Monday, July 4, 2011

JE Z;BAR ITAKUWA VIPI KTK JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI NCHI AU MKOA WA PWANI Z;BAR


NI IPI NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI?
Kwa hakika kauli mbili zilinivutia katika wiki iliyopita na kutokana
na kauli hizo ndiko ambako nitatoa mada yangu ya wiki hii katika safu
hii inayoangaza matukio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa
upande wa Zanziibar.
Moja ni kauli iliyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail
Jussa wakati akichangia kwenye Baraza la Wawakilishi kwenye Bajeti ya
Wizara ya Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd na kwa kiasi
Fulani kulitikisa Baraza hilo.
Wengine tulifikiria kwa jinsi Jussa alishikilia suala hilo kuwa
alikuwa anaelekea kutishia kutoa shillingi katika Bajeti hiyo, lakini
nafikiri cha muhimu kilikuwa ni kuweka indhari na kwa sehemu kubwa
kuweka rekodi kuwa jambo hilo limedaiwa na siku moja kuja kukumbushia.
Yalikuwa ni matakwa ya Jussa kuwa Serikali impe kauli kwamba itaanza
taratibu kwa kuandika barua ili kutaka Zanzibar ipewe hadhi ya aina
ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki yenye nchi 5 za Kenya, Uganda,
Burundi, Rwanda na Tanzania.
Hoja ya Jussa ilijikita juu ya Zanzibar kuwakilishwa kwa kila kitu na
Tanzania kwenye Jumuia hiyo hata kwa mambo yasio ya Muungano, mtindo
ambao umeendelea kwa miaka 47 ya Muungano ambapo nje ya Tanzania basi
huwa Zanzibar inawakilishwa na Tanzania katika Mambo Yasio ya
Muungano, kinyume na ridhaa ya Zanzibar.
Watanzania sote tunajua kuwa tuna mambo ya Muungano ambayo 11
yalipatikana moja kwa moja kupitia Mkataba wa Muungano na mengine 11
yameongezwa moja moja hadi sasa yamefikia kuwa ni 22 ambayo
yanazunguka maeneo ya kiuchumi, kisiasa na kifedha na hata mitihani na
utafiti.
Si madhumuni ya makala hii kujiuliza juu ya uhalali wake, maana
mengine mengi yanahojiwa, wala si madhumuni ya makala kwa leo
kujiuliza iwapo ni kweli 23 au ni mengie zaidi iwapo yatanyumbuliwa na
pia si nafasi ya makala hii pia kujiuliza mengine kadhaa yanayoingizwa
kwa kuongeza kifungu kisemacho “Sheria hii itatumika Tanzania Bara na
Tanzania Visiwani” yanafaa kweli kuitwa Mambo ya Muungano.
Ila itoshe kusema kuwa kuna Mambo ya Muungano 23 chini ya Katiba na
ndani ya mambo hayo Zanzibar haiwezi kutia mkono wake lakini ina nguvu
kamili sawa na Tanganyika kwenye Afya, Elimu, Kilimo, Utalii na katika
haya Zanzibar inajisimamia kikamilifu kabisa.
Ndipo Jussa akahoji sasa inakuwaje kwamba katika mambo ambayo Zanzibar
inajisimamia kikamilifu tena iwakilishwe na isemewe? Jee imetoa
ridhaa, jee inasemewa, jee inasemewa vyema? Hili alionyesha shaka kama
ambavyo uzoefu wa Wazanzibari wengi umekuwa juu ya Tanganyika kwamba
choa mbele na cha Wazanzibari nyuma, kwao hakuna ya njugu nirembwe na
alo mbele hubakia mbele.
Kwa mnasaba na hofu ya Zanzibar kuzidi kumezwa ndani ya Jumuai yenye
Muungano wa kisiasa miaka michache ijayo, pengine Jussa akaona
alikazanie hili mapema nalo ni kujaribu Zanzibar kupata fursa ya
kujiwakilisha wenyewe angalau katika kiwango fulani na akaitaka
Serikali ya Zanzibar itume barua au ianze mazungumzo ya kuipatia
Zanzibar uwanachama shirikishi.
Mwandishi wa makala hii, akitoa mada kuhusu Jumuia wiki iliyopita
alipendekeza kuwa Zanzibar ipewe fursa ya kikatiba ya kuhudhuria ngazi
ya Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki ambako huko itaweza
kujisemea juu ya mambo yake wenyewe ambapo tunaambiwa kuwa katika
mambo 17 ya ushirikiano katika Jumuia hiyo ni 4 tu ndio yanayoihusu
Zanzibar na Tanganyika na mengine 13 kila upande Tanganyika na
Zanzibar una fursa na mamlaka sawa kabisa.
Lakini Serikali ya Zanzibar kupitia Waziri Muhammed Aboud na
