Wednesday, December 5, 2012

DR KUMBI SHEIN 2015 ATAJITILIA KURA MWENYEWE ATASHINDA MWENYEWE ATAJITAWALA MWENYEWE WENZAKE WASHAMCHOKA


Aliyekuwa Waziri asiye wizara maalum kwenye Baraza la Mawaziri la Dk. Ali Mohammed Shein, Mansour Yussuf Himid, alifutwa kazi na bosi wake mnamo mwezi Oktoba. Inaaminika kwamba ni kutokana na msimamo wake wa kutaka mfumo wa Muungano ulio tafauti na ule unaotakiwa na bosi wake. Himid ni mmoja wa watu sita waliokuwa injini ya Maridhiano ya Wazanzibari kutoka upande wa CCM. Hilo lilikuwa dogo.
Kubwa likawa ni kukashifiwa kwa Rais Mstaafu na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Amani Karume, wakati na baada ya hotuba yake ya kihistoria kwenye ukumbi wa CCM, Dodoma. Msingi ulikuwa ule ule wa kuonesha maoni tafauti na ya chama chake kuelekea haki ya Wazanzibari kufanya maamuzi na kuheshimiwa maamuzi hayo linapohusika suala la Muungano.
Aliyechukuwa nafasi ya Karume, Dk. Shein akagongomelea msumari mwengine kwenye suala hilo, pale aliposema kwenye viwanja vya Kibandamaiti mwishoni mwa mwezi Novemba kwamba atasimamia muundo wa Muungano uliopo. Bila ya shaka, Dk. Shein alikuwa akipiga ndege wengi kwa jiwe moja kwa hotuba yake hiyo iliyojaa vijembe mbele ya maelfu ya wafuasi wake: Ndege wa kwanza alikuwa mtangulizi wake, Rais Mstaafu Karume, kwamba hata kama kutakuwa na maoni ya muundo mwengine wa Muungano ambayo yeye Karume alishauri yaheshimiwe, ajue kuwa hilo si wakati wa Dk. Shein akiwa rais na makamo mwenyekiti wa CCM.

Ndege wengine, ni wale Karume aliowaita – na baadaye wenyewe kujikubalisha – kuwa samani, yaani wahafidhina wa Zanzibar, ambao walimtukana Karume kabla, wakati na baada ya mkutano wa Dodoma, kwamba yu pamoja nao kwa msimamo. Ndege wa tatu walikuwa ni CCM Dodoma, ambao kwa kauli hiyo alitaka kuwaridhisha kwamba kazi sasa wamempa mtu ndiye anayeweza kuaminika kuilinda sera ya chama (au kwa usahihi zaidi sera ya Dodoma kuelekea Zanzibar).
Baada ya haya yote, mtu angelidhani kwamba Dk. Shein sasa ana nguvu za kutosha sasa kutoka kila nguzo ya kuitegemea, ukiwacha ile nguzo kuu yaani Wazanzibari walio wengi, ambao kwa kawaida ya siasa za CCM Zanzibar, huwa si nguzo muhimu kubakia au kuingia madarakani. Nakusudia kwamba tayari ana kofia zote mbili za ukuu wa chama na serikali, ana imani ya Dodoma (ambayo ndiyo iliyompatia kofia hizo) na ana mizizi kwenye nyoyo za wahafidhina wa Zanzibar.
Lakini, ikiwa nawe ni miongoni mwa walioamini hivyo, hebu sasa soma haya yafuatayo, ambayo yanatokana na mchakato wa maoni ya Katiba Mpya. Kupitia ukurasa wa Facebook, kuna hadithi ya kweli imesambazwa. Nayo inasema hivi:
“Katika waliotoa maoni Maungani (ilichanganywa na Shakani) alikuwa Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Yeye alisema anaunga mkono muundo wa Serikali mbili zilizopo lakini akasema mambo ya Muungano yabakie yale 11 ya mwanzo tu, na mengine yote 11 yaliyoongezwa baada ya 1964 yafutwe na yarejeshwe kwenye mamlaka ya Zanzibar.

“Katika mambo hayo 11 yaliyoongezwa baadaye alotaka Dk. Mwinyihaji yaondoshwe katika Muungano ni pamoja na sarafu, mabenki na fedha za kigeni, mafuta na gesi asilia, takwimu na leseni za viwanda, elimu ya juu, takwimu, baraza la mitihani la taifa, usafiri na usafirishaji wa anga, mahkama ya rufani, na vyama vya siasa. Hiyo maana yake hata CCM itavunjika au kutakuwa na CCM Zanzibar na CCM Tanganyika ikiwa suala la vyama vya siasa pia liondolewe katika mambo ya Muungano.
“Lakini raha zaidi ni kuwa aliya-challenge hata baadhi ya hayo mambo 11 ya asili. Kwa mfano, alisema pamoja na Bandari kuwa suala la Muungano yeye hajaona faida hata moja Zanzibar iliyoipata kwa kuwemo suala hilo kwenye Muungano na badala yake mpaka leo kila nchi inaendesha bandari kivyake. Rungu la mwisho akalipiga aliposema tusidanganyane kero za Muungano hazimaliziki maana kushaundwa Kamati na Tume chungu nzima lakini hakuna moja lililokuwa.
“Akasema hata hiyo Kamati ya Pamoja ya Serikali Mbili chini ya Makamu wa Rais wa Muungano haifanyi chochote maana hata kukutana kwake ni mashaka. Sasa huyu kabakisha nini? Kwa ujumla, nadhani ukiachilia mbali nidhamu ya woga, kaeleweka Wazanzibari wanataka nini. Na mimi nampa heko kwa kuwa na uthubutu wa kuwaondolea uvivu waliotufikisha hapa. Dk. Mwinyihaji Makame asiwe na wasiwasi. Hayo anayoyataka atayapata tu kupitia mfumo mpya wa mashirikiano kati ya Zanzibar na Tanganyika kupitia Mkataba.”

Hayo kama hayatoshi, hebu soma haya mengine:
“Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Yussuf Mohamed Yussuf, alikuwa ni mmoja kati ya watu waliojitokeza kutoa maoni mbele ya Tume ya Katiba katika kituo cha Mombasa S.O.S. jana tarehe 3 Desemba, 2012. Katika maoni yake, akasema anataka muundo wa Muungano ubaki kama ulivyo lakini akataja orodha refu ya kero za Muungano.
“Akapinga kuwepo kwa mamlaka mbili za kodi kwa upande wa Zanzibar na kutaka TRA imalizie Tanganyika na Zanzibar ibakie ZRB, akataka masuala ya Forodha kila mmoja aendeshe peke yake, akataka mafuta na gesi asilia yaondolowe kwenye Muungano na pia Zanzibar iachiwe kuendesha uchumi wake kwa namna ambavyo itaona ina maslaha kwake. Mwisho, akamalizia anataka Zanzibar iwe na mamlaka kamili.”
Aliyetuma hadithi hizo, Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa, alimalizia kwa kujiuliza: “Sasa sijui na huyu naye atatolewa makaratasi atukanwe? Au na yeye atatakiwa afukuzwe kwenye Chama?”
Mimi namalizia kwa kujiuliza, baada ya yote haya, je Rais na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Shein, amebakia na nani wa kumuunga mkono kwenye msimamo na ahadi yake ya kuitumikia sera ya Tanganyika dhidi ya matakwa ya Wazanzibari? Ana nani pamoja naye? Borafya Silima na Baraka Shamte tu? Hajioni akiwa mtupu!?

No comments:

Post a Comment