Thursday, December 26, 2013

HAKUNA ANAYEKATAA USHIRIKIANO, PIA HAKUNA ATAKAYEKUBALI UKOLONI


Na, Ismail Jussa.
Ni ndefu kidogo lakini utapata kujifunza zaidi kuh. Madai yetu yaliyo wazi.
Katika dunia ya leo hakuna anayeweza kukataa USHIRIKIANO ila pia hakuna atakayekubali UKOLONI.
Haya yanayofanywa dhidi ya Zanzibar ni akhasi ya ukoloni. Hata huyo Mngereza hakuifisidi Zanzibar namna ambavyo inafisidiwa na mfumo uliopo wa Muungano. Mngereza alikuwa akifidia nakisi ya bajeti ya makoloni yake.
Huyu wa leo anakamua mpaka maziwa hayatoki tena. Ulikuwa uongezee nukta nyengine kwamba katika PAYE, kuna watumishi wa Muungano waliopo Zanzibar ambao huduma zao zote zinatolewa na SMZ kupitia bajeti yake lakini PAYE wanazolipa kama shilingi bilioni 10 kwa mwaka zinachukuliwa kwenda Tanganyika.
Isitoshe kuna mashirika na taasisi yanayoitwa ya Muungano na humo Zanzibar siyo tu haina mamlaka yoyote katika uendeshaji wake bali hata mapato yake yote yakijumuisha huduma zinazotolewa na matumizi ya eneo la Zanzibar kama anga yake hakuna senti nyekundu inayovuka maji kuja Zanzibar. Mashirika hayo ni pamoja na TTCL, TPC, TPDC, TCAA, na TCRA.
Tunadanganywa kuwa tunapewa asilimia 4.5 ya mapato ya Muungano wakati ukweli ni kwamba tunapewa asilimia 4.5 ya fedha zinazotolewa na nchi wahisani au washirika wa maendeleo kama misaada ya moja kwa moja ya bajeti (General Budget Support-GBS).
Kwa upande mwengine, Tanganyika ikiendelea kujivika joho la Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano imekuwa ikikusanya matrilioni ya shilingi kama misaada ya kisekta (sectoral development programs) ambayo senti moja haivuki maji kuja huku.
Zanzibar imetoa asilimia 11.02 ya hisa iloanzisha Benki Kuu (BOT) lakini haikupata gawio lolote la faida (dividend) kwa miaka 28 tokea 1966 – 1994. Na baada ya hapo imekuwa ikipewa gawio la asilimia 4.5 badala ya asilimia 11.02 ya kima cha hisa katika mtaji uloanzisha BOT.
Zanzibar imelazimishwa kuingia katika kile kilichoitwa usawazishaji wa kodi (harmonisation of tariffs) ili kuua uchumi wake huku ikijulikana hakuna usawazishaji wowote maana bado bandari za Tanga na za mipakani Namanga na Horohoro hutoza viwango vya chini ya vile vilivyowekewa Zanzibar. Hatua hizo zimechukuliwa bila ya kufanywa au kutekelezwa mpango wowote wa kuifidia Zanzibar hasara ya usawazishaji huo ambao kama ingekuwa na mamlaka yake ingeweza kusarifu sera zake za uchumi
vile ipendavyo kwa maslahi yake.
Zanzibar ilifika mahala ikaamua kuanzisha sera ya Off-Shore Banking na Off-Shore Companies na kufikia kuandaa miswada ya sheria kwa madhumuni hayo lakini Waziri wa Tanganyika mwenye mamlaka Kighoma Malima (wakati huo) akamzuia Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Amina Salim Ali, asiiwasilishe Barazani kwa sababu Mtawala hajataka.
Tunaambiwa Mambo ya Nje ni mambo ya Muungano lakini Zanzibar haifaidiki na fursa zozote na ilipotaka kujiunga na OIC ikaamriwa ijitoe. Leo hata makao makuu ya Wizara zote, Idara zote, Mashirika yote, Vikosi vyote vya Muungano yapo Tanganyika na hiyo
maana yake ni fursa ya ajira, uwekezaji, mzunguko wa fedha kibishara katika matumizi, ongezeko la mchango katika GDP na fursa nyengine nyingi na zote hizo ziko Tanganyika. Haya ni
machache zaidi ya yale makubwa uliyokwisha yaeleza kwa ufasaha
mkubwa Abu Muhammad.
Basi labda haya ndiyo hiyo SPECIAL STATUS tunayoambiwa tunaipata. Kama alivyosema Kaplan (ambaye kwa hakika anakariri tu maneno au dira ambayo imeshaelezwa kinaga ubaga hapa hapa), hakuna wa kuizuia Zanzibar kuwa mlango mkuu wa biashara baina ya Afrika ya Mashariki, Kati na Kusini na Bahari ya Hindi. Nafasi ya Zanzibar ni kama zilivyo bandari za Bombay, Dubai, Hong Kong na Singapore. Tatizo ni kukandamizwa kiuchumi, kisiasa na kijamii na kukoseshwa mamlaka ya kujiamulia sera zake huru katika kuