Friday, March 29, 2013

SHEIKH RASHID NASSOR AL-BATASHI AFARIKI DUNIA


Tunapenda kuwatangazia kifo cha Sheikh wetu Rashid Nassor Al Batashi kilichotokea leo huko Hospitali ya Mnazi Mmoja na mwili wake utasaliwa katika Msikiti wa Jumuiya ya Waarabu Rahaleo baada ya sala ya Ijumaa na maziko yake yatafanyika nyumbani kwake Mlandege. Inshallah Mwenyeenzi Mungu amrahisishie safari yake na ampe kauli thabit na ampe pepo. Ameeen
Sheikh Rashid ni miongoni mwa wanazuoni maarufu hapa Zanzibar na wamefanya kazi kubwa katika kuitangaza dini ya kiislamu na kufundisha maadili ya dini hiyo, mchango wake kwa jamii ni mkubwa sana mbali na taaluma yake ya kufundisha darsa lakini alikuwa akisomesha watu katika maisha kawaida na namna ya kuishi kwa kufuata kitabu kitukufu cha Allah Quraan, na akiwausia vijana sana suala la kumcha Mwenyeenzi Mungu na kuachana na utamaduni usiokuwa wetu wa kuishi na wanawake kabla ya kufunga ndoa, Sheikh Rashid atakumbukwa kwa mengi lakini suala hilo alikuwa akilikemea kwa nguvu sana Allah atampa ujira wake inshaallah.Sheikh Rashid alikuwa akiudhika sana wanaume na wanawake kuishi pamoja kinyumba au kutenda maovu kabla ya kuoana zinaa, Sheikh Rashid katika uhai wake tunafahamu alikuwa akifungisha ndoa lakini ni mtu pekee akionesha msimamao wake hadharani bila ya kujali kwamba anaowafungisha ndoa ni watu wa karibu yake au jamaa zake au ni watu wenye familia kubwa kubwa na iwapo watakuwa anaotaka kuwafungisha ndoa wametembea kimwili kabla ya kufunga ndoa alikuwa akikakabili kwanza na kuwauliza na iwapo wamefanya hivyo alikuwa akikataa kuifunga ndoa hiyo na mara kadhaa ameshawahi kwenda kuzivunja ndoa hizo akisema hataki kuchukua jukumu mbele ya Allah.
Sheikh Rashid alikuwa kiishi maisha ya kawaida sana na kama mnavyomuona hapo kwake yeye mkubwa mdoo ni sawa na akiwa heshima sana akipenda sana kusimama na kuwasalimia watu na hawezi kuwasalimia tu bali hukupa maneno mawili matatu ya hekima na kuwaombea dua kabla ya kuondoka. Basi kwa wema na matendo hayo ambayo mengi ameyafanya na kuyatenda wakati wa uhai wake basi hatuna budi kwa pamoja kumuombea dua kwa Mola wetu Mlezi Mwenyeenzi Mungu amlaze mahali pema na amjaalie kaburi lake liwe miongoni mwa mabustani ya Peponi Yarabbiy. (AMEEN)

No comments:

Post a Comment