Tuesday, October 2, 2012

WANANCHI WA NCHI YA TANGANYIKA WASEMA VIONGOZI WENYE UTENDAJI MBOVU WAPIGWE RISASA AU WANYONGWE HADHARANI.


KAMISHINA wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Paramaganda Kabudi amesema wananchi wengi wanachukizwa na utendaji mbovu wa viongozi kiasi kwamba wanapendekeza adhabu ya kupigwa risasi kwa wale watao patikana na hatia ya kwenda kinyume na maadili ya uongozi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Profesa Kabudi alisema suala hilo ni miongoni mwa maoni ya wananchi ambayo yamejitokeza kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya, unaoendelea sehemu mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau kuhusu marekebisho ya sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 ulioandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Profesa Kabudi alisema wananchi wengi wanaelekea kuchoshwa na tabia za viongozi.
“Watu hawafurahii kabisa juu ya viongozi wanao enda kinyume na maadili ya uongozi na wengine wamependekeza wanyongwe     ama kupigwa risasi hadharani,” alisema Profesa Kabudi.
Aliongeza: Sisemi naunga mkono maoni yao, lakini inaonyesha watu wana ghadhabu na wamechoka.
Alisema kuna haja ya Katiba kuweka msingi madhubuti kwa ajili ya kuwa na maadili yanayomfunga na kumbana mwananchi wa kawaida pamoja na kiongozi ambaye amepewa dhamana.
Profesa Kabudi alishauri kuwa kiongozi yeyote anayeona dalili za wananchi kumkataa ni afadhali kujiondoa mwenyewe kuliko kusubiri fedheha.
Wakati mwingine ikibidi jambo zuri la busara na heshima ni kuondoka kabla ya fadhaha,alisema.
Alipendekeza pia katika mabadiliko ya sheria hiyo, suala la biashara na siasa litenganishwe na kuhakikisha sheria hiyo inaendana na matarajio ya wananchi wale kwa kuzingatia utamaduni chanya wa jamii.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, mapendekezo mengine ni sekretarieti hiyo kupewa mamlaka kamili ya kuchunguza akaunti za viongozi ndani na nje ya nchi bila kutakiwa kupata kibali cha mahakama.
Mapendekezo mengine ni viongozi wa umma na familia wasiingie katika mikataba ya Serikali na taasisi zake pamoja na viongozi kutoshiriki kwenye majadiliano ama maamuzi ya mambo ambayo wanahusika.
Alisema sheria hiyo imekuwepo kwa muda mrefu lakini katika mazingira ya sasa inahitaji kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuhakikisha inaweka misingi ya jinsi gani nchi iweze kujiendesha katika miaka ijayo.
Pia alitaja mapungufu mbalimbali yaliyomo kwenye sheria hiyo kuwa ni kukosekana kwa mfumo unaomwezesha kamishna wa maadili kupata taarifa kuhusu zawadi za viongozi.
Kasoro nyingine ni za wananchi kutoruhusiwa kukagua madeni na mali za viongozi, jambo ambalo haliweki wazi uhuru wa kuhoji juu ya utajiri wa viongozi.
Vilevile alisema katika sheria za maadili ya viongozi hakuna kifungu kinachowalinda watoa taarifa na kusababisha wananchi kutoa ushirikiano mdogo kwa kuhofia kulipizwa kisasi.
Awali, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angella Kairuki alisema katika mazingira ya sasa kuna haja ya kupanua wigo wa kuifanya sheria hiyo iwamulike watumishi wa umma wasio viongozi.
Wapo watumishi wa umma ambao wamejilimbikizia mali nyingi zisizolingana na vipato vyao na wengine wanatumia ofisi zao kujinufaisha isivyo halali,alisema Kairuki.
Kwa upande wake, Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda alisema mkutano huo una lengo la kuchambua udhahifu uliomo katika sharia hiyo ili ipewe nguvu mpya itakayoleta tija katika utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment