Monday, August 15, 2011

BAA ZAZIDI KUCHWOMWA MOTO ZANZIBAR KUSAFISHA NAJISI

 Zimelipuliwa baa sita, hoteli moja
Baa nyingine imechomwa moto katika eneo la Kisauni jana na kufanya idadi ya matukio ya ulipuaji moto baa na nyumba za wageni visiwani Zanzibar kufikia matatu katika muda wa wiki moja.
Walioshuhudia baa hiyo iitwayo Maisha Plus ikichomwa moto, walisema tukio hilo lilitokea saa moja usiku baada ya kundi linalokadiriwa kuwa na watu saba kuvamia baa hiyo katika Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.Kabla ya kuchoma moto baa hiyo, watu hao wakiwa na silaha walimshikilia mlinzi Isaya Juma (29) na badaye kumjeruhi kwa kumkata mkono wa kushoto.Tukio hili limekuja baada ya watu wengine wasiojulikana kuchoma moto Hoteli ya Matemwe Beach Villa katika eneo la Kiwengwa Jumapili iliyopita na baa ya Amani Fresh juzi katika eneo la Amani mjini Zanzibar.Akithibitisha kutokea kwa tukio la jana ambapo baa ya Maisha Plus pia ilichomwa moto jana, Kamishina wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema uhalifu huo ulitokea saa moja dakika 40.Alipoulizwa juu ya mfululizo wa matukio hayo na kama kuna watu wamekamatwa kusaidia polisi baada ya kushukiwa, Kamishna Mussa alisema polisi haiwezi kukamata watu kabla ya uchunguzi.“Hadi sasa hakuna mtu tuliyemkamata na bado hatujui sababu ya baa kuchomwa moto Zanzibar,” alisema Kamishna Mussa.Hata hivyo alisema vitendo vya uchomaji moto mali za watu ni uvunjaji wa sheria na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi. Alipoulizwa juu ya hatua zilizochukuliwa na polisi juu ya matukio mengine manne ya aina hiyo katika kipindi cha mwaka huu peke yake, kamishna Mussa pia alisema hakuna aliyekamatwa.Mlinzi wa baa ya Maisha Plus aliyezungumza na Nipashe akiwa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimoja, Juma alisema watu waliomvamia, mmoja alikuwa na bastola na wengine walikuwa na mapanga na marungu.Alisema watu hao walimkata mkono wa kushoto kwa kutumia panga wakati akijaribu kuwazuia kumwaga mafuta ya petroli kutoka katika madumu mawili waliyokuwa nayo na baadaye kuchoma moto baa hiyo.“Nasikia maumivu makali sana, naomba Uniache nipumzike, nasikitika mkono wangu umekatwa,” alisema Juma. Mmiliki wa baa hiyo, Jamilah Awadh alisema baa yote imeteketea pamoja na mali zote zilizokuwemo ndani, ikiwa ni pamoja na majokofu, majiko, vinywaji vya aina mbalimbali, samani ambavyo hata hivyo hakuweza kukadiria thamani yake.

No comments:

Post a Comment