Wednesday, November 9, 2011

SHEIN AKUBALI KULA KIAPO CHA KUWA YEYE NI WAZIRI ANAYE WAKILISHA MKOA WA PWANI ZANZIBAR.JAMANI NCHI YETU YA ZANZIBAR ISHAMEZWA

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande ili kuingia katika baraza la mawaziri la Tanzania kiapo ambacho kimezusha manunguniko miongoni mwa wazanzibari kuwa kimemdhalilisha rais wao

SHEREHE ya hivi majuzi ya kuapishwa Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, kuwa waziri asiye na wizara maalum katika Serikali ya Muungano imewashangaza na kuwaudhi watu wengi huko Zanzibar.Wanavyohisi ni kwamba Rais wao hatambuliwi kuwa ni Rais huko Bara kwa vile huko anakuwa waziri tu na pingine anakuwa chini ya amri na uongozi wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano kama ilivyo ada ya mawaziri wote wa Serikali ya Muungano wa Tanzania.Kadhia hiyo inatukumbusha yaliyojiri miaka mitatu iliyopita pale Wazanzibari waliposhtushwa kusikia kwamba nchi yao ya Zanzibar si nchi. Na tafsiri waliokuja nayo ni kwamba kama Zanzibar si nchi basi labda ni mkoa tu wa Tanzania.Bila ya shaka hisia hizo zimezuka kwa sababu ya yale mageuzi makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Hati ya Muungano, mageuzi ambayo kwa kweli yanakwenda kinyume na Hati hiyo kwa vile haikutoa nafasi ya kufanywa mageuzi yoyote yale seuze kuongezwa kwa Mambo ya Muungano kutoka idadi ya 11 na kufikia jumla ya sasa ya Mambo 22. Wala Hati ya Muungano haikuupa upande mmoja wa Muungano haki ya kujiongezea tu kiholela Mambo ya Muungano.Kwa mujibu wa Hati ya Muungano, ikiwa Rais wa Muungano anatoka upande mmoja wa Muungano, tuseme Tanganyika, basi Makamu wa Kwanza wa Rais atoke upande wa pili, yaani Zanzibar. Ndipo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akawa Rais wa Muungano na Sheikh Abeid Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.Hali hiyo iliendelea hata wakati Aboud Jumbe alipokuwa Rais wa Zanzibar. Mambo yalibadilika baadaye pale serikali ya Muungano ilipoamua kuishusha hadhi ya Rais wa Zanzibar na kumfanya awe waziri asiye na wizara maalum katika Baraza la Mawaziri la Muungano. Huo ulikuwa uamuzi wa kusudi.Nini athari ya badiliko hilo? Badiliko hilo la Hati ya Muungano limeifanya Zanzibar iwe ni kama jimbo la uchaguzi la Tanzania na limeishusha hadhi ya Zanzibar ya kuwa mshiriki sawa wa Tanganyika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako mawaziri huwa ni wabunge waliochaguliwa katika majimbo yao ya uchaguzi.Hivyo, kwa hali ilivyo mawaziri hao wanakuwa na hadhi sawa na Rais wa Zanzibar katika baraza la mawaziri la Tanzania. Na bila ya shaka katika Muungano, Waziri Mkuu anakuwa na hadhi ya juu kuipita ile ya Rais wa Zanzibar.Tukio hilo limewatia uchungu Wazanzibari. Wao wanahisi kwamba Rais wao amedhalilishwa kwa makusudi na hadhi ya nchi yao imeshushwa, pia kwa kusudi.
Hatua hiyo ya kumfanya Rais wa Zanzibar awe waziri wa Muungano ni ya kuchekesha. Ni kama, kwa mfano kumuapisha Rais wa Ufaransa kuwa Kamishina katika Muungano wa Ulaya na hivyo kuwa chini ya Rais wa Kamisheni ya Ulaya.Tukio hilo la kumuapisha Rais wa Zanzibar awe waziri katika baraza la mawaziri la Muungano linakwenda sawa na ile sera ya kuipunguzia Zanzibar mamlaka yake na mtindo wa kuyahamishia Bara mamlaka au madaraka hayo.Kama nilivyokwishaonyesha, wakati Hati ya Muungano ya mwaka 1964 ilikuwa na Mambo 11 ya Muungano, hii leo kuna Mambo 22 ya Muungano. Hayo 11 yaliongezwa yalihaulisha dhamana mahsusi na mamlaka ya utawala kutoka Zanzibar kupelekwa kwenye Serikali ya Muungano.Si hayo tu, lakini kila moja ya hayo Mambo 11 ya ziada liliongezwa bila ya kufanywa mashauriano ya maana au makubaliano ya hiyari baina ya Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano.
