Monday, February 18, 2013

MAALIM SEIF AMTOLEA UVIVU NCHIMBI NA VYOMBO VYA HABARI NCHINI TANGANYIKA


                                                                                                                                                                                                             Makamo wa Kwanza wa Rais Nchini Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad ametoa kauli nzito kulaani kitendo cha kuuliwa kinyama Padri Muchi. Amesema kitendo hicho hakikubaliki na kinapaswa kulaaniwa na kila mwenye kuipendelea kheri nchi hii ya Zanzibar. Amesema waliofanya hivyo bila shaka ni watu wasioipendelea mema katika nchi ya Zanzibar na watu wake, wasiofurahi kuona umoja wa wazanzibari unaduma na wasiopenda amani na maendeleo kwa wazanzibari.
Maalim Seif amesema anaunga mkono agizo la Rais Kikwete la kutaka timu maalum ikishirikiana na wataalamu kutoka nje kuchunguza kwa makini tukio hilo na waliohusika kutiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua za kisheria. Hata hivyo amesisitiza kwamba katika utekelezaji wa agizo hilo la Rais vyombo vya dola viweke pembeni ushabiki wa aina yoyote ambao unaweza kupelekea kuwanyanyasa wasiohusika.
Aidha kwa mshangao na mshtuko mkubwa Maalim Seif amezihoji kauli za vyombo vya habari vya nchi ya Tanganyika (Tanzania)   na viongozi wa Jamhuri ya Muungano hususan ile ya waziri wa Mambo ya ndani,Emmanuel Nchimbi kwamba kitendo hicho ni ugaidi unaofanyika Zanzibar. Maalim Seif amehoji ni kwa nini..? kwa ushahidi gani..? na kwa azma gani..? waziri Nchimbi ametoa kauli ya kulihusisha tukio hilo na ugaidi unaofanyika Zanzibar...? Amesema wale wote wanaotoa kauli hizo hawana nia njema na Zanzibar kwa kuwa wanaijengea Zanzibar  hii taswira mbaya katika jamii ya kimataifa kwamba Zanzibar ni eneo ambalo kunafanyika vitendo vya kigaidi.
Maalim Seif amehoji kwamba matukio ya watu kuuwawa ni ya kawaida kule Tanganyika (Tanzania) Mkoani Geita na hivi karibuni kumetokea mauwaji na watu kadhaa kujeruhiwa kutokana na vurugu za kidini na haikusikika kauli ya waziri Nchimbi akiyaita mauwaji hayo na vurugu hizo kuwa ni ugaidi unaofanywa Tanzania bara badala yake kistaarabu kabisa waziri Mkuu amekwenda Geita na kujaribu kutuliza hali hiyo.. “Kwa nini kauli za ugaidi ni kwa Zanzibar tu..? alihoji Maalim Seif.
Maalim Seif amewataka viongozi wa Jamhuri ya muungano kufahamu kwamba Zanzibar ni nchi na inao viongozi wake kamili, hivyo kiongozi yoyote wa Jamhuri ya Muungano hapaswi kuja Zanzibar na kutoa kauli mbaya kama hiyo bila kwanza kukaa na kushauriana na viongozi wa nchi ya Zanzibar.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zamnzibar ameyasema hayo alipokuwa akizindua mafunzo maalum kwa madiwani wa CUF yanayofadhiliwa na FNS katika ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Chake chake Pemba leo asubuhi.

No comments:

Post a Comment