Saturday, June 16, 2012

MINAFIIKI NA MIJITU ILIYOHADAIKA NA DUNIA YAJAJU KWA KUPONDA UISLAMU NA DINI YA KISLAMU ILI KUHIFADHI THULMA NA UNYANGANYI WALIO ZOEA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAONI YA VYAMA VYA UPINZANI VYA TADEA, SAU, NLD NA AFP KUHUSU TUKIO LA VURUGU LILILOTOKEA HIVI KARIBUNI.
Ndugu waandishi wa habari na wananchi,
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana nanyi leo tukiwa katika hali ya uzima na afya. Pili napenda kushukuruni nyinyi kwa dhati kwa kukubali mualiko wetu na kuhudhuria kwa wingi kwenye mkutano wetu huu muhimu kwa wananchi wa Zanzibar hasa wale wenye kuitakia amani, utulivu na maendeleo nchi yetu hii.
Ndugu waandishi na wananchi,
Mtakumbuka kuwa Mei 26, mwaka huu, Zanzibar tulishuhudia tukio lisilo la kawaida la uvunjwaji wa amani lililofanywa na wenzetu ambao tumekuwa nao katika harakati mbali mbali za maendeleo. Wananchi hawa walisababisha maduka kuvunjwa, nyumba za ibada kuchomwa moto, mipira ya gari kuchomwa barabarani na kusababisha uharibifu wa miundo mbinu ambayo imejengwa na wageni waliokuwepo nchini. Watu walishindwa kufanya shughuli zao hasa maeneno ya mjini. Mitandao na vyombo vyote vya habari vilijaa habari mbaya kuhusu Zanzibar. kwa ufupi hali ilikuwa ni ya kutia aibu na mbaya sana kwa upande wetu hasa ukizingatia taswira nzuri iliyojengeka chini ya uongozi wa pamoja wa Serikali yetu. Tunahisi ushirikiano bado unahitajika sana katika kuweka hali ya utulivu sambamba na juhudi kubwa ambazo Serikali imekuwa ikizichukua. Kwa moyo safi kabisa, leo hii tumeamua kuitisha mkutano wetu huu maalum kuzungumzia hali halisi iliyojitokeza ndani ya nchi yetu.
Hatuna lengo la kulaumu upande wowote kutokana nay ale yaliyotokea, lakini ili kuepuka masuala yale yasitokee tena, ni vyema tukaangalia chanzo cha tukio lenyewe na mazingira yake ili baadae tuweze kuchukua hatua zinazofaa. Sote ni mashahidi kwamba sababu ya vurugu ni mihadhara na maandamano yaliyokuwa yakiendeshwa na Jumuiya ya Uamsho. Harakati za muda mrefu za Jumuiya hiyo ndizo hatimaye zilitoa mianya kwa watu wengine kuifikisha pabaya nchi yetu, ambayo mwelekeo wake kiuchumi ilishaanza kuonesha mafanikio makubwa. Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislam yenye kuzungumzia Uamsho ni Jumuiya ya Kidini kwa mujibu wa usajili wake.
Mimi binafsi nashangaa kuona kwamba pamoja na taratibu nzuri zilizowekwa za watu kutoa maoni yao kwa salama na amani, Jumuiya hii inahamasisha watu kufanya mambo kinyume na utaratibu uliowekwa. Harakati za Jumuiya hii zilianza kwenye Misikiti, kuingia mitaani na sasa viwanjani. Hii inaonesha dhahiri kwamba kundi hili lina agenda ya siri na lieltwa makusudi kuchafua hali ya siasa, amani na utulivu na nchi yetu, na dalili za vurugu zimeanza kuonekana.
Sisi kama wanasiasa tunafahamu kwamba jina la Jumuiya hii linatumika kama kivuli, lakini harakati hizi zinaendeshwa na viongozi ambao wamo ndani ya Serikali na ndani ya vyama vya siasa. Tunalaani vikali vitendo vya Jumuiya hii kwani havina maslahi ya nchi yetu. Aidha, tunafahamu kwamba Jumuiya hii inapata ufadhili wa kifedha kutoka nje ya nchi.
Ndugu Waandishi,
Ushahidi wa haya ninayoyazungumza hauhitaji taaluma kubwa kuweza kujua chama kipi cha siasa kinahusika. Harakati za Jumuiya hii zinaendeshwa kwenye maeneo na wafuasi wa Chama hicho ninachokizungumza. Lakini hata viongozi wake wanashindwa kuzilaani hadharani harakati za Jumuiya hii, licha ya athari zilizojitokeza za kuharibu vibaya jina na sifa ya visiwa hivi, vinavyoendelea kujijengea umaarufu katika maendeleo. Nchi nyingi zimevutiwa sana na hatua zinazochukuliwa na nchi yetu katika kuleta maendeleo.
Kupitia mkutano huu tunawaomba sana Wananchi wa Zanzibar, Unguja na Pemba na wale wanaoishi nje ya Visiwa hivi kuwa makini sana na kundi hili. Tunawatanabahisha akinamama wasikubali kutumiwa namna hiyo kwani hatua hiyo inaweza kuwaletea maafa. Dalili zinaonesha kuwa viongozi hao wako tayari kusababisha maafa na kuwatupia lawama watu wengine mradi tu waweze kufikia malengo yao. Ninawasihi sana wasicheze ngoma wasiyoijua. Sehemu nyengine duniani, vikundi kama hivi vimesababisha matokeo mabaya sana na kusababisha maafa makubwa. Kwa mfano Alkayda, Bokoharam kule Nigeria, na Al-Shabab kule Somalia. Hali za nchi zenye makundi haya zinasababisha kuondoka kwa hali ya usalama na amani.