Na wala wakuu wanaohusika hawakukaa na kufikiria kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halijawahi kuwa na mamlaka ya kisheria yanayohitajika ili paweze kufanywa mabadiliko aina hiyo.Tukiiangalia katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaona kwamba Muungano hauwezi kukana kwamba ingawa ni Muungano wa nchi mbili, lakini si Muungano wa pande zilizo na usawa. Ni Muungano wa papa kummeza dagaa.Katika Muungano huu Tanganyika imekuwa ikitumia nguvu zake kwa Zanzibar huku ikijifanya kuwa inafanya hivyo kwa kutumia mamlaka ya kisheria. Kusema kweli wakuu wa Tanganyika wamekuwa wakifanya ujanja wa kuhakikisha kwamba Zanzibar inapoteza nguvu zake zote za utawala.Badala ya Zanzibar kuzihodhi nguvu hizo hivi sasa zimenyakuliwa na Serikali ya Muungano kwa kisingizio kwamba hayo yamefanyika kisheria.Hilo ni moja miongoni mwa mambo kadhaa yanayowafanya Wazanzibari wajione kwamba wanaonewa na waupinge Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Imefika hadi kwamba hii leo pakipigwa kura ya maoni ya kuulizwa watu kama wanautaka ama hawautaki Muungano basi kwa hisia zilizopo Zanzibar si hasha kwamba asilimia isiyopungua 85 ya Wazanzibari watapiga kura kuukataa.
Ni jambo la kusikitisha kwamba tunalijadili suala hili katika wakati ambapo kumeanza mchakato wa kutunga katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Inasikitisha kwamba Serikali za Zanzibar tangu mwaka 1964 pamoja na viongozi Wakizanzibari walioiwakilisha Zanzibar katika taasisi mbalimbali za Muungano waliridhia bila ya kulalamika pale maslahi ya nchi yao na ya watu wao yalipoingizwa hatarini.
Inasikitisha pia kwamba miaka yote hiyo Wazanzibari walikuwa wamegawanyika kichama. Tafauti hizo za kisiasa zilichangia kuiua nchi na watani wao na kuufanya uchumi wake ukwame. Hali hiyo imeyafanya maisha ya wengi wa wananchi wake yazidi kuwa magumu na ufukara uzidi kutanuka.Kwa bahati nzuri hivi sasa Wazanzibari wana fursa wasiowahi kuwa nayo ya kufanya mageuzi ya kimsingi yatayowezesha papatikane mfumo mpya wa mahusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar.Ni jambo la kutia moyo kwamba hii leo Wazanzibari wameungana na wako imara na wanauona huo umoja wao kuwa ni silaha muhimu ya kujipatia muradi wao.Wenyewe wanasema kwamba mradi huo ni wa kuwa na Zanzibar waitakayo yenye kufuata misingi ya kidemokrasi na utawala bora na ambapo wananchi wake wote watanufaika kiuchumi.
Hivi sasa wengi wao wanateseka kwa mfumko wa bei na mapato, bei za kuruka za vyakula na ukosefu wa huduma za kuridhisha za afya na elimu.Yapo masuala mingine yenye kuwashughulisha zaidi Wazanzibari. Masuala yenyewe ni muhimu kwa hali za maisha za Wazanzibari wote.Moja ya masuala hayo ni lile la mafuta na gesi asilia. Suala hilo limezusha mabishano na mgogoro kati ya pande mbili za Muungano na hadi leo halijapatiwa bado ufumbuzi.Suala hilo limekwamisha mengi kwani Serikali ya Muungano haiwezi kuanza kuyachimba hayo mafuta yaliyopo katika eneo la Zanzibar bila ya ridhaa ya Serikali ya Zanzibar.
Na makampuni ya kimataifa nayo hayawezi kuisaidia Zanzibar katika shughuli za uchimbaji mafuta bila ya ridhaa ya Serikali ya Muungano.Hali iko hivi kwa sababu ijapokuwa suala la mafuta na gesi asili limeondoshwa kwenye dhamana ya Serikali ya Muungano, bado suala hilo ni la Muungano.Wazanzibari wanauliza hivi: ikiwa kweli Rais wa Muungano na serikali yake wana hamu ya kutaka Zanzibar iendelee kiuchumi na kijamii, basi nini kinachowazuia wasiwasilishe Muswada kwenye Bunge la Muungano ambao utaondoa Mafuta na Gesi Asilia kutoka orodha ya Mambo ya Muungano?Wazanzibari wanaamini kwamba ikiwa hatua hiyo itachukuliwa, basi Serikali ya Zanzibar itakuwa na uwezo wa kusimamia uchimbaji wa hizo maliasili kwa manufaa ya Wazanzibari wote na hivyo kuziinua hali zao za kimaisha.
DUNGU ZETU MULIOKUWEKO NJE MUSISEME KUWA MUNA NCHI INAITWA ZANZIBAR TENA SEMENI MUNATOKA KATIKA MKOA WA PWANI ZANZIBAR SIO NCHI HATUNA NCHI SISI WALIYOYASEMA WATANGANYIKA SASA YASHATHIHIRI...........

No comments:

Post a Comment