Monday, July 11, 2011

KIWANJA CHA MPIRA BWELEO CHA JENGWA KTK NCHI YA ZANZIBAR

Hassan Gharib
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatua ya wananchi wa kijiji cha Bweleo kujenga uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, inakwenda sambamba na sera ya Serikali ya kulitangaza Taifa kupitia michezo.
Maalim Seif amesema hayo jana katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira waiguu huko Bweleo, Wilaya ya Magharibi Unguja.Ujenzi wa uwanja huo wa kisasa, ulioanza kwa kazi za kusafisha ardhi na kung’oa mawe, unakadiriwa kutumia zaidi ya shilingi Milioni 162 hadi kukamilika kwake.
Amesema Serikali inaunga mkono kwa dhati juhudi zilizoanzishwa na wananchi hao, ikitilia maanani kuwa ni moja kati ya mambo yatakayoweza kuitangaza Zanzibar ndani na nje ya mipaka yake.Alisema Zanzibar, ilio chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa, inalenga kuimarisha michezo kwa kurejesha utaratibu wa zamani wa michezo mashuleni, ili kupata wachezaji bora kutoka katika kila nyanja.
Alisema iwapo kutakuwa na maandalizi mazuri Zanzibar inaweza ikatoa wachezaji mahiri, hususan katika mpira wa miguu kama zilivyo nchi kadhaa za Afrika Magharibi.Alisema jambo kubwa linalopasa kufanyika ili kupiga hatua na kulingana na nchi hizo, ni kuandaa sera nzuri za kimichezo, kuwa na viwanja bora pamoja na kufanya juhudi katika kuwaendeleza vijana wenye vipaji.
Maalim Seif aliwaeleza wanakijiji na wanamichezo waliohudhuria hafla hiyo kuwa mbali na michezo kuimarisha afya, lakini pia hutoa ajira na kuainisha uwepo wa soko la uhakika katika soka, huku wachezaji wakilipwa fedha nyingi zaidi ya maprofessa.
Alipongeza uamuzi wa wanakijiji hao kwa azma yao ya ujenzi wa uwanja huo, na kusema hatua hiyo inakwenda sambamba na mahitaji ya Ulimwengu huku akieleza matumaini makubwa aliyonayo ya kukamilika kwa uwanja huo kutokana na ari waliyoanza kuionyesha wanakijiji hao.
Katika hatua nyengine Maalim Seif alisikitishwa na tabia ya baadhi ya watu, wakiwemo watendaji wa Serikali ya kuvamia maeneo yaliotengwa kwa shughuli za kimichezo, hivyo kuwashukuru wananchi wa Bweleo kwa hatua ya kutenga ardhi kwa shughuli hizo.
Mapema Mkurugenzi mtendaji wa ujenzi huo, Hassan Gharib alimweleza Makamu wa kwanza wa Rais kuwa ujenzi wa uwanja huo umezingatia vigezo vya kimataifa, ikiwemo vipimo, vyoo, vyumba vya wachezaji kubadilishia, chumba cha waamuzi pamoja na kuwa na jukwaa kwa ajili ya watu mashuhuri (VIP) ambalo litaezekwa kuhifadhi jua au mvua.
Alibainisha kuwa pale utakapokamilika unatarajiwa kuchukua nafasi ya pili kwa ubora wa viwanja hapa Zanzibar, ukitanguliwa na ule wa Amaan.Alisema hadi hivi sasa kiasi cha shilingi Milioni 12 tayari zimeshaatumika na kuwashukuru wadau mbali mbali wa soka waliotoa michango yao ya hali na mali kuendeleza ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment