Saturday, October 13, 2012

SISI NI WAZANZIBARI TUNA PASSPORT YETU HATUTAKI PASPOTI LA KITANGANYIKA.


Azimio la Wazanzibari Waliohudhuria Kikao Cha Kuzungumzia Mustakbal wa Zanzibar, Ukumbi wa Rumaisa Hotel.

Sisi Wazanzibari tuliohudhuria kikao cha kuzungumzia Mustakbal wa Zanzibar, ukumbi wa Rumaisa Hotel, Malindi baada ya kutathmini hali halisi ya Zanzibar – hususan kuhusiana na uhusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika chini ya mfumo wa Muungano wa Katiba wenye muundo wa “Taifa Moja Serikali Mbili”, kama ilivyo hivi sasa na kama ilivyo kuwa kipindi cha takriban miaka hamsini; na baada ya kuzingatia umuhimu wa mchakato wa kutafuta katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mustakbal wa Zanzibar, na umuhimu wa kuwatafutia haki Wazanzibari kwa kupitia utaratibu wa amani na demokrasia, ambao msingi wake ni mawazo ya walio wengi yanatawala, tunaazimia ifuatavyo:

• Kudumisha umoja wetu, na kulinda maridhiano ya Wazanzibari; halikadhalika kugombania maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari bila ya kujali itikadi zetu za kisiasa, kabila, dini, jinsia au umri.
• Kwa kuamini kwamba mfumo muafaka wa uhusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika ni Muungano wa Mkataba baina ya mataifa mawili: kujitahidi kwa juhudi zetu zote kuhakikisha kwamba Tume ya Katiba inafahamishwa kwamba wazanzibari wanahitaji Zanzibar yenye mamlaka na madaraka kamili kitaifa na kimataifa, kwa maslahi ya Wazanzibari wote; halikadhalika kuhakikisha kwamba Wazanzibari wote wanafahamu kwamba ni haki yao pekee kuamua hatima ya nchi yao, kwani Zanzibar ni mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa – umoja unaolinda wanachama wote, na mahusiano baina ya wanachamana kulingana na kanuni zake za kidemokrasia, kujitawala, na usawa baina ya mataifa yote bila ya kujali ukubwa au idadi ya watu.
• Kwa kuamini kwamba ni muhimu kuunganisha juhudi zetu: kuimarisha Umoja wa pamoja uliopo Zanzibar unaojumuisha taasisi zote za Wazanzibari zenye lengo na nia moja – kuhakikisha kwamba Zanzibar inatendewa haki na inaendelea kwa manufaa ya Wazanzibari wote; kwani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyoasisiwa Aprili 1964 uliunganisha mataifa mawili huru, na lengo letu ni kuhakikisha ya kwamba Zanzibar inarejesha haki yake ndani ya Muungano wa Mkataba baina ya Zanzibar na Tanganyika ambao utakua ndio mwanzo wa ushirikiano wa kudumu na wenye kuleta faida kwa nchi zetu mbili.
Kwa hali hii huu ni mwito kwa Wazanzibari kuimarisha Umoja wetu, kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu, na kuhakikisha ya kwamba harakati zetu za kuitafutia uhuru na maendeleo Zanzibar zinaendelea, kwa niaba ya Wazanzibari wote, na kwa ajili ya maendeleo yetu na usawa na udugu miongoni mwetu.
JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR– KWANZA !

No comments:

Post a Comment