Monday, July 11, 2011

MAALIM SEIF AWAPA MOYO WAZENJI KUHUSU HAKI ZAO NA VITAMBULISHO JE YATATIMIZWA..?

Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kendwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, baada kumaliza ziara yake ya Kichama kuzungumza na Viongozi wa Jimbo la Ngungwi na Kendwa
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema maridhiano yaliofanyika baina ya vyama vya CCM na CUF na hatimae kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yalilenga kuhakikisha kila mzanzibari anapata haki zake za msingi bila kubaguliwa.
Amesema kila Mzanzibari na hasa kila kiongozi ana wajibu mkubwa wa kulea na kuendeleza maridhiano hayo kwa faida na mustakbali wa uhai wa Taifa.Maalim Seif ambae pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amesema hayo jana huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, alipozungumza na wananchi wa jimbo hilo, katika ziara yake za kuzungumza na viongozi wa CUF wa majimbo ya Mkoa huo.
Alisema wakati Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikijizatiti kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuondokana na umasikini, kuna baadhi ya watu wakiwemo viongozi bado wamejawa na ‘masimbi’ wakitaka kuwarejesha Wazanzibari kule walikotoka.
Alisema katika baadhi ya maeneo kumeibuka tatizo kubwa la wananchi kukosa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, bila ya kuwepo sababu zozote za msingi.Akitolea mfano wa kauli yake, alisema katika Jimbo la Nungwi kuna watu wapatao 2500 waliokosa vitambulisho hivyo, huku kukiwepo malalamiko kwa baadhi ya wageni kupatiwa vitambulisho hivyo bila ya kuwa na sifa.
Alisema kila Mzanzibari mwenye sifa ana haki ya kupata kitambulisho hicho na kuainisha kuwa hatua ya kuwanyima kitambulisho Wazanzibari wenye sifa ni jambo lisilokubalika, huku akionya hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wale wote wanaokwaza mshikamano uliopo.
Alisema akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais anakusudia kulisimamia jambo hilo yeye mwenyewe na kuhakikisha kila Mzanzibari mwenye sifa na haki ya kupata kitambulisho hicho anapatiwa bila usumbufu wowote.
Katika hatua nyingine Maalim Seif amewataka wananchi wa jimbo hilo kushikamana katika kutetea maslahi ya Zanzibar, hususan wakati wa kutoa maoni kwa ajili ya mswada wa kupatikana Katiba mpya utakapowadia.
Alisema kila jambo litakalozungumzwa mbele ya Tume itakayoundwa ni budi ijengewe hoja ili ipatikane Katiba yenye maslahi kwa Zanzibar, na kuwataka wananchi hao kutotoa nafasi kwa wasioitakia mema Zanzibar.

No comments:

Post a Comment