Friday, March 8, 2013

DUNI ASEMA IWEJE LEO TUKUBALI KUTAWALIWA NA MKOLONI KUTOKA TANGANYIKA.Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuwa na umoja na mshikamano na kuhakikisha wanaitetea Nchi yao mpaka iwe yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa jambo ambalo litawawezesha wananchi waliowengi kujikwamua kimaisha tofauti na ilivo hivi sasa ndani ya nchi yao ya Zanzibar.
Kauli hio imetolewa na Mjumbe wa baraza kuu Taifa la CUF Juma Duni Haji ambae pia ni Waziri wa afya na ustawi wa jamii katika serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho pamoja na wazanzibar wanaopenda maendeleo ya Nchi yao ya Zanzibar katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Magogoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Duni amesema kuwa hapo zamani Nchi ya Zanzibar ilikua na hadhi yake lakini kwa ubaya wa watu watanganyika wakiongozwa na Nyerere walifanya kila juhudu kuhakikisha kuwa wanaidhofisha Zanzibar kwa kuipora hadhi  iliokuwa nayo kwa kuingiza Zanzibar  kimabavu  ndani ya makucha ya Muungano huu uliopo hivi sasa ambao una kila aina ya vitimbi vinavoifanya Zanzibar isipige hatuwa ya kimaendeleo.
Amesema kuwa alichokifanya Nyerere wakati huo ni kumtisha Karume na kibaya zaidi  ni ile hatuwa yake ya kuweza kukiua chama kilichokuwa na nguvu hapa Zanzibar ambacho kila mzanzibar alijivunia kutokana na ushujaa waliokuwa nao viongozi wa chama hicho (ASP)’’lakini Bwana Nyerere aliweza kunyanganya  kila ambacho kilimilikiwa na chama hicho hapa Zanzibar kutokana na uhasidi aliokuwa nao zidi ya Nchi yetu’’.
Aidha Duni amefahamisha kuwa kufuatia  mchakato aliopo hivi sasa wa katiba mpya ulikuwa na lengo la kuimaliza kabisa nchi yetu ya Zanzibar ili iendelee kutawaliwa na wakoloni wa Tanganyika kwa maslahi yao binafsi lakini wanamshukuru Mwenyezimungu kwa kuwazindua Wazanzibari na kuliona hilo kwani kumewawezesha asilimia kubwa ya wazanzibar kusimama kwa pamoja na kutoa maoni yao ya kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa ikifuatiwa na Muungano wa mkataba.
Sambamba na hayo amesema kuwa hali inayoonekana hivi sasa kutokana na Muungano huu uliopo ni kama vile dudumizi ambao hutafuna ndani kwa ndani.
“Ni ukweli usiofichika  wenzetu wa Tanganyika walikuwa na lengo lao zamani sana la kuunda katiba mpya kutokana na vitabu mbali mbali walivovitunga”.
Akitolea mfano moja miongoni mwa vitabu kilichotungwa na Pr: Shivji na kuzinduliwa na Jaji Warioba ambacho kinajulikana kwa jina la (Je tutafika)ndani ya kitabu hicho kuna kipengele  kinachoonesha kuwa nchi yetu ya Zanzibar imejumuishwa kuwa ni miongoni mwaa mikoa ya nchi ya Tanganyika.
Pamoja hayo Duni amesema anashangazwa sana na baadhi ya watu wa Zanzibar licha ya kufanyiwa vitimbi mbali mbali na Tanganyika lakini wamekuwa wakingangania kuwepo kwa muungano huu dhalim wakati huko nyuma viongozi wetu kwa pamoja walifanya Mapinduzi kwa lengo la kujitawala na kuendesha mamlaka ya Nchi yao, iweje leo hii tukubali kutawaliwa tena na mkoloni  kutoka Tanganyika.
Aidha duni alimalizia kwa kuwataka Wazanzibar wote kwa pamoja wasikubali kabisa kugawiwa na watu wenye maslahi yao binafsi na badala yake waungane kwa pamoja kuhakikisha wanairudishia nchi yao ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment