Tuesday, June 12, 2012

SHIRIKA LA UTANGAZAJI NCHINI OMAN,LAAHIDI KUISAIDIA ZBC-TV-WANAOTAKA KUNYWA SUMU MUKANYWE SASA


Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Mhe Said Ali Mbarouk, akizungumza na ujumbe wa Wafanyakazi wa TV Oman ulipofika ofisini kwake kujitambulisha kwa ujio wao Zanzibar wa kutengeneza Program ya Utalii wa Zanzibar na Majumba ya Mji Mkongwe na sehemu za Historia ya Zanzibar kuitangaza Kitalii Oman, kushoto kwa Waziri Balozi wa Oman Zanzibar Mansoor Al Busaid na Wafanyakazi wa TV Oman.


UONGOZI wa Shirika la Utangazaji nchini Oman, umeahidi kulisaidia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC – TV) katika nyanja mbali mbali, ikiwemo za kiufundi na kitaaluma, ili liweze kuharakisha juhudi zake za kutoka kwenye mfumo wa Teknolojia ya habari wa Analogy na kuelekea ule wa Digital.
Ahadi hiyo imetolewa jana na Uongozi wa Shirika hilo, wakati ulipokutana na kubadilishana mawazo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar, Said Ali Mbarouk, ofisini kwake Mnazi Mmoja.
Ujumbe huo wenye timu ya waandaji wa filamu, upo nchini kwa ajili ya kutayarisha filamu katika maeneo ya kihistoria, hususan Mji Mkongwe, ambapo pamoja mambo na mengine filamu hiyo itaisaidia kuitangaza Zanzibar kiutalii.
Ujumbe huo ambao uliambatana na Balozi mdogo wa Oman nchini, Mansoor Al Busaid, umeahidi kukutana na Menejment ya ZBC, ili kubadilishana uzoefu pamoja na kuangalia maeneo yepi ambapo Shirika hilo linaweza kusaidia kiufundi na kitaaluma.
Mmoja wa viongozi wa Shirika hilo, Ebrahim Al Yahmad alisema ZBC inaweza kunufaika sana kuwepo mashirikiano na Shirika hilo na kuharakisha safari yake ya kuelekea Digital,kwa kuzingatia kuwa tayari Oman inaondoka katika mfumo huo (Digital ) na kuelekea mfumo wa DH.
Alisema Shirika la Utangazaji la Oman, (ambalo lina Waziri wake) limepiga hatua kubwa sana katika nyanja ya mawasiliano ya habari, hivi sasa likiwa tayari limejenga Studio kubwa ya kisasa, huku likiendelea na maandalizi ya program za mafunzo kwa mfumo wa DH.
Alisema katika dhana ya kuendeleza mashirikiano kati ya mashirika hayo mawili, vijana wa Zanzibar wataweza kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzao wa Oman na kuona vipi wanafanya kazi.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo alisema hatua ya kuja kwao nchini na kuandaa filamu katika maeneo ya kihistora kutaisaidia sana kuutangaza Utalii wa Zanzibar, kwa kujua kuwa Zanzibar ni eneo bora kwa biashara ya Utalii.
Aidha alimwomba Waziri Mbarouk kusaidia upatikanaji wa nakala za magazeti ya zamani ambayo yaliwahi kuchapishwa hapa nchini, au kumpata mtu ambae anaweza kueleza kwa ufasaha juu ya uwepo wa magazeti hayo.
Mapema Waziri Mbarouk alisema Serrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu na ndugu zao wa Oman.
Alisema hatua ya Oman TV kuja nchini kwa ajili ya kuandaa filamu maalum katika maeneo ya kihistoria, ni hatua muafaka inayounga mkono juhudi za Serikali katika kuutangaza utalii wa Zanzibar hadi nje ya mipaka na kufanikisha ‘dhana ya utalii kwa wote’.
Alisema mbali na ujumbe huo kuangalia eneo la Mji Mkongwe, pia wapaswa kuangalia maeneo zaidi ya kihistoria, ikiwemo msitu wa Jozani, magofu ya Mtoni, fukwe zenye kupendeza pamoja na magofu ya Mazrui yalioko Chwaka kijiji cha Tumbe, kisiwani Pemba.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii, na kutoa mfano wa Hifadhi yam situ wa Jozani, wenye kupatikana Kima Punju, wanyama ambao hawezi kupatikana mahala popote pale Duniani, isipokuwa Zanzibar.
Aidha aliyasifia magofu yalioko Chwaka Tumbe, kwa kusema kuwa ni eneo kubwa, linalovutia na lenye historia inayosisimua, likielezwa kuwa ni mji uliopata kuishi watu kutoka Oman kabla ya kuja kwa Wareno.
Akizungumzia kuwepo kwa magazeti ya zamani, Mbarouk alisema kuna idadi kubwa ya magazeti yaliokuwa yakichapishwa hapa Zanzibar miaka mingi iliopita, na kuuahidi ujumbe huo kupata baadhi ya nakala zake pamoja na watu wanaoelewa historia ya kuwepo kwa magazeti hayo.

No comments:

Post a Comment