Sunday, July 7, 2013

CCM KISIWA CHA PEMBA MTAKIONA HIVI HIVI HAMSHINDI KURA HAPA HATA MUIGEUZE PEMBA KUWA QATAR YA PILI



UKWELI husababisha matatizo, hasa mtu anapoukataa na kujifanya hauoni. Siku zote ni vizuri kuukubali ukweli hata ikiwa ladha yake ni chungu kama shubiri.Ukiukataa ukweli uongo hutokea siku ukakwambia “Mimi si mwenzako.” Juhudi za kuukataa hugonga ukuta na kumtonesha kidonda  anayeukataa   au kuanzisha jeraha jengine.
Hapana ubishi kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimegonga ukuta Pemba. Kwa mara nyengine imedhihirika wazi katika uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge jimbo la Chambani Mkoa wa Kusini Pemba kuwa Pemba ni ngome imara ya Chama cha Wananchi (CUF).
Uchaguzi huo ulifanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake, Salum Hemed Khamis, kufariki dunia Machi 28, mwaka huu.
Lakini tunasikia kauli za viongozi wa CCM kuwa ati hali inabadilika Pemba kutokana na kujipanga upya kwa kile wenyewe wanachokiita “utaratibu waliojiwekea au kujivuwa gamba nacheka kwanza hahahahahahaha.”
Wapo wanaoujiuliza hivi ni nini hasa sababu ya Pemba kuipa mgongo CCM..???
Sababu ni nyingi, lakini hasa ni za kuwauwa kila wakati wa changuzi,majeshi na polisi wakitwana Tanganyika kuwanajisi watoto wao na serekali haisemi kitu,kuwathulumu ardhi yao, uchumi, dharau, matusi, jeuri, kibri na vitendo vya kuwabagua watu wa Pemba ambao ndio wazalishaji wa zaidi ya asilimia 85 ya zao kuu la kiuchumi la karafuu linalochangia hadi asilimia 30 ya mapato ya fedha za kigeni kwa Zanzibar. Hapo zamani karafuu ilichangia asilimia 90 ya mapato.
Tokea kufanyika Mapinduzi ya 1964, watu wa Pemba wamekuwa wakikosa kutendewa haki na Serikali iliyoongozwa kwanza na Afro-Shirazi Party (ASP) na baadaye CCM. Hata Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wanaiona haijafanya marekebisho ya maana ya staili yake ya utendaji kiasi cha kuwapa imani watu kuwa wameanza kuthaminiwa na serikali yao. Huu ndio ukweli, tuutake au tuukatae.
Miongoni mwa mambo ambayo watu wa Pemba wanataka ni biashara ya karafuu kuwa huru kama ilivyo kwa mazao mengine nchini kama vile mpunga, ndizi, nazi, kahawa, chai na pamba.
Wakulima wamelazimishwa tokea baada ya Mapinduzi kuuza karafuu kupitia Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) ambalo wanaliona haliwalipi wanavyostahiki.
Kwa sasa wanalipwa karibu asilimia 80 ya bei ya soko la dunia, lakini katika mwaka 1965 walikuwa wanapewa asilimia 2.25 tu (narudia asilimia mbili nukta mbili tano) ya bei ya soko. Hapana shaka haikuwa haki.
Katika mwaka 1975 wakulima walilazimishwa kuuza karafuu ZSTC kwa shilingi 2 kwa kilo. Hii ilikuwa ni asilimia 4.09 ya bei ya soko la dunia iliyokuwa ya wastani wa dola 6,873 (wakati ule dola moja ikiwa sawa na shilingi 7.105). Hii ni kusema wakati ZSTC ilinunua kilo moja kwa shilingi 2 ilikuwa inaiuza kwa shilingi 48. Faida kubwa iliyoje!!!!!!!
Baada ya kipindi cha karibu robo karne, mkulima wa karafuu alipunguziwa maonevu mwaka 1986 pale kilo moja iliponunuliwa na ZSTC kwa shilingi 900, ikiwa ni sawa na asilimia 60.33 ya bei ya soko la dunia. Baada ya hapo, alilipwa chini ya asilimia 45 ya bei ya soko la dunia.
Serikali iliweka adhabu ya kifo kwa mtu anayekamatwa akisafirisha karafuu kwa magendo, lakini adhabu hiyo nzito haikuwazuwia watu kujitosa baharini usiku wa kiza wakisafirisha karafuu kwenda Tanga na Mombasa.
Waliokamatwa nchi kavu na baharini kwa madai ya kusafirisha karafuu kwa magendo walisukumwa jela kwa miaka mingi na hakuna aliyehukumiwa kifo.
Kabla ya Mapinduzi, wafanyabiashara walishindana kununua karafuu na mkulima alikuwa huru kuuza karafuu zake kwa kiwango alichotaka na muda aliotaka. Wengine walizihifadhi kama akiba ya kumsaidia wakati wa shida, lakini hali ikabadilika baada ya kuifanya ZSTC mnunuzi pekee wa zao hili na kuuza nje. Wakulima wameilalamikia sana hatua hiyo, hasa kwa vile bei ya ZSTC ilikuwa ya unyonyaji.
Kwa muda mrefu tokea wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya nne, Dk. Salmin Amour Juma na mpaka hivi karibuni, serikali imetoa ahadi ya kuifanya biashara ya karafuu huru, lakini kila siku zinasikika kauli za viongozi wakuu wa serikali kwamba mipango ya kufanya hivyo “ipo mbioni.”
Serikali sasa inamlipa mkulima wastani wa asilimia 80 ya bei ya soko la dunia na kwa kiasi fulani hatua hii imefurahiwa kiasi cha kupunguza wimbi la kuisafirisha karafuu kwa magendo kwenda nchi jirani.
Hata hivyo, ipo haja kwa serikali kuliangalia upya suala hili na kuifanya biashara hii kuwa kweli huru. Wananchi wauze watakako.

Jengine linalowafanya watu wa Pemba kutoipenda CCM ni mambo waliyotendewa katika miaka ya kwanza baada ya Mapinduzi. Binafsi, nimeshuhudia watu wakitandikwa bakora barabarani mchana kweupe nilipotembelea Pemba miaka ya nyuma na palikuwa hapana pa kulalamika na hadi leo serikali haijakiri kufanyika uovu huo na kuwaomba radhi wananchi kwa mateso yale.
Mfumo wa vyama vingi uliporuhusiwa tena mwaka 1992, hali ilikuwa mbaya kwa wapinzani na zaidi kisiwani Pemba ambako watu kunajulikana kulivyo na watu wenye msimamo imara kisiasa na kidini. Watu waliuliwa na Pemba ikaweka historia ya kupata mauaji ya kwanza ya raia kwa mkono wa dola baada tu ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa.
Mwananchi wa kwanza huyo alikuwa ni mkazi wa Shumba Mjini ambaye alipigwa risasi na askari polisi kwa sababu tu alikuwa amepandisha bendera ya CUF mara baada ya kusajiliwa rasmi.
Taarifa ya Polisi ilisema kwamba tukio hilo lilikuwa la bahati mbaya kwani risasi ilipigwa juu na kumpata mwananchi huyo iliporudi chini.
Mwenendo wa kupiga watu na kuwavumbulia kesi bandia za kutia kinyesi mashuleni na visimani ulifurutu ada. Hii ilisababisha watu wengi kukimbia Pemba na kuhamia mikoa ya jirani nchini Tanganyika kama Tanga, Pwani,Dar na kadhaa kuhamia kisiwa kikubwa Unguja.
Balaa lilizidi ulipokuja uchaguzi. Maelfu ya Wapemba walinyimwa haki ya kupiga kura na zaidi ya watoto wao 200 waliokuwa wanasoma Unguja katika shule za sekondari zilizokuwa na dakhalia walifukuzwa kwa sababu walitaka haki yao ya kupiga kura.
Baada ya hapo mamia ya Wapemba, wakiwemo walimu na watumishi katika taasisi za serikali na vikosi vya ulinzi walifukuzwa kazi na wengi kufunguliwa kesi za kumkashifu na kumtukana Rais.
Ajira serikalini kwa watu wenye mtizamo wa upinzani, hasa Wapemba, zilikuwa ngumu na Dk. Salmin ambaye alipachikwa jina la Komandoo kwa uongozi wake wa mabavu dhidi ya wapinzani, alisema kwa kuwa Wapemba walimnyima kura hakuona sababu ya kuwaweka katika utumishi wa serikali.
Yapo madai hata wakati wa kuajiri wafanyakazi katika vikosi walichukuliwa vijana kutoka Unguja kwenda Pemba kuajiriwa ili ionekane ajira pia ilifanyika kisiwani Pemba.
Kila Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inapoangalia upya majimbo ya uchaguzi na kuamua kuyarekebisha, majimbo ya Pemba hupunguzwa. Yalikuwepo majimbo 25 katika uchaguzi wa 1995, yakapunguzwa hadi 24 na sasa ni 21. Sababu inayotolewa ni idadi ya wapiga kura Pemba kuwa ndogo, lakini ukweli ni kuwa watu wengi Pemba hawapati haki ya kupiga kura na kwa sababu ya maisha magumu yasiyotoa matumaini ya kubadilika, watu wanaondoka na kuhamia kisiwa kikubwa Unguja na kwengineko kama nchini Kenya,Uganda,Burundi,Rwanda,Somalia,canada,U.S.A,England,Belarus,U.A.E,Oman,South Africa,Skan Navia,India,South Korea,China,Russia,Cuba,Comoro, n.k.
Hivi sasa Wapemba wengi wanahangaika kupata kitambulisho cha Mzanzibari I.D. na kinachosikika ni ahadi za kuwapatia haki hiyo, lakini upatikanaji wa kitambulisho hicho ungali unakumbwa na urasimu mkubwa huku wananchi hao wakibaguliwa kisiasa.
Pamekuwepo matusi ya nguoni yaliyoelekezwa kwa Wapemba na wanaofanya hivyo, ikiwa ni pamoja na kuandika katika mabao ya maskani za CCM, hawaguswi kama vile kitendo hicho kinakubalika. Matusi pia huenezwa kupitia vipeperushi ambavyo hata vinaposhikwa na Polisi, huahidi tu watachunguza lakini ripoti za uchunguzi hazitolewi.
Hata baadhi ya viongozi hawaoni vibaya kuwadhalilisha Wapemba. Kwa mfano, kiongozi mmoja aliyekwenda Pemba kumfanyia kampeni mgombea wa CCM katika uchaguzi wa Chambani hapendezi Pemba kwa vile aliwafananisha Wapemba na “vijibwa vya santuri” (sauti ya bwana wao).

Huu ndio ukweli uliosababisha CCM kuambulia chini ya asilimia 12 ya kura za Rais na chini ya asilimia 10 ya kura katika majimbo mengi ya uchaguzi. Katika jimbo la Chambani, CCM siku zote imekuwa ikipata chini ya asilimia 10, lakini safari hii imefikisha asilimia 12.
Wakati umefika kwa serikali kuchukua hatua kuwapunguzia unyonge Wapemba ili waone wanatendewa haki na serikali na wanathaminiwa katika nchi yao. Mtindo wa kupeleka wapiga kura mamluki kwa visingizio vya kufungua kambi za vijana Pemba ukomeshwe.
Ni vizuri kukubali makosa yamefanyika na si vibaya pakatolewa fidia kwa waliofanyiwa maovu wakiwepo waliouliwa ndugu na jamaa zao. Kutenda kosa ni kosa na kurejea kosa ni dhambi kubwa.

No comments:

Post a Comment