Wednesday, July 17, 2013

HIVI KWELI WAZANZIBARI MAAFTARI YANAWASHUKA WAKATI MASHEIKH WAKO JELA MASHEIKH WANAFUTURU NINI..?


Kuna kimya kikubwa kinachonishangaza. Nacho ni cha ‘wanaharakati’ wa Kizanzibari walioziba midomo yao kuhusu madhila yanayowakuta wale waliokuwa wakiwaita “mashekhe wetu wa Uamsho”.
Tangu mashekhe hao 10 waanze kukamatwa Oktoba 16, 2012 mpaka leo kesi yao haijatajwa mahakamani. Hadi sasa wamesomewa tu mashtaka dhidi yao, mashtaka ambayo yanahusika na vurugu zilizotokea Zanzibar Mei mwaka jana.
Washtakiwa hao walifikishwa mara ya mwisho mahakamani Julai 3 mwaka huu na wanatarajiwa kupandishwa tena mahakamani Julai 18.
Washtakiwa wenyewe ni Farid Hadi Ahmed, Msellem Ali Msellem, Mussa Juma Issa, Azan Khalid Hamdani, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Ghalib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.
Mashtaka yanayowakabili ya kusingiziwa ni kuchochea vurugu, kuharibu mali za umma na za watu binafsi zenye thamani ya shilingi milioni 500, kufanya vurugu katika eneo la Magogoni na kuhatarisha usalama wa taifa la Zanzibar.
Wanashtakiwa pia kuhusu kadhia ya Farid Hadi Ahmed aliyetoweka Oktoba 16, 2012.
Shekhe Farid alitekwa na aliibuka siku nne baadaye na kusema alitekwa nyara na watu waliovaa barkoa waliojitambulisha kuwa ni polisi. Serikali imelikanusha dai hilo.
Mashekhe uamsho wamefungiwa kwenye gereza la Kiinua Miguu wakiwa chini ya ulinzi mkali. Kama wiki mbili za mwanzo baada ya kutiwa nguvuni wakidhalilishwa kwa kunyimwa hata nafasi ya kubadili nguo au ya kuonana na familia zao.
Tena kila mtuhumiwa alikuwa akiwekwa katika chumba cha peke yake. Tunavyosikia ni kwamba siku hizi wameondoshewa madhila hayo ingawa bado mazingira yao si ya kuridhisha.
Cha kushangaza ni kwamba hatusikii sauti zozote zenye kuwatetea masheikh hawa. Labda kwa sababu wao ni mashekhe na si wanasiasa..?? Labda wangekuwa wanasiasa tungewaona wanaharakati, kwa mfano, wakiwasiliana na jumuiya za kimataifa za haki za binadamu na kuzizindua kuhusu janga lililowafika mashekhe hao.
Labda devu zao mashekhe zimewatia hofu wanaharakati, wanachelea wasije wakashtumiwa kuwa wanawatetea ‘magaidi’..?? maana siku hizi kwa wakubwa wa dunia hizi devu, Uislamu na utetezi wa haki ni mchanganyiko wa hatari.
Na si kwa hao wakubwa tu bali hata kwa baadhi ya taasisi, magazeti, na wanasiasa wa Tanganyika ambao bila ya ushahidi wowote wameihusisha Uamsho na vitendo vya kigaidi.
Juu ya yote hayo, kuna sababu halali za kuwatetea. Sababu kubwa ni kazi walioifanya ya masheikh hawa ‘kuwaamsha’ Wazanzibari wenzao wautambue utaifa wao na waachane na chuki, uhasama na ubaguzi uliokuwepo baina yao kwa muda mrefu.
Jengine jema walilolifanya ni kuwahimiza vijana wa Kizanzibari warudi kwenye maadili ya Kiislamu badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoleta madhara katika jamii kama vile vya kubugia mihadarati na uasherati.
Pengine kuna wanaharakati wenye kujuta, wenye kuona kwamba walipoteza nguvu zao walipokuwa wakiwaunga mkono hao mashekhe. Wale waliokuwa na majazba waliokuwa wakiota kwamba siku moja nchi yao itaamka ghafla ionekane na sura nyingine sasa itawabidi waote ndoto nyingine.
Sina dhamira ya kuingilia kesi inayowakabili washtakiwa hao. Hiyo ni kazi ya wazanzibar wenye na mahakama zao za njaa na ya mawakili wa masheikh.
Dhamiri yangu ni kukizungumzia hiki kimya kilichotanda kama wingu juu ya kesi hii.Na zaidi nataka kugusia haki wanayonyimwa washtakiwa ya kuachiwa kwa dhamana huku kesi ikiwa inaendelea. Kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi hiyo ni adha kubwa kwa washtakiwa.
Inavyoonyesha ni kama serikali ya wahafidhina na sultani wao mkoloni mweusi Tanganyika imeamua kuwatia adabu ingawa hawakupatikana na hatia.
Ikiwa dhana hiyo ni sahihi basi serikali ya wahafidhina itakuwa imeamua hivyo kwa sababu za kisiasa na kumfurahisha sultani wao mkoloni mweusi Tanganyika. Serikali inazidi kujifaragua ikiamini kwamba kuwatia adabu viongozi wenye muelekeo wa Kiislamu hakutowakera wakubwa wa dunia hii.
Labda serikali inaamini kwamba balozi za Marekani na Uingereza zitayafumbia macho wanayotendewa mashekhe hao kwa sababu zimekwishatiwa sumu ya Uamsho kusingiziwa ugaidi.
Ndio maana kesi hiyo ikawa inaakhirishwa na kuakhirishwa tena na tena kwa lengo la kuwaweka ndani tu mashekhe hao. Mara ya mwisho Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar alisema wanasubiri waletewe daftari la kesi kutoka Mahakama ya Rufaa,ya sultani mkoloni mweusi Tanganyika jijini Dar es Salaam.
Sijui Wazanzibari wenzangu wanapofuturu na aila zao katika mwezi huu mtukufu kama wanawafikiria wananchi wenzao walio gerezani au niulize swali wakati tunafuturu ftari zetu zinashuka kweli na hali tunajuwa wakombozi wa nchi hii wako jela je zinashuka...??
Nijualo ni kwamba ingawa uamuzi ni wa mahakama wengi wenye kuifuatilia kesi hii wanaamini washtakiwa hao wanaendelea kuwekwa ndani kwa sababu hivyo ndivyo watakavyo viongozi wa juu wa serikali ya wahafidhina ya Zanzibar.
Mara mbili tatu hivi Ali Mohamed Shein mwenyewe amesema hadharani kuwa atawashughulikia ati wanaochochea fujo.Wakati mwingine huwataja Uamsho.
Zanzibar ya leo ni nchi yenye kuhuzunisha; haisikitishi tu bali inahuzunisha. Ni nchi yenye kutatanisha, wakati mwingine hujikanganya yenyewe.Na viongozi wake. Naona hata haina haja ya kuwaeleza walivyo; bora tulifunike kombe…

No comments:

Post a Comment