Ndugu Waandishi wa Habari na Wananchi,
Tumepata taarifa kuwa kundi jengine la wananchi wa Zanzibar linalopendelea Muungano tayari linaanzisha harakati dhidi ya wale wanaoupinga Muungano, wakidai kuwa udongo uliochanganywa katika kuunganisha nchi mbili hizi ulitoka Unguja na Tanganyika na sio Pemba. Kwa msingi huo basi wananchi wa Pemba hawahusiki na Muungano, kundi hilo linadai kuwa wasiotaka Muungano ni Wazanzibari kutoka kisiwa cha Pemba. Kutokana na sababu hizo, kundi hilo linawaomba wasioutaka Muungano waondoke Unguja kwa hiyari yao warudi kwao walikotoka.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Hizi ni athari za ubaguzi na kwa kweli ni hatari kwa hatma ya nchi yetu. Tunapaswa tukumbuke kuwa Zanzibar kwa muda mrefu tulikuwa tumefarikiana kwa sababu za kisiasa. Mungu ametujaalia miaka miwili iliyopita tumekaa pamoja na tumeondosha tofauti zetu na matunda yake yameonekana kwa kipindi kifupi sana katika kuinua pato letu la Taifa sote tumeshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya Kilimo na hasa Karafuu na utalii nchini.
Taarifa za uchumi zinaonesha kuwa tumepata mafanikio makubwa ya kukuza uchumi wetu ndani ya kipindi kifupi. Kwa mujibu wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/2013, pato la mtu mmoja limeongezeka kutoka wastani wa Tsh. 782,000 mwaka 2010 na kufikia Tsh. 960,000 mwaka huu.
Haya ni mafanikio makubwa ambayo hayakupatikana katika nchi nyengine duniani. Kwa wenzetu wa Chama Tawala – CCM tayari wameshavuka lengo lao la miaka mitano katika muda wa miaka miwili tu. Wao walilenga pato la mwananchi lifikie wastani wa Tsh. 884,000 ifikapo 2015.
Ndugu Wanahabari,
Hapa ndipo inapokuja hofu kwamba kuna mkono wa siasa kuvuruga mafanikio haya hasa kwa vile hayo ni matunda yanayotokana na hali ya amani, utulivu na mshikamano wa Wazanzibari, ambapo wananchi waliweza kuendelea na shughuli zao za uzalishaji na biashara bila ya sumbufu, wageni waliendelea kufurika nchini na wawekezaji wameedelea kuwekeza.
Ndugu Waandishi,
Mafanikio ya kukua kwa uchumi wetu yanaendelea kutupa funzo juu ya umuhimu wa kuilinda amani, utulivu na mshikamano wetu ambao umetujengea sifa kubwa. Hivyo napenda kuitumia fursa hii kwa niaba ya vyama vya upinzani kusisitiza mambo yafuatayo:-
1. Tunaiomba Serikali kuangalia usajili wake Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislam kutokana na kwenda kinyume na masharti ya usajili wao na kwamba mwelekeo wake ni kuirejesha Zanzibar kwenye mafarakano, vurugu, siasa za chuki na uhasama miongoni mwa Wananchi.
2. Serikali ichukuwe juhudi maalum kuhakikisha kuwa vurugu zilizotokea hazitokei tena, na vyombo vya sheria viwachukulie hatua kali za kisheria wale wote watakaohusika katika kuanzisha na kuendeleza harakati za uamsho za kupinga Muungano.
3. Tuweke mbele maslahi ya nchi yetu kwa maslahi yetu na vizazi vijavyo. Kwa kufanikisha hili, tujitahidi kadri tuwezavyo kuepuka vitendo vyote ambavyo hatimaye vitavuruga mshikamano wetu, amani na utulivu uliopo.
4. Tunawasihi Masheikh na Maulamaa wote wasitumie dini kama ngao ya kuwapotosha wananchi na kusababisha vurugu ndani ya nchi.
5. Tunawaomba Wananchi walioanza harakati za kutaka kuigawa nchi misingi ya uzawa, kuachana na kasumba hizo kwani hazina hatma njema miongoni mwa Wazanzibari.
6. Tunawaomba viongozi wote wa kisiasa kulaani vikali harakati za Uamsho na vitendo vyote vyengine kuashiria uvunjifu wa amani kama ambavyo amekuwa akifanya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Pili wa Rais.
7. Tunaungana na viongozi wetu wa vyama siasa na Serikali waliojitokeza hadharani kulaani matukio yenye mwelekeo wa uvunjifu wa amani na tunatoa wito kwa wale ambao bado hawajafanya hivyo wafanye kwa haraka na kwa nguvu zote kwani hatua hiyo itaonesha nia yao ya dhati katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.
8. Tunapongeza kwa dhati juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa chini ya Uongozi wa Dkt. Ali Mohammed Shein kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimaendeleo katika kipindi kifupi tokea Serikali hiyo iingie madarakani.
DAIMA TADEA UMOJA NA AMANI
Tunawashukuru sana kwa kutusikiliza

No comments:

Post a Comment