Wednesday, December 21, 2011

MAALIM SEIF ASEMA-MSIOGOPE KUITWA WAISLAMU

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia uwanja wa Taifa katika hafla ya kuchangia kituo kimoja cha televisheni cha kiislamu.
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewahimiza Waislamu nchini kote kujitokeza kwa wingi kuchangia uanzishwaji wa kituo cha televisheni kiitwacho Imani, kwa sababu televisheni hiyo itatoa mchango mkubwa kufuta dhana potofu dhidi ya Uislamu, na kutoa taaluma ya maadili mema ndani ya jamii.
Alisema hayo leo alipokuwa akihutubia kwenye hafla ya kuchangia uanzishwaji wa televisheni hiyo, inayoanzishwa chini ya Jumuiya ya Islamic Foundation, ambayo pia inaendesha Redio Imani iliyopo mkoani Morogoro. Maalim Seif alisema vituo vingi vya televisheni hapa nchini mara nyingi huonesha vipindi vinavyokwenda kinyume na maadili mema ya jamii, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia kuharibu maadili ya jamii na zaidi vijana na watoto wadogo.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema mbali ya kujenga maadili mema kituo hicho cha televisheni pia kitaweza kufanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wanajamii, juu ya mazuri na mchango wa Uislamu na kufuta dhana inayoenezwa na baadhi ya watu, dhana ambazo zinapotosha na kuipaka matope dini ya Kiislamu.
“Waislamu jitokezeni kuchangia mambo ya kheri, kuanzishwa kwa televisheni hii ni jambo la kheri, wafanyakazi serikalini, Mashirika ya Umma na taasisi binafsi changieni, na wala msione haya kujuilikana nyinyi ni Waislamu, Uislamu ndio dini sahihi” alisisitiza Maalim Seif.
Alieleza kuwa wapo waislamu wenye uwezo mkubwa na nafasi ya kuchangia mambo kama hayo yenye faida kwao na Waislamu wote, lakini kuna wengi miongoni mwao , licha ya kuwa na uwezo huo wamekuwa wagumu kutoa, na badala yake kujikita zaidi katika kuchangia mambo ya anasa.
Katika hafla hiyo, Waislamu mbali mbali walijitokeza kuchangia ambapo, Makamu wa Kwanza wa Rais alichangia shilingi milioni mbili kwa ajili ya uanzishwaji wa kituo hicho cha televisheni. Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh Ali Basaleh alisema vyombo vingi vya habari nchini, vikiwemo vituo vya televisheni havina tabia ya kutangaza mambo mema yanayogusa Uislamu na Waislamu, na badala yake vyombo hivyo vimekuwa vikijikita zaidi kuripoti mambo mabaya dhidi ya Uislamu na kuyapa umuhimu mkubwa.
Basaleh alieleza kwamba televisheni hiyo ya Kiislamu ikianza matangazo yake itasaidia kutangaza na kutoa taaluma juu ya mambo ya Uislamu, ikiwemo kufuta dhana hizo potofu zinazoupaka matope Uislamu. Mkurugenzi wa Islamic Foundation, Sheikh Arif Nahad alisema Waislamu wakiamua wanaweza, kwasababu hivi sasa wameamka baada ya miaka mingi ya kujiweka nyuma na kufunga mikono katika shughuli za kimaendeleo.
Sheikh Nahad alieleza kuwa hakuna sababu televisheni hiyo ishindwe kuanza, na kwa kuwa jumuiya yake imeahidi itatekeleza hilo na kuwaahidi mamia ya watu waliohudhuria kuwa televisheni hiyo ipo njiani inakuja.

No comments:

Post a Comment