Sunday, April 22, 2012

ZANZIBAR KUMEPAMBAZUKA WAZANZIBAR MULIO NJE YA NCHI JE MUSHAMKA..?

“Usiku uwe mrefu uwavyo, lazima kutakucha tu”.
Kumepambazuka: Jamhuri ya Watu wa Zanzibar karibu kutia nanga..
Usiku wa Wazanzibari haujawa wa kuhisabu masaa na masiku, bali wa kuhisabu miaka na dahari. Wazanzibari walilazwa, si kwa kubembelezwa, bali kwa kumwagiwa utupa uliowalevya wakalewalewa, wakaghumishwa na kujingishwa wakashindwa kujitambua, hata walipo tanabahi, dahari zishapita. Wakaulizana kama walivyoulizana as-habul-kahfi “ni siku ngapi tumelala?” na wakajibiana kuwa ilikuwa ni siku tu, au baadhi yake. Lakini wakawa washalala miaka hamsini, takriban.
Walipopambazukiwa, hammad! washaibiwa, washaporwa, washanyanganywa. Kila kilichokuwa chao kilihauliswa kikawa si chao tena, na kilichobaki pao kikabaki pao bila ya kuwa chao. Jina lao lilibaki kama lilivyokuwa, ila halikuwa tena na maana na ile sharafu yake ya mwanzo, kwani lilipovuka n’gambu tu Mzanzibari ilibidi alishereheshe ili muambiwaji aweze kufahamu Zanzibar ni nini, na ipo wapi. Ilibidi aseme, mathalan, “Zanzibar imo ndani ya Tanzania”. Wengine hawakuipenda sherehe hii ingawa ndio ilikuwa rahisi kufahamika, hivyo wakaamua kuikwepa na kutumia ya “Zanzibar ni visiwa vilivyopo kwenye mwambao wa pwani ya Afrika ya Mashariki. Vipo karibu na Kenya”.Sherehe hizo, na nyinigine, hazikubadilisha ukweli kwamba Zanzibar ilishaliwa na Zimwi, ilikuwepo kinadharia tu, ila katika uhalisia ilishatoweka.Katika kiza totoro cha usiku mrefu Wazanzibari nao wakapata tabu ya kujitambulisha kwa watu wengine duniani wenye tambulisho zao za kitaifa. Katika ndimi zao [Wazanzibari] bado jina la Zanzibar lilitamkika vizuri, na mtu alijihisi kujiramba kwa utamu wake zama alipolitamka. Ila halikutosha kuusema utaifa wa Mzanzibari, kwa maana halikuwemo katika daftari la tambulisho za kitaifa za dunia. Badala yake Wazanzibari wakabatizwa kwa jina lisilo lao, jina wasilolitaka. Wako waliolitumia jina lao la ubatizo, na kuna wale walioasi, licha ya kuwa na stakbadhi ya ubatizo, kitabu cha kijani, ambamo ndani yake waliandikwa kuwa wao si Wazanzibari, bali ni watu wengine, kwa maana Zanzibar haikuwepo.Katika Zanzibar ya asili, Wazanzibari walijiamulia mambo yao bila ya kuingiliwa. Walipanga na kupanguwa wenyewe, wakafanya kila lililokuwa na maslahi kwa Zanzibar yao kwa ridhaa zao na mapenzi ya Zanzibar yao. Ila ilipokuja Zanzibar ya kiza, hayo nayo yakapotea arijojo kama ilivyopotea Zanzibar yenyewe. Imamu wa Masjidi Rikunda hakuchaguliwa tena na maamuma wa Rikunda, bali ilitoka amri kutoka kwa makasisi wa nchi nyingine na kuwaambia Wanarikunda kwamba chaguo lao halikuwa sahihi, na badala yake makasisi ndio waliochagua maimamu wa kuongoza swala- za sunna na faradhi- katika Masjidi Rikunda na miskiti mingine ya