisha tunasimamia haki zetu na kuzitetea kwa nguvu zote,” alijizatiti Shamuhuna.
Akiwatoa khofu wananchi juu ya suala hilo alisema kumiliki sekta ya mafuta Zanzibar suala hilo litapatiwa ufumbuzi wa kudumu, kisheria kupitia Katiba mpya inayoendelea kuandaliwa.“Muswada wa mapitio ya Katiba mpya utakapoanza kutolewa maoni, naomba wawakilishi na wananchi, ajenda yetu namba moja ni kupata Katiba inayotoa haki kwa Zanzibar kumiliki mafuta na pia tunakuombeni katika hili sote tusimame kwa kauli moja katika suala hili,” alisisitiza Shamuhuna.Waziri Shamuhuna pia alikerwa na Muungano ambapo alisema umekuwa si ndoa bali ni ndoano iliyofika kooni, huku kila anachosema Mzanzibari juu ya matatizo ya muungano akitizamwa kwa jicho baya na kuonekana ni msaliti.Aliwaeleza wajumbe hao kwamba sio rahisi kwa muwekezaji anayeweza kuleta kampuni zake kuja kuchimba na kuwekeza katika mafuta kwa wakati huu kutokana na kuwepo migogoro ya katiba na sheria katika suala hilo.Akitoa historia ya utawala wa aliyekuwa rais wa Zanzibar wa awamu ya tano, Dk Salmin Amour Juma, Waziri Shamuhuna alisema shirika la TPDC liliileta kampuni ya kutoka Canada kuja kufanya utafiti wa mafuta, lakini rais huyo alikataa kwani nchi hiyo iliigomea kuipa misaada Zanzibar.Wakati ule mimi nilikuwa waziri lakini hawa TPCD walipokuja na wageni wao Dk Salmin aliwafukuza akawaambia ondokeni nendeni zenu nyinyi si mmeigomea Zanzibar kuisaidia” alisema Shamuhuna na kupigiwa makofi na wajumbe wenzake.Shamuhuna alikuja na mafaili makubwa ya tafiti za mafuta kwa mbele ya wajumbe ambapo alisema yale yalio katika mamlaka yake kuhusu suala la mafuta yamekuwa yakifanyiwa kazi ambapo alieleza taarifa mbali mbali za kiutafiti zinazoendelea katika kuyatafuta katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mansour Yussuf Himid alisema dhamira ya serikali na wananchi wa Zanzibar ni kuliondisha suala hilo katika mambo ya muungano.“Msimamo wangu mimi ni sawa na watu wote humu ndani, sikubali leo, sikubali kesho sikubali Abadan!, ni dhambi kulikubali suala hili kuendelea kuwa katika mambo ya muungano”.“Ajenda yetu ni kuyatoa mafuta na gesi asilia katika mambo ya muungano, narejea tena kuyatoa, hiyo ndio ajenda na msimamo wetu, tupitisheni bajeti ya mheshimiwa Shamuhuna ili tutizame aliopo mbele yetu maana tuna kazi kubwa ambayo ya kuingia mitaani na kuwaelimisha wananchi wetu”,alisema Mansoor.Mansoor ambaye alikuwa waziri wa nishati katika kipindi kilichopita alisema jambo la msingi liliopo mbele yao ni kuwaandaa wazanzibari ili wajadili upya mambo ya muuungano na kueleza bayana ni mambo yepi wanayataka na yepi yatolewe, na hata ikibidi pia kuangalia mfumo wa muungano wenyewe ikiwemo kujadili serikali ngapi.Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Othman Masoud alisema suala la mafuta linahitaji umakini na kuwepo utaratibu maalum ili kuwepuka machafuko kama yale yanayoshuhudiwa kutokea katika nchi nyingine huku akiwasisitiza wajumbe kuwa na busara aktika suala hilo kwani nchi nyingi zimeingia katika mapigano kutokana na rasilimali hiyo.Othman alisema Zanzibar inahitaji kuunda sheria ya mafuta, kwani hivi sasa haipo, kwani sheria ya mwaka 1951, imekufa baada ya mafuta kuiingiza katika orodha ya mambo ya Muungano.“Ni muhimu jambo hili kulitatua kikatiba liwe wazi na tuweze kukaribisha wawekezaji kwenye sekta ya mafuta, hakuna njia ya mkato tusubiri marekebisho ya katiba ya Jamhuri yaje tuone tutfahanya nini”. Alisema mwanasheria huyo.Naye Katiba na Sheria, Abubakari Khamis Bakari, ambaye mara kwa mara kwa mara aliazimika kusimama na kutoa ufafanuzi wa kisheria alisema serikali lazima ikae itafute mbinu ya kulitoa katika orodha ya Muungano kwanza halafu ndio hatua nyengine zifuate.“Suala la mafuta limeshaamulia na Baraza la Wawakilishi, serikali inalishughulikia kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar, tunalishghulikia kwa nguvu zetu zote na katika hili msimamo wetu upo wazi kwamba tutaheshimu na kutekeleza maoni ya wananchi”, alisisitiza Bakari.Bajeti hiyo baada ya majadiliano na kuchukua muda mrefu hatimae ilipitishwa ambapo wajumbe wa baraza hilo waliotishia kuondosha shilingi walisikia ufafanuzi na hatimae kupitisha kwa sauti moja makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment