Tuesday, October 2, 2012

BALOZI MDOGO WA SEREKALI YA TANGANYIKA NCHINI ZANZIBAR AMWAGA SUMU WILAYA YA KASKAZINI B


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi  na balozi wa nchi ya Tanganyika nchi Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, amesema serikali ya Zanzibar imshajitosheleza katika mfumo wa serikali yake na haina haja ya kuwa na serikali ya mkataba kwani kufanya hivyo ni sawa na kutaka kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja uliofanyika katika Hoteli ya Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini’B’ Unguja.
Balozi Seif, alisema muundo wa serikali ya Zanzibar tayari umetoa fursa ya kuwa na vyombo muhimu vya juu ambavyo vimeweza kuunda serikali na hakuna haja ya kutaka kuwapo kwa serikali ya Mkataba ambayo ni sawa na kuuvunja Muungano.
Akifafanua kauli hiyo Balozi Seif, alisema mfumo wa serikali ya Zanzibar ndani ya Katiba umeruhusu kuwa na Katiba yake, Baraza la Wawakilishi, Muhuri, Bendera, Mawaziri, Wawakilishi na Wabunge jambo ambalo tayari mfumo huo umejitosheleza.
Alisema matamshi yanayoendelea kutolewa hivi sasa kupendekezwa kuwapo kwa serikali ya Mkataba ni sawa na kuuvunja Muungano na kwa wanachama kuanza kuiona hatari hiyo na kuyakataa mapendekezo hayo.
Alisema sera ya Chama Cha Mapinduzi ni kuona hadi hivi sasa inaendelea na msimamo wake wa kuimarisha Muunganao wa serikali mbili na haitakuwa busara kuona wanachama wa CCM wanakumbwa na sera zinazoendana kinyume na serikali yao.
Alisema ndani ya serikali ya Muungano Wazanzibari wameweza kutanua mambo mbali mbali ya akimaisha, zikiwemo biashara na umiliki wa ardhi na kuishi kwa uhuru ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Alisema kutokana na fursa hizo ni vyema kwa wanachama wa CCM kuona hawawi chanzo cha kuvunjika kwa Muungano na badala yake wawe wenye kuuenzi na kuudumisha.
Alisema kinachoonekana kwa wanaohubiri suala hilo wana lengo la keleta matakwa ya watu binafsi na sio faida kwa ajili ya kuimarisha serikali ama Wazanzibari.
“Wameanza kuniita Balozi wa Tanganyika ndani ya Zanzibar sasa tujiulize hawa wengine wao ni mabalozi wa wapi, tusionyosheane vidole bila ya kujianagalia sisi wenyewe” Alisema Balozi Seif.
Akizungumzi juu ya uchaguzi huo balozi Seif, aliwataka wanachama wa Chama hicho kuhakikisha wanatumia nafasi zao vyema kutimiza matakwa yao ya kuchagua viongozi wazuri.
Alisema Chaguzi za Chama ni sawa nitimu za mpira kufanya usajili wake na chaguzi unaoendelea kufanyika hapa nchini ni kwa ajili ya kukivusha Chama katika uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema CCM hivi sasa inataka viongozi bora na waliomakini wataoweza kukisababishia Chama kufunga magoli katika uchaguzi Mkuu ujao na sio kuchagua wataolizamisha jahazi la Chama hicho.
Balozi Seif alisema haitapendeza kuona baada ya uchaguzi huo kumalizika kunajitokeza viashiria vya kukatiana rufaa hapo baadae na ni lazima wahakikishe wanakuwa wamoja baada ya kukamilisha kazi hiyo.
Alisema dhamira aya Chama cha Mapinduzi hivi sasa ni kuona inapata viongozi wataoendeleza kukitetea chama bila ya kutafuna maneno ama woga kuelezea msimamo wa CCM katika kuimarisha chama na serikali zote mbili
Pamoja na amani ya nchi.
Balozi Seif, aliwataka waliokosa kuchaguliwa katika uchaguzi huo kutokata tamaa kwani CCM imekuwa na uhuru wa demokrasi inayowataka wanachama kuchagua mtu ambaye wataona anafaa kuendelea na mchakato huo.
“Sisi Chama Cha Mapinduzi ni lazima ilani inasema kuimarisha Muungano wa serikali mbili tunataka viongozi wataoutetea sera hiyo ni lazima hakuna kutafuna maneno kwa kuogopa kulisema hadharani kwani tayari baadhi ya wapinzani wameanzisha sera ya kutaaka Muungano wa serikali ya Mkataba na wameshaeleza hadharani sasa nanyi semeni Muungano gani mnautaka.
Aidha, Balozi Seif alisema hivi sasa serikali ya Muungano inaendelea kupokea maoni ya Wananchi juu ya uundwaji wa Katiba mpya ambapo mwezi ujao mchakato huo unatarajiwa kufanyika mwezi ndani ya Mkoa wa Kaskazini.
Kutoakana na hali hiyo Balozi Seif, aliwataka wanachama hao kuona wanatumia nafasi waliyonayo kushiriki kwa wingi katika utoaji wa maoni pale utapoanza kufanyika katika Mkoa huo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanachama wa Wilaya hiyo Mzee wa Chama Ali Ameir Mohammed, alisema wanachama wa CCM wanapaswa kutambua bado kuna maadui wa Chama cha Mapinduzi na ni lazima watafute njia za kuwaepuka ili kuifanya nchi ibaki katika amani na mikononi mwa wazanzibari.
Alisema wanaodai maslahi ya Chama yaje mwisho ni sawa na wavurugaji wa amani ya nchi na waliothubutu kueleza hilo hawama uchungu kuzitetea sera za Chama cha Mapinduzi na wanahitaji kutoshwa.
Mkutano huo ulifanyika kwa kwenda sambamba na Mikoa mengine ya Tanzania kupitia ngazi hiyo.

No comments:

Post a Comment