Tuesday, August 9, 2011

HAKUNA SEREKALI TATU NI KUVUNJA MUUNGANO TU BASI


Tumeona katika makala iliopita kuwa Muungano wa Tanzania haukutokana na ridhaa ya wazanzibari na kuwa hata kupita miaka 47 baadae, serikali ya Muungano “HAITHUBUTU” kuitisha kura ya maoni kuwauliza. Tumeona pia kuwa mzee Abeid Karume alilazimishwa kuridhia Muungano kwa kutishiwa kuvamiwa serikali yake ya mapinduzi na dola ya magharibi ambayo haikupndezwa na upepo wa kimapinduzi uliovuma Zanzibar, Januari,1964. Matokeo ikawa nipe nikupe:Kambi ya Magharibi ilishinda vita baridi dhidi ya ile ya Mashariki na Mwalimu Nyerere akatunukisa Zanzibar kwa mchango wake.
Ikiwa Mungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuja bila ya ridhaa ya Wazanzibari, (kwavile hawakuulizwa) ni dhahiri vitisho vilitumika nyuma ya pazia .Halafu ikawa “Funika kombe mwanaharamu apite”, eti “Pan-Africanism” that never was”.Kuleta “umoja wa Afrika”.Nani tangu enzi zile aliejiunga na Muungano huo wa Afrika na Pan Africanism ya Mwalimu imefikia wapi? Kinyume chake, muungano wa Mali na Guinea ulivunjika na hata ule wa Senegambia (Senegal na Gambia).
Ingawa Muungano haukuwa wa hiyari bali ni “ndoa ya kulazimisha”, Zanzibar haina nguvu za kijeshi wala za kisiasa wakati huu kujikomboa.Nasema hivyo kutokana na ukweli wa mambo mawili: Zipo “Military and political factors to reckon with. ” Wazanzibari tunapaswa kutambua ukweli wa kijeshi na wa kisiasa: Wa kisiasa ni ule alioutilia mkazo hivi Punde mbele ya Baraza la waakilishi Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Idi. Tuanze na wa kijeshi:
UKWELI WA KIJESHI: 
Thuluthi-mbili ya majeshi yaliopo Zanzibar na Pemba, yasemekana ni kutoka bara na sidhani ndani yake kuna mzanibari.Nasikia hata KMKM iko chini ya Mtanzania-bara. Waziri wa ulinzi ni “mzanzi-bara “-mwana wa mzee Rukhsa.Na mchango wa wake unajulikana kuwa hata Zanzibar iliomlea tangu mdogo na kumsomesha ni “rukhsa ” kuiuza kwa bara.
Hivi ni vikosi hata nyakati za usalama bila ya uchaguzi, hufanya mazowezi yao mitaani mwa raia kuwatisha tu wazanzibari. Badala ya kufanya mazowezi yao kambini au kingo za bahari-pwani (kizingo),hupita na kuhemkwa mitaani mwa raia. Tumewaona kwa macho yetu alaasiri tukiwa ndani ya daladala huko Chukwani wakipita barabara ya Baraza la Waakilishi hadi Kiembesamaki na kurejea kwa njia hiyo kambini. Raia ndani ya daladala na walio nje, hutumbua macho tu kuangalia vijana wakihemkwa. “fanya fujo uone”.
Yasemekana Tanzania-bara ina kambi 25 Zanzibar na Pemba.Je, Zanzibar imekaliwa kijeshi ? Au imefunga ndoa kwa hiyari ? Au ililazimishwa kufunga ndoa kwa vitisho ? Ikiwa ndoa ilikua ya hiyari,basi kuna usemi katika kitabu cha Ali Muhsin Barwani (Kiongozi wa ZNP-Hizbu) akizungumzi Muungano: “Lugha anayoitumia mwanamme kumtongoza mwanamke kufunga nae ndoa, ni tofauti na ile anayotumia baada ya kufunga ndoa.” Huu basi ndio ukweli wa KIJESHI wazanzibari tunpaswa kuutambua tunapodai “kuvunja Muungano”.
UKWELI WA KISIASA:
CCM-ZANZIBAR inahubiri sera ya” serikali 2 (Je,kuelekea 1?) Sera hii hivi karibuni,imepigiwa upatu na kuhanikiza tena na viongozi wa CCM- Zanzibar kuzima sauti ya mzalendo wa chama hicho Mansur Himid, aliedai mfumo wa sasa wa serikali 2 ni butu. Kwa kadiri hakuna wajumbe wengi wa CCM-Zanzibar, walio wazalendo kama Himidi wanaothubutu kubisha sera hiyo, wazanzibari ,hatuna budi bali kuutambua ukweli huu wa kisiasa.CCM-Zanzibar inawekwa madarakani na CCM-bara (Sustained to power-mapinduzi daima.”
Isitoshe,dola za Magharibi, kutokana na kile kilichoitwa “Mfumo Kristu”, haziko tayari kuiachia Zanzibar, kurejea tena kuwa (Mecca) ya uislamu ili kuathiri bara na Afrika Mashariki nzima kama zamani pale “zumari likipulizwa visiwani wachezao bara.”
Kufuatia ushindi wa dola hizo za kikristu huko Mindenao (Philipines), East Timor (Indonesia) na karibuni Sudan /Kusini, dola hizo hazitakuwa tayari kuregeza kamba na kuiachia Tanzania-bara ikidhibitiwa na waislamu.Na ndio sababu kuu Zanzibar ikashinikizwa na Mwalimu itoke Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (IOC) na pia ndio maana hadi leo, Tanzania kwa jumla, haijungi na IOC. Hii lakini, haina maana wazanzibari tusalim amri na kutoendeleza mapambano ya kujikomboa. Iko siku waislamu wa Tanzania-bara watatanabahi mchezo gani unachezwa juu ya Zanzibar na dola hizo ambao mwishoe, utawaathiri hata nao huko bara.
SILAHA YETU NI IPI ?
Umoja, mshikamano na uadilifu, utayafanya majeshi ya Tanzania-bara yaliokalia Zanzibar kuwa butu. Hayatathubutu kuwafyatulia risasi wazanzibari ikiwa watazungumza kwa sauti moja tangu majumbani,mitaan na hata miskitini. Silaha ya UADILIFU na NGUVU za HOJA na sio HOJA YA NGUVU, yaweza kutufikisha tunakotaka : Kivuko ni serikali 3:Ile ya Zanzibar,Tanganyika na ya Muungano. Baada ya hapo tutatafakari.
Kuna wanaoweza kusema Laila anaota ndoto. Je, Mandela na ANC,waliuangusha utawala wa kibaguzi na mtengano huko Afrika Kusini kwa mtutu wa bunduki au kwa busara na uadilifu ?
Majeshi ya wazungu ya akina De Klerk yangweza kuendelea kutawala hata miaka 10 zaidi.A.Kusini Ilikua na nguvu kubwa za kijeshi na kiuchumi,lakini haikua na nguvu za uadilifu kutetea ubaguzi na mtengano(APARTHIED) au kukiuka miko ya demkrasi kwa wachache kuwatawala wengi.
Tanznia-bara nayo inajivunia kuwa ilikuwa Makao MAKUU ya vyama vya ukombozi barani Afrika na Makao Makuu ya Vyama vya Wafanyikazi wa Afrika. Vipi leo nchi iliokua safu ya mbele katika ukombozi, igeukeMkoloni wa nchi ndogo ya Zanzibar kama ilivyokua Uingereza?
Vipi Umoja wa Afrika na Ulaya ya Magharibi, ufumbe macho huku dola moja huru ya kiafrika (Tanganyika) ina imeza dola nyengine huru (Zanzibar) bila ya ridhaa ya wananchi wake ?
Tanzania-bara inaelewa kwamba ,Muungano ulikuwa ni wa kushinikizwa na sio wa hiyari. Na ikiwa wanabisha hoja hii ,WAITISHE KURA YA MAONI huko Zanzibar juu ya Muungano ili kuuhallisha ? Hawathubutu kwani hawakufanya hivyo miaka 47 iliopita iweje sasa wanapojiandaa kutoka serikali 2 kwenda 1?

WAZANZIBARI SASA TUFANYEJE ?

Wenzetu Waeritrea walishika silaha hadi kujikomboa kutoka Ethiopia baada nao kuanguka mateka wa mikakati ya dola za kikoloni kama vile Zanzibar pale Eritrea ( koloni la Mtaliana) ilipounganishwa kimabavu na hila na Ethiopia. Ushauri wangu : Zanzibar itumie kwanza silaha ya uadilifu ,umoja na mshikamano;kwani kuna ule usemi”Maji hukata kamba”.

No comments:

Post a Comment