Sunday, March 24, 2013

MVUA YAZUWA MAFURIKO MAKUBWA NCHINI TANGANYIKA
  Mvua kubwa iliyonyesha nchini Tanganyika jana jijini Dar es Salaam, ilisababisha mafuriko makubwa katika baadhi ya maeneo, hivyo nyumba kadhaa kujaa maji na baadhi ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.
Mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua iliyoanza kunyesha muda wa asubuhi, pia yalisababisha hasara kubwa kutokana na vitu na mali mbalimbali kuchukuliwa na maji.
Muandishi wetu alitembelea maeneo mbalimbali na kushuhudia wananchi wakihangaika kuokoa mali zao, baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kujaa maji.
Barabara kadhaa zilikuwa hazipitiki kutokana na kujaa maji, huku baadhi ya nguzo za umeme na simu ambazo zilikuwa karibu na mifereji ziliharibiwa na kusombwa na maji.
Mafundi wa Shirika la Umeme Tanganyika (Tanesco) walionekana katika maeneo kadhaa ya jiji wakihangaika kuokoa baadhi ya nguzo hizo.
Athari kubwa ya mafuriko hayo ilitokea katika eneo la Kigogo Darajani ambako baadhi ya nyumba zilikuwa zimejaa maji na baadhi ya vitu vilionekana vikielea kwenye mikondo mikubwa ya maji.
Mmoja wa waathirika hao, Andrew Simon (35) alisema nyumba yake ilijaa maji kwa takriban futi nne kwenda juu na kusababisha hasara ya mali ambayo alikuwa bado hajafahamu thamani yake.
“Sisi tulitoka kwenda kwenye shughuli zetu, baadaye tulipigiwa simu kwamba kuna mafuriko jambo lililonifanya nirudi haraka ndiyo nikakuta nyumba yetu ikiwa imefurika, huku vyombo vyote vikiwa vimeharibika,” alisema Simon.
Kuhusu kutii agizo la Serikali ya Tanganyika la kuwataka wananchi wa mabondeni kuyahama makazi yao, Simon alisema yeye ni mpangaji hakufahamu kuwa mafuriko yangetokea.
Mbali na Kigogo Darajani maeneo mengine ya Ubungo, Tabata, Magomeni Kagera, Jangwani, Msasani, Mikocheni, Kimara na Mbezi pia yaliathiriwa na mvua hizo hali iliyozua hofu miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.
Pia hali ilikuwa mbaya eneo la Tabata Relini nyumba na magari vilifunikwa na maji na kuwafanya watu kupanda kwenye mapaa ya nyumba zao.
Reli inayopita katika eneo hilo ilifunikwa na maji kiasi cha kusababisha kuwapo kwa wasiwasi kama treni ya usafiri wa abiria itafanya kazi leo.


No comments:

Post a Comment