Tuesday, June 26, 2012

WAWAKILISHA NCHINI ZANZIBAR WAANZA KUTOKA USINGIZINI NA KUTAKA PIA MUUNGANO FEKI UVUNJWE


SUALA la Muungano limezidi kutawala mijadala katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea huku baadhi ya wajumbe wakitamka wazi kuwa hawataki Muungano. Katika kikao hicho ambacho tayari kimepitisha bajeti kuu ya serikali ya Zanzibar wajumbe wa baraza hilo jana walijadili bajeti ya ofisi ya makamo wa pili wa rais wakitaka serikali isimamie kupata uhuru zaidi wa kiuchumi katika muungano.
Ofisi ya makamo wa pili wa rais ndio inayotambulika kuwa msimamizi mkuu wa shughuli za serikali ndani ya baraza la wawakilishi.
“Mheshimiwa Naibu Spika mimi niseme wazi kwanza kwamba sitaki muungano na katika kitu ambacho nakichukia sana basi ni huu muungano maana kwa miaka 48 ya muungano huu kila siku tunaambiwa kuna kero wala hazitatuliwi basi ni uvunjike tu” alisema Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma.
Juma alisema kupigania haki ya Zanzibar haimaanishi chuki katika muungano na kwamba muungano uliyopo ni wa nchi mbili huru ambazo lazima kuwepo na haki sawa kwa pande zote mbili.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM) Makame Mshimba Mbarouk alisema “Lazima mheshimiwa makamo wa pili wa rais tuamke muungano huu, siwo…tunataka maslahi ya Zanzibar na tunataka haki zetu zote kuanzia mapato ya gesi. Nitazuwia bajeti hii mpaka niambiwe katika accounti ya Zanzibar imepata kiasi gani kwa mapato ynayotokana na gesi maana ni haki yetu” alisema Mbarouk.
Abdallah Juma Abdallah Mwakilishi wa Jimbo la Chonga (CUF) alisema viongozi wa serikali na vyama wamewekwa madarakani na wananchi hivyo sio sahihi kubeza maoni ya wananchi ambayo hawautaki mfumo huu wa muungano na kuahidi kusimama pamoja na wananchi wa jimbo lake iwapo waamua kuukataa.
“Kiongozi yeyote kuanzia rais, wabunge na hata sisi wawakilishi tumewekwa hapa kwa kuchaguliwa na wananchi na tunasimama kuwasilisha maoni ya wananchi sasa ikiwa wananchi watasema hawataki muungano, mheshimiwa naibu spika lazima tusimame nao” alisema Mwakilishi huyo na kuongeza.
“ Mimi kama mwakilishi wa chonga nasema wananchi kama watasema hawataki muungano basi nitasimama nao na nitakuwa bega kwa bega na kwa sababu wamenichagua kwa kuniamini na pia nahitaji tena kurudi katika nafasi hii na nikidharau maoni yao au matakwa nayo hawatanirejesha tena” alisema Abdallah.
Mwakilishi wa nafasi za wanawake Asha Bakari Makame (CCM) kwa upande wake aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kutoka CCM na CUF kwamba wanadhamana kubwa ya kuwatetea wazanzibari bila ya kuhofia nafasi zao na kwamba wazanzibari wanawatazama wao kwa kuwaamini.
“Mheshimiwa naibu spika ni CCM na CUF pekee tuliyopo humu ndani wananchi wanatuamini na lazima turejesha imani kwa wananchi wetu ikiwemo suala kuu la kutetea Zanzibar ndani ya muungano…kero gani hizi zisizokwisha?” alihoji Asha ambaye aliwahi kuwa waziri wakati wa SMZ .
Asha Bakari ambaye ni naibu mwenyekiti wa umoja wa CCM Tanzania (UWT) alisema ni umoja na mshikamano miongoni mwa wazanzibari ndio silaha pekee itakayoweza kuwavusha wazanzibari katika kudai maslahi yao ndnai ya muungano.
“Mimi siogopi chochote na kwa umri huu tena naona lolote litakalonifika ni sawa tu lakini nawaambia wenzangu kwamba tuiteteni Zanzibar na tusiwe na woga maana wengine wamezowea kututisha” alisema kwa kutoa tahadhari.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu alisema serikali ya Zanzibar inafanya makosa makubwa ya kuridhia kila kitu ambacho kinatolewa na serikali ya muungano.
“Ni muda mrefu wimbo ndio huo huo wa ahadi ya kushughulikia kero za muungano na kero zenyewe hazishi …kwa sababu hata hizo kamati hazipo kisheria za kutatua kero” alisema.
Jussa alitaka viongozi wa serikali kuwaunga mkono wananchi katika madai yao ya msingi kwa kuwaelekeza nini waseme wakati wa kutoa maoni ya katiba mpya ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na kwamba bila ya kutoa muongozo wananchi watababaika.
“Mimi nina imani kubwa na serikali yangu ya umoja wa kitaifa na ninaipenda lakini naomba itoe msimamo hapa katika kuwaelekeza wananchi wakadai nini wakati wa tume itakapokuja kukusanya maoni” alisema Jussa na kupigiwa makofi na wajumbe wenzake.
Aidha mwakilishi huyo aliwataka wananchi na viongozi wa siasa kutokuchanganya misimamo ya siasa pamoja na dini katika kutoa maoni kwani inaweza kuharibu na kuwagawa wazanzibari.
Awali akiwasilisha hutuba ya bajeti ya makamo wa pili ya kuomba kuidhinishiwa shilingi billioni 12.3 kwa mwaka wa fedha za 2012/2013 Waziri wa nchi Ofisi hiyo Mohammed Aboud Mohammed alisema juhudi zimekuwa zikiendelea katika kutatua kero za muungano na kwamba wajumbe wa baraza la wawakilishi wawe wavumilivu.

No comments:

Post a Comment