Zanzibar.Kilichobaki Zanzibar ikawa ni hadithi na vitabu vya tarikhi vilivyosimulia haiba na uzuri wa Zanzibar ya asili. Mitaani ungeweza kusikia sifa za Zanzibar zikisimuliwa kwa wale akina sisi –tusio bahatika kuiona Zanzibar ya asili. Tungeambiwa, “Zanzibar bana, ilikuwa ni dola kubwa iliyotapakaa mpaka Kongo na baadhi ya sehemu za Somalia mpaka Msumbiji”. Au ungesikia “Zanzibar ilikuwa kitovu cha elimu na ustarabu wa kiislam. Watu walitoka Azhar kuja kusoma ilmu Zanzibar. Au “Zanzibar imekuwa na taa za umeme barabarani kabla ya London… Zanzibar ndio nchi ya mwanzo kuwa na TV ya rangi kwa Afrika. Na simulizi za sifa kadhaa wa kadhaa ya jamii hiyo ambazo zilileta maumivu zaidi kuliko afuweni.Hakuna usiku usiogongana na alfajiri. Na alfajiri kukumbatiana na asubuhi. Na ndio wakati huu uliopo sasa. Ni asubuhi. Kushapambazuka. Wazanzibari washaamka. Wanajaribu kuisahau ndoto yao mbaya waliyoiota kipindi cha miaka hamsini waliyolala. Ndoto-kweli. Wanaiangalia nchi yao ishararuliwa raruraru. Haijulikani mbele wala nyuma. Umasikini umetawala. Maneno kama uchumi, biashara, balozi na sera ya nje hayatumiki tena. Lugha ishapotea. Tarabu ishageuzwa sindimba. Wazee wa kishihiri wauza kahawa kwa mideli wakiwa na mavazi yao rasmi hawapo tena, nafasi zao zimechukuliwa na wavamizi wasiojua hata maana ya usafi. Watu wasiokuwa wao ndio waliojazana, na wale wao hawapo. Washaliwa na Mazimwi. Waliopo hajulikani mgonjwa wala mzima, wote sawa. Kuna wanaojiona wazima kumbe ni wafu. Maiti kwenenda maskini! Sura zao kama zilizotopewa. Hajulikani aliae wala achekae. Wote sawa maskini!.
Katika hali hii ndipo wale waliosalia wanaamua kuizaa upya Zanzibar. Wanafanya kila waliwezalo ili kuhakikisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar inarudi katika hadhi yake ya nusu karne iliyopita. Midahalo, makongamano, mashairi, mafumbo na kila aina ya mikakati inatumika kuhakikisha Zanzibar mpya na salama inazaliwa. Katika uwanja wa Tahrir wa Zanzibar, wanasiasa si waongozaji tena, bali ni waskilizaji. Wazanzibari sasa ndio wanaotumia viriri, na kupiga mbiu ya mgambo ya uwokozi wa Zanzibar.
Ila katika mazazi haya – kama vilivyo vizazi vingine- kuna maumivu makubwa ambayo yatawapata Wazanzibari. Kuna wachawi ambao tangu sasa wanataka kumhujumu mtoto atakaezaliwa, na wamo mbioni kulitekeleza hilo. Wazanzibari watatishwa, kwamba huenda mtoto wakampoteza. Watapoteza damu, watasumbuliwa, watabughudhiwa na watasubukuliwa. Na kuna kipindi wakunga wao watajifanya wakali, ukali utakao wapa mori Wazanzibari. Wazanzibari wataisikia sauti inayowaambia: “Vuta pumzi kwa nguvu…fumba mdomoo… sukumaa!!” Hatimae mtoto atazaliwa. Tukichukue kitoto chetu, tukibimbe, tukishum na tukilinde. Mafisadi na wenye vyoyo vya roho tuwaache na mashaka yao.
Tuanze safari mpya.

No comments:

Post a Comment