Mwanasheria Mkuu Othman Masoud ikatunisha misuli kupinga wazo halua
kama hilo na ikawa ni yale yale ya Zanzibar kuwa adui wake wenyewe.
Maneno kadhaa matamu yakatolewa lakini yote yakilenga kukataa
kujifiunga (to commit) Serikali juu ya kupeleka ombi hilo.
Hoja ya Serikali ya Zanzibar kukataa hoja ya Jussa ni dhaifu. Hoja
iliyotolewa ni kuwa kwa sasa Mkataba unaziruhusu nchi kamili kujiuunga
na Zanzibar haiwezi kuwa na nafasi, ambapo Zanzibar yenyewe ilitakiwa
ijisemee, ama kwa kuibana Tanzania au kwa kuitikisa Jumuia ijue kuwa
ndani ya wanachama wake basi mmoja ana mgogoro wa ndani ambao lazima
upatiwe suluhu.
Inakuwa ni kichekesho kwa Jumuia ya Afrika Mashariki kuendelea
kujidanganya kama kwamba haijui kuwa kuna hali hiyo na ambayo
inavukuta na kuchemka kiasi ambacho ingefaa kuchukuliwa hatua na
Jumuia wenyewe. Ni kichekesho pia kwa Jumuia hiyo kunyamaza kimya
ilhali inajua kuwa Tanzania haina mamlaka ya kuiwakilisha Zanzibar
katika mambo 13 na bado inafanya hivyo.
Mtu atajiuliza Jumuia iliwahi kuiuliza Tanzania imepata wapi nguvu za
kuisemea Tanzania katika mambo 13 yakiwemo ya kilimo, afya, elimu na
kama hayo? Na kama inafanya hivyo jee haivunji vipengele vya Mkataba
wa Jumuia hiyo?
Kauli nyengine iliyonivutia ni ile iliyotolewa na mwanaharakati Juma
Sanani katika warsha ya siku moja juu ya Mchakato wa Uchaguzi na
Vijana iliyoandaliwa na Jumuia ya Uamsho wa Kiislamu ambapo Sanani
alisema kuwa Zanzibar isisubiri kumalizwa kwa kuja Jumuia ya Afrika
Mashariki bali ijitoe katika Muungano.
Sanani alisema kila bidii imefanywa ili kuwa na Muungano wenye uwiano,
lakini alillamika juu ya kile alichokiita kukosekana kwa nia nzuri kwa
upande wa Tanganyika na akanena kuwa kwa sasa Zanzibar haina njia
isipokuwa kujitoa katika Muungano na ikutane na Tanganyika katika
Jumuia ya Afrika Mashariki ambako uwanachama wao utakuwa ni sawa
kimamlaka na kihadhi.
Sanani alisema vijana na wananchi wa Zanzibar wanapaswa hilo kuliweka
wazi katika Mchakati wa Katiba ujao ambao rasimu yake itapelekwa
Bungeni baada ya rasimu ya kwanza kukataliwa lakini zaidi rasimu hiyo
ikichanwa ilipowasilishwa Zanzibar.
Naamini kwamba kauli hizi mbili zitakuwa kama kengele ya kuamshwa kwa
Serikali ya Zanzibar lakini pia Serikali ya Tanzania, ingawa nina
sababu za kuamini kuwa kengele hii itapuuzwa kama ambavyo zimepuuzwa
nyingi na kusubiri maharibiko ndipo hatua ichukuliwe.
Lakini pia yaweza kuwa ni kauliza debe shinda ambapo hazitafikia
popote pale iwapo huo Mchakato wa Katiba ujao haukuweka kipengele kuwa
kauli za Wazanzibari sisikike na ziheshimiwe peke yao na sio katika
kapu kubwa la maoni ya Watanzania wote.
Na hio kwa muda mrefu imekuwa ndio shida ya Muungano kwamba
imesahulika kuwa zilizoungana na nchi mbili huru na kwa hivyo kwa kuwa
hadi sasa tuna Muungano wa nchi mbili basi sauti, matakwa na matumaini
ya nchi hizo yaonekana wazi wazi maana yana wapiga kura wake na
mamlaka yanayotlewa kwa Serikali ambapo Serikali inakuwa na mipango na
sera zake na matarajio hayo kutgemewa kutekelezwa.
Mara kadhaa imeonekana kuwa wengi wa mawaziri wa Tanzania hawaijui
Zanzibar kiundani katika mambo ambayo yako chini yao si ya Muungano
lakini wanayoisemea Zanzibar, lakini pili hakuna utaratibu wa kikatiba
kuhusu hili na ndio maana kelele zinapigwa lakini mwenye nyumba hataki
kusikia.
Rai yangu iwapo Serikali ya Zanzibar haioni haja ya kuchukua hatua kwa
mujibu wa mapendekezo ya Jussa basi wakati umefika kwa wananchi wa
Zanzibar kuibana Serikali yao na pia Serikali ya Tanzania kwamba
Zanzibar inataka iwe na sauti juu ya mambo yake ndani ya Jumuia ya
Afrika Mashariki.
Sina haja ya kutoa mbinu hapa maana najua kuwa Wazanzibari ni weledi
katika hilo na ujumbe utafika

No comments:

Post a Comment