Thursday, September 26, 2013

MADISCO,BAA NA KUMBI ZA STAREHE VYATIA FORA YA UFUSKA NA KUSABABISHA VIJANA 30 KUAMBUKIZWA UKIMWI PAJE NCHINI ZANZIBAR


Wananchi wa Kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja nchini Zanzibar wamewalalamikia wamiliki wa baa na kumbi za starehe na madisco zilizomo katika kijiji hicho kutokana na vitendo viovu vinavyo kwenda kinyume na heshima na maadili ya kijiji hicho na nchi ya Zanzibar.
Wananchi hao wametoa malalamiko yao katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk na wamiliki wa baa na madisco zilizomo kijiji hapo uliofanyika Ofisini kwa Waziri Kikwajuni.
Walisema wamiliki wa baa na kumbi za starehe wamekua wakiwasumbua kwa kupiga disco usiku kucha na kusababisha kushindwa kulala majumbani mwao kabisa.
Waliongeza kuwa tabia hiyo inapelekea vishawishi kwa watoto wao na kujiingiza katika mambo maovu yanayokwenda kinyume na mila silka na utamaduni wa kijiji chao na nchi ya Zanzibar pia.
Disco linatuletea usumbufu mkubwa kwa watoto wa kijiji chetu wapo baadhi hawalali makwao usiku mzima,” alisema Mbaraka Salum askari Jamii wa kijiji hicho.
Mbaraka alisesema vitendo vya ngono na kubakwa kwa watoto wa kiume vimekuwa vikifanywa bila woga na vijana 30 wa kijiji hicho tayari wameshaambukizwa virusi vya ukimwi.
Wananchi hao wa Paje wameishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuzuia vibali vya kupiga Disco kumbi zote za starehe ndani ya kijiji hicho kwa kuhofia kutokea madhara makubwa zaidi.
Wamiliki wa Baa na kumbi za starehe kwa upande wao wameitaka serikali iwaangalie kwa jicho la huruma kwa sababu burudani ya ngoma ndiyo inayopelekea kupata wateja na kuongeza kipato chao kinyume chake ni hasara katika biashara yao.
‘’Tunaiomba Serikali ituruhusu japo siku moja kwa wiki tupige ngoma ili tuweze kuingiza mapato,”alisema Mariyam Simba Mkwasi mmiliki wa baa la Vuvuzela. astahafiru allah kisha jina lake ni mariyam
Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Mhe, Said Ali Mbarouk alisema kuwa vibali vya musiki vitaendelea kuzuiliwa ikiwa wamiliki wa sehemu hizo watashidwa kufuata taratibu ziliziowekwa .
‘’Ni bora tukose mapato Serikalini kuliko kuendelea kuwanyima uhuru wananchi wetu tutaendelea kuzuiya vibali vya disco mpaka mujenge kumbi zisizotoa sauti,‘’alisema Waziri wa Habari.
Alisema iwapo kuimarika kwa sekta ya utalii Zanzibar kutasababisha Utamaduni wake kumongonyoka hilo halitawezekana na hatuwezi kupanda mbegu ya ufuska katika visiwa vyetu.
Alisema Zanzibar ina ustaarabu na utamaduni wake, hivyo ametaka kila mmoja ahakikishe kuwa utamaduni huo unalindwa, unadumishwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Kumbi za starehe na burudani zilizolalamikiwa zaidi na wananchi wa kijiji cha Paje ni pamoja na Vuvuzela, Jambo, Gereje na Deman Loge

No comments:

Post a Comment