Friday, April 12, 2013

ABDULRAHMAN MOHAMMED BABU NDIYE ALIYE MJULISHA NYERERE CHINA NA UKOMONISTI


Nchina na Zanzibar kuna ukweli mwingine wenye nguvu zaidi usiojulikana kwa wengi kwamba, bila Zanzibar na wanaharakati wake wa kimapinduzi, Tanganyika wala Nyerere wasingeijua China na Mao, achilia mbali hata ule uwezekano tu wa Tanganyika na Zanzibar kuungana mwaka 1964.
Itoshe tu kusema kwa utangulizi kwamba, tangu harakati za uhuru wa Tanganyika na kabla na baada kidogo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Nyerere alikuwa mpinzani mkubwa wa sera za nchi za Mashariki, ikiwamo China. Alilazimika kuikumbatia China baada ya kuzidiwa kete na wanaharakati wa Zanzibar.
Mwanzo wa harakati na uhusiano
Harakati za kudai uhuru Zanzibar zenye kueleweka zilianza na Zanzibar Nationalist Party (ZNP), kilichoundwa Desemba 1955 kama mrithi wa Chama cha awali cha Hizbul Watan Raiatul Sultan (National Party of the Sultan’s Subjects – NPSS), yaani, “Chama cha Kitaifa cha raia wa Sultan” – Hizbul.
Tofauti na maoni ya baadhi ya watu, kwamba ZNP ndiyo HIZBUL, ZNP hakikuwa zao la HIZBUL wala sera zake, bali kilikuwa Chama cha Kitaifa kwa raia wa matabaka yote na kwa kuhakikisha nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Chama hicho zilishikwa na Waafrika sio warabu kama inavyo zushiwa kama historia za uwongo na kuwapoteza watu katika historia ya kweli ya nchi ya Zanzibar.
Kwa kuwa kilikuwa ndicho Chama pekee cha kiharakati wakati huo kabla ya Afro-Shirazi (ASP), kilichoundwa Februari 1957 kwa kuunganisha African Association na Shirazi Association, kiliweza kukua na kupata nguvu haraka na kuvuta hisia za wengi kwa wito wake mashuhuri wa “Uhuru sasa hivi”.
Katika kipindi hicho, akatokea na kujiunga na ZNP, kijana Mzanzibari machachari kwa jina Abdulrahman Mohamed Babu mwaka 1957, baada ya kurejea kutoka London, alikokaa kwa miaka mitano na akawa pia ndiye Katibu Mkuu wa Chama hicho na Kiongozi wa Vijana. Babu alifunzwa harakati na mbinu za mapinduzi na Wachina.
Miaka minne baadaye, na baada ya kupima uzito wa harakati za uhuru Visiwani, Babu aliwapeleka baadhi ya vijana wake wa Kizanzibari mafunzo ya kijeshi nchini Cuba kwa maandalizi ya baadaye kwa “lolote linaloweza kutokea”. Alikuwa na uhusiano wa karibu na China, na aliweza kuanzisha gazeti la kipropaganda lililoitwa “ZANEWS” kwa msaada wa Shirika la Habari la China – “Hsinhua” mwaka 1960, kama sehemu ya juhudi za kueneza itikadi za Kikomunisti ili kuamsha hisia za kimapambano Zanzibar, na alifungua ofisi ya kudumisha uhusiano na China Visiwani humo.
Mwaka 1962 alikamatwa na kushitakiwa kwa kuandika makala ya uchochezi kwenye gazeti hilo na akahukumiwa kifungo cha miezi 15, hivyo kazi ya uhariri wa gazeti ikachukuliwa na mwanaharakati mwingine, (Dk.) Salim Ahmed Salim.
Mwaka 1963, Babu alifarakana na wenzake ndani ya ZNP baada ya kudai Chama hicho hakikujielekeza vya kutosha kuelekea kwenye “Ujamaa wa Kisayansi”. Kwa hiyo, yeye na kundi lake la vijana walijiengua na kuunda Umma Party (UP) na Salim Ahmed Salim akaendelea kuwa Mhariri wa gazeti jingine la kiharakati la Chama hicho kipya.
Harakati za Babu ndani ya Zanzibar na uhusiano wake na nchi za Kisoshalisti hususani, China, ulizidi kumfanya aonekane mtu hatari na mwiba kwa utawala wa Zanzibar kiasi cha kuwindwa ili adhibitiwe, na ikiwezekana aangamizwe. Aliishi maisha ya wasiwasi huku akiendeleza harakati kwa kuunganisha pia nguvu za baadhi ya vijana wa ASP wenye fikra za mrengo wa kushoto (Wakomunisti), akiwamo Abdallah Kassim Hanga na wenzake.
Wakati wa mazungumzo ya Kikatiba kuelekea uhuru ya Lancaster House, Uengereza; kati ya ofisi ya makoloni ya Uengereza na vyama vya ZNP, Zanzibar and Pemba People’s Party [ZPPP] na ASP, Babu na Chama chake aliachwa, na alikuwa amenyang’anywa Pasi yake ya kusafiria; lakini kwa kutumia mbinu thabiti, akapata Pasi ya dharura ya Tanganyika kisha wakamsitukia kwenye mazungumzo hayo, wakaduwaa. Baada ya Lancaster House akaenda Peking, China kwa “mashauriano” kadhaa na kurejea siku chache kabla ya uhuru wa Zanzibar, Desemba 10, 1963.
Ni Babu na vijana wake, ambao ndiyo tu walikuwa wamerejea kutoka mafunzoni Cuba, kwa kushirikiana na vijana wa ASP wenye sera za mrengo wa Kikomunisti, waliopanga na kufanikisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964 bila kuwafahamisha wala kuwashirikisha viongozi wakuu wa ASP kwa hofu kwamba wangeyazuia maana viongozi wa ASP wengi wao walikuwa waoga sana. Kutokana na Mapinduzi hayo, Babu aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje katika serikali ya umoja wa kitaifa (mseto), wanaharakati wenzake wa Umma Party, kama kina Khamis Abdallah Ameir, Ali Sultan, Salim Rashid, Badawi Qullatein na wengineo, nao walipewa nyadhifa kubwa. Kwa kutumia nafasi yake ya uwaziri, Babu aliimarisha zaidi uhusiano wa Zanzibar na China.
China ilivyojidhihirisha Visiwani
Ushawishi wa China Visiwani na sera zake za Kikomunisti kupitia kwa Babu ulikuwa dhahiri kabla na baada ya Mapinduzi. Baada ya Mapinduzi, majina ya kikoloni yalibadilishwa na badala yake yakawekwa majina ya Kikomunisti. Kwa mfano, Uwanja wa Mpira wa Taifa uliitwa Mao Tse Tung; shule moja mashuhuri ikaitwa Fidel Castro; Hospital ya Taifa ikapewa jina la V. I. Lenin na madaktari wa Kichina wakaletwa Zanzibar kwa wingi kufanya kazi humo.
Wakati nchi za Magharibi zilichukua miezi sita kuitambua Serikali ya Mapinduzi kwa madai kwamba “Wakomunisti wamechukua madaraka Visiwani vya Zanzibar”, China, Urusi, Ujerumani Mashariki, Czechoslovakia na Cuba ziliitambua sawia na kuanza kumwaga misaada mikubwa kwa wingi.
Mwanzoni tu na kwa haraka, Serikali mpya ilikaribisha na kupokea wataalamu na misaada mbalimbali kutoka China. Nayo Urusi ilileta meli iliyojaa magari, mizinga na bunduki kubwa za kutungua ndege na vifaru pamoja na silaha nyingine ndogo. Mwishoni mwa Februari, 1964, Babu akaitangazia dunia kuwa Zanzibar ilikubali kupokea msaada wa shilingi 3,700,000 kutoka China na akajigamba kwa kusema, “Huo ni mwanzo tu”.
Naye Rais wa Zanzibar wa wakati huo, hayati Abeid Amani Karume, akimpokea Balozi kutoka China, Meng Ying, aliishukuru nchi hiyo kwa misaada, akisema: “Zanzibar inaitegemea China, siyo kama rafiki, bali kama ndugu kabisa”.
Kwa Marekani, Uingereza na Ujerumani Magharibi walipingwa na butwa na macho kuwatoka kama mjusi kabanwa na mlango,na nchi hizo kwa wakati huwo Tanganyika ilikuwa tegemezi kwake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa uhusiano hatari na Wakomunisti. Tayari jumuiya ya kimataifa ilikuwa imeibatiza kama “Cuba ya Afrika”kwa chuki na hasira zao. Kwa sababu hii, Waziri wa Nchi wa Marekani (Usalama), Dean Rusk, aliwaagiza Mabalozi wa Marekani nchini Kenya na Uganda, wawashawishi Nyerere, Kenyatta na Obote wamweleze Karume “hatari kwa yeye (Karume) kumtegemea Babu, na jinsi Babu alivyokuwa hatari kwa usalama wa Zanzibar na Afrika Mashariki kwa ujumla kuigeuza kuwa afrika mashariki komunusti”.
Rusk akaendelea kupendekeza akisema: “Je, inawezekana kumshawishi Nyerere, licha ya yeye kukataa hapo mwanzo, (sasa) akubali wazo la kuunda Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar, kama njia ya kumuimarisha Karume na kupunguza ushawishi wa Babu. Hatua kama hiyo inaweza pia kumsaidia Nyerere wakati huu (juu ya hofu ya kupakana na Ukomunisti) kwa nafasi yake”.
Wakati Rusk akipendekeza hivyo, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) tayari lilikuwa limeanza kuandaa mazingira ya Shirikisho la Tanganyika/Zanzibar tarajiwa, na kwa kuchochea uhasama miongoni mwa wanamapinduzi wa Zanzibar kama wanavyo chochewa sasa Wazanzibari na kuanza kuchukiana; na pia kutia hofu miongoni mwa viongozi wa Afrika Mashariki juu ya Zanzibar kugeuka ya Kikomunisti.
Nyerere na Waziri wake wa Ulinzi na Mambo ya Nje, Oscar Kambona kwa upande wao walikerwa, kama zilivyokerwa nchi za Magharibi, juu ya uwezekano wa nchi dogo kama ya Zanzibar kuwa Wakomunisti na kuwa kwenye kingo za nchi ya Tanganyika,Kenya na Uganda abazo zote zilikuwa ni vibaraka wa nchi za Magharibi na athari zake, kwamba nchi za Magharibi zingepoteza imani kwa Nyerere na Tanganyika.
Nyerere akubali ya Marekani
Mbinu za Marekani za kuwafarakanisha Wanamapinduzi Zanzibar zilianza kuzaa matunda. Kulizuka mgogoro ndani ya Serikali ya Zanzibar kwa Wanaharakati wa Umma Party na baadhi ya wale wa ASP wenye siasa za Kikomunisti kudai kuwa Karume alishindwa kuongoza na kusimamia Mapinduzi, hivyo ajiuzulu vinginevyo wangempindua. Mashuhuri kati yao hao walikuwa ni Khamis Abdallah Ameir, Ali Sultan, Babu, Ali Mahfoudh (Kanali), Salim Rashid, na Badawi Qullatein kwa upande wa Umma Party; na wenzao wa ASP, kina Abdullah Kassim Hanga, Abdulaziz Ali Twala, Othman Sharrif, Hassan Nassoro Moyo na wengineo.
Jinsi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyofikiwa kwa kasi isiyo ya kawaida, ni dhahiri ilikuwa ni kwa Nyerere kukidhi matakwa ya nchi za Magharibi, na kwa Karume kujiponya na wahasimu wake waliotishia kumpindua. Kutokana na Muungano huo, wahasimu hao ama walihamishwa na kupewa nafasi za uongozi katika Serikali ya Muungano kumfanya Karume apumue, au walibakia Zanzibar bila nyadhifa, lakini chini ya jicho kali la serikali na wengine kuuawa kikatili na mpaka leo wengi wao walio uliwa hawajulikani makaburi yao yalipo.mfano mdogo Ali Mahfoudh ((kanali)) alipelekwa Mozambiq na mpaka kufia huko bila kurudi kwao Zanzibar na wengine ndio kama tulivyo eleza hapo juu kuwa wameuliwa kikatili na makaburi yao mpaka leo hayajulikani yalipo.
Nyerere azisaliti nchi za Magharibi
Kutokana na Muungano, Nyerere alibanwa na Mataifa ya Magharibi apunguze nguvu za Wachina na Wajerumani Mashariki Visiwani, lakini akakataa kwa sababu kubwa mbili: Mosi, hakutaka kuingiliwa kwa mambo yake ya ndani; pili hakuwa na uwezo wa kuingilia mambo ya Zanzibar kwa wakati huwo maana wakati huwo Wazanzibari wengi ni wasomi na mashuja sio waoga kama hawa viongozi walio sasa wa Zanzibar pia hakuweza kuingilia mambo yasiyo ya Muungano. Kana kwamba alikuwa anayakomoa mataifa hayo, Agosti 1964, alipokea Wachina saba na Wakalimani wao wanne, kuja kufundisha Jeshi la Tanzania kwa miezi sita maana hapo ndio muungano huwo feki una anza.
Na alipobanwa tena na mataifa hayo aeleze kama alitambua hatari ya kuwakubali Wachina, Nyerere aling’uka akasema: “Hatari iliyo kubwa kuliko zote ninayoiona ni kwamba Jeshi (langu) litaasi kama lilivyoasi mwezi Januari (1964). Halikuwa limefunzwa na Wachina!”.
