Thursday, September 26, 2013

KAMISHNA MUSSA ALI MUSSA WACHA KUJIFICHA NJOO UELEZE UKWELI AU DOMO LAKO LIMEKUPONZA..???


JESHI la Polisi nchini Zanzibar limekaa kimya na halitoi maelezo yoyote ya kinachendelea katika uchunguzi wa madai yake kuwa huenda watu wenye uhusiano na kikundi cha Al Shabaab cha Somalia wanahusika katika mashambulizi ya tindikali nchini Zanzibar.

Lakini wakati polisi wakiwa kimya, kelele zinasikika kila pembe zote za nchi ya Zanzibar na kutoka nje, zikiwemo taarifa za habari za kimataifa, mitandao ya jamii na ya taasisi za nje, kutaka kujua zaidi juu ya habari hizi.

Hali imeonekana kuwa tete zaidi na mijadala kuwa mingi kila pembe ya nchi ya Zanzibar, mijini na vijijini, baada ya shambulio kali la Al Shabaab mwishoni mwa wiki katika Jiji la Nairobi, nchini Kenya, lililosababisha watu zaidi ya 62 kuuawa na wengi kujeruhiwa.

Baadhi ya watu, kwa sababu zao tofauti, wanaonyesha shaka kubwa, na wengine hawataki kabisa kuamini taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi nchini Zanzibar, Mussa Ali Musa.

Mjadala mkubwa umezuka juu ya picha ambazo Kamisha Mussa mwenyewe anaonyesha mageloni madogo meusi ya tindikali zilizokamatwa, na kwamba watu 15 walikuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi. Mengi yamezuka juu ya kauli ya kamishna na hiyo picha inayoonyesha tindikali.


Kwanza watu wanataka kujua nini kimetokea katika kuwachunguza watu hao 15, wangapi wanashikiliwa na polisi na wangapi wameachiliwa...?

Jingine ni wasi wasi kama hicho kilichoonyeshwa ni tindikali au maji ya betri za magari kwa vile hizo chupa zilikuwa na maandishi ya “distillery water”. Je, ni kweli hayo ni maji ya betri au hayo maandishi ni bandia..??

Wataalamu wanaofahamika kujua vizuri masuala ya tindikali na wanaotumia katika kazi zao katika maabara mbalimbali wanasema maji ya betri hayana madhara makubwa kiasi cha kuweza kubabua mwili wa mtu.

Jingine ni kwamba hizo chupa zilikuwa na chapa, maandishi ya wenye maduka. Je, katika uchunguzi imegundulika watu hao wamezipata kihalali..??

Vile vile inasemekana palifanyika uchunguzi katika maabara mbalimbali, zikiwemo za utafiti. Je, nini kilichogunduliwa huko..??

Ni muhimu wananchi kujua ili kila raia mwema ambaye huenda akawa anajua chochote juu ya suala hili aweze kulisaidia Jeshi la Polisi katika uchunguzi wake, kwa sababu linafanya kazi ya kunusuru maisha ya wananchi.

Unapoisoma mitandao mbalimbali ya kijamii na ile ya taasisi za kimataifa ndiyo utaona upo mkorogo juu ya suala hili.

Jamaa mmoja katika mtandao amekwenda mbali zaidi na kuhoji ikiwa maji ya betri ni kosa la jinai. Akasema basi kama ni kosa madereva wote wa magari Unguja na Pemba (pamoja na polisi) wanafanya kitendo cha uhalifu kwa kuendesha gari ambazo betri zake zina maji hayo.

Maelezo haya, kwa vyovyote vile, huenda yakawa ya kejeli, lakini ni ishara ya kuonyesha namna ambavyo watu hawaridhiki na jinsi polisi wanavyolichunguza suala hili.

Ukimya uliopo ndio unatoa mwanya zaidi wa uvumi na hata kusingizia polisi mambo yasiyo ya kweli katika hii kadhia ya mashambulizi ya tindikali.

Kwa vyovyote vile, Kamishana Mussa halitendei haki Jeshi la Polisi, Wazanzibari na Watanganyika kwa ujumla kwa kukaa kimya au kukwepa kujibu maswali ya waandishi wa habari.

Kwa taarifa yake, wanachojaribu kufanya waandishi ni kuwafahamisha wananchi kinachoendelea na hawana ajenda ya siri na wala sio wao waliotaka ajiuzulu kwa madai ameshindwa kazi.

Kama kamishna alikuwa hataki kuulizwa maswali ili atoe ufafanuzi juu ya mambo mbalimbali, basi asingelitoa habari hizo hadharani.

Hapa nigelipenda kukumbusha kwamba Inspekta Jenerali Saidi Mwema, mara tu alipoingia madarakani alifika Zanzibar na kuwataka waandishi wa Tanganyika kulitendea wema na haki Jeshi la Polisi na kutaka pawepo mashirikiano kwa maslahi ya nchi.

IGP Mwema alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Habari Tanganyika (MCT)lilopo Shangani, mbele ya Hoteli ya Serena.

Kauli hii ya IGP ilifuatiwa na Jeshi la Polisi kuweka hadharani kwa waandishi wa habari namba za simu za wakuu na makamanda wa polisi wote wa mikoa. Sasa huu mwenendo wa kukwepa waandishi wa habari unatoka wapi au Jeshi la Polisi limeamua kwenda kinyume na wito wake..??

Kamishna wa Polisi Mussa anapaswa kufahamu kwamba kauli yake ya kuwepo Al Shabaab Visiwani imewashitua sana Wazanzibari wengi ndani na nje na kuanza kujiuliza kama visiwa vyao vipo salama, hasa wakitilia maanani waliyosikia kutokea Somalia na sasa Kenya.

Kama Jeshi la Polisi litafanya utafiti wa haraka haraka litagundua kwa kiasi gani hali imekuwa mbaya na watu kujaa hofu juu ya kuwepo Al Shabaab Visiwani.

Kwa upande mwingine, wataalamu kadha wanaoelewa kwa undani na kufuatilia kwa karibu masuala yenye kuhusu mashambulizi ya kigaidi duniani, wanasema hawana kumbukumbu zinazoonyesha kuwa Al Shabaab wanatumia tindikali katika mashumbulio yao.

Badala yake hutumia silaha za moto, maroketi na mabomu. Hili pia limeonekana katika shambulio liliofanyika Nairobi mwishoni mwa wiki nchini Kenya.

Vile vile sio kawaida kwa Al Shabaab kumlenga mtu mmoja mmoja au wawili, bali hutafuta eneo lililojaa watu na kufanya mashambulio  yao.

Katika hali hii wapo watu wanaouliza je, hawa Al Shabab wanaosemekana kuwepo Visiwani na kufanya mashambulizi kwa kutumia tindikali ni tofauti na hao wanaodaiwa kuwa wenzao waliopo Somalia na wale wanaofanya mashambulizi kwengineko..??

Haya ni masuala mazito ambayo Kamishna Musa anawajibika kwa kila hali kuja hadharani na kuyatolea maelezo, na katika zama hizi za kutafuta ukweli na uwazi, ni vizuri akawa muwazi na kuwa tayari kujibu maswali na sio yeye tu kutaka kuzungumza na kusikilizwa.

Ni vizuri akafahamu kuwa kwa hili hakuna anayemuonea, ni upande wa pili wa sarafu wa kazi ngumu na jukumu alilokuwa nalo kama Kamishna wa Polisi wa nchi ya Zanzibar.

Katika dunia yetu ya leo, hata katika shule, wanaoambiwa jambo au kufundishwa na mwalimu huwa na haki ya kuuliza, tofauti na hali inavyokuwa katika ibada misikitini au kanisani ambako kila anachotamka kiongozi wa dini hupokelewa kimya kimya au kuitikiwa kwa watu kutamka “Amin”.

Ni vizuri kwa Jeshi la Polisi Zanzibar likavunja ukimya na kuuleza umma kinachoendelea.

Hii itaepusha uvumi ambao kwa kawaida haujengi bali unabomoa. Pia kutoa nafasi kwa umma kuchangia kwa njia moja au nyengine kuwanasa hawa wanaotukosesha raha usiku na mchana kwa matumizi ya tindikali kushambulia watu wasiokuwa na hatia na kutuharibia jina la nchi yetu ya Zanzibar.

Tuache ukimya na tuelezane kinachoendelea

No comments:

Post a Comment