Akitetea uwepo wa Wachina Zanzibar alisema: “Je, tunataka Wazanzibari wakae tu kama wapumbavu, wasifanye lolote..?? Walikubali msaada wa kijeshi kutoka China na Urusi; hawakuwa na jingine la kufanya”, kisha akaongeza kusema:
“Kwangu msaada wa Wachina ndiyo ulio karibu zaidi na maombi yangu. Tatizo kwa Wachina ni lipi..?? Mimi silioni!”
Mwezi Februari, 1965, Mwalimu alifanya ziara nchini China, akashangazwa na jinsi matatizo ya China yalivyofanana na ya nchi yetu, na namna China ilivyodhamiria kuyatatua. Nchi hiyo ilikuwa imeamua kuwa ya Kisoshalisti kwa kuruka hatua ya ubepari kwa kutangaza “Mruko mkuu kwenda mbele” – (The Great Leap Forward) tangu mwaka 1948.
Naye Nyerere miaka miwili baadaye, Februari 5, 1967, aliiga kwa kutangaza “Azimio la Arusha” kama dira ya Maendeleo na ujenzi wa “Ujamaa” – (Usoshalisti) kwa kuruka hatua ya ubepari ili kuufikia “Ujamaa”.
Nyerere, kwa kufurahishwa na sera za uchumi wa China wakati wa ziara yake, alitamka mapema kwenye dhifa ya kitaifa huko Peking: “Ingawaje lengo letu sote ni lile lile, (lakini) tunatekeleza malengo hayo kwa mapito ya njia tofauti kwa kuelewa kwamba tutakutana kituo kimoja kile kile cha madhumuni na matarajio ya safari yetu”.
Leo, miaka 48 tangu ziara hiyo ya kihistoria ya Mwalimu nchini China, Watanganyika wala Wazanzibari hatujakitia machoni “kituo cha matarajio”, wakati wenzetu (Wachina) walishafika, wakila mavuno na kusaza na kututupia wanachosaza ili tugange njaa kama watu waliolaaniwa. Kwa nini..??
Ni kwa sababu Wachina waliazimia kuendesha Usoshalisti wa Kisayansi (Scientific Socialism), tofauti nasi tulioazimia kuendesha Usoshalisti (Ujamaa) wa kiujima kwa lelemama na kubakia “Wajima” kijamii na kiuchumi hadi tumevamiwa tena na ubepari, ubeberu na ukoloni tulioupiga teke miaka ya 1960.
Ni kwa sababu hii Babu na Nyerere walikuwa hawaishi kugongana huku Babu akimtuhumu Nyerere  kwa kuipeleka nchi kwenye Usoshalisti pole pole, kwa woga na bila misingi ya kisayansi.
Ukweli, Babu ndiye aliyemtambulisha Nyerere kwa Wachina, na alikuwa bingwa wa Usoshalisti kuliko Nyerere kiasi cha kuwavutia Wachina kuelekeza fikra zao kwenye “Cuba ya Afrika  Mashariki”Zanzibar na hatimaye Tanganyika.lakini Nyerere hakutaka kujulikana ndio maana alipeleka Tanganyika chini chini Nchini China kisiri ili asiwauthi wakoloni wa Ubepari na Ubeberu.hii ni kuonyesha wazi kuwa Nyerere hakutaka jambo lolote linalo leta manufa kwa Wazanzibari lifanikiwe ndio maana akaweka vikwazo na kuzunguka mlango wa nyuma na kuipeleka Tanganyika leo hii tunaona Omani ya Mtanganyika na China nayo ya Mtanagnyika.Wazanzibari tumebaki na siasa za chuki wewe Muarabu wewe Mpemba wewe Mzaramo wewe Mnyamwezi wewe Mgazija n.k.
Huenda, kama mwanaharakati huyu angesikilizwa, pengine nchi yetu ingekuwa imeikaribia China kiuchumi na hata Korea Kaskazini ambayo tulianza nayo safari ya kuelekea kwenye “Ujamaa” mwaka mmoja. Je, tuseme sasa China inarejea hima kutukomboa kwenye mazingira ya vita baridi mpya..?? je Wazanzibari tutaugana na kuijenga nchi yetu bila kusikiliza chuki zinazo pandwa na Watanganyika na nchi za Magharibi..?? au tutabaguwana wewe Mpemba na wewe Muarabu na wewe Maakonde na Mnyamwezi na kugojeya tena miaka mengine 50 ipite ndio tufikiria la kufanya..??  Tutafakari.

1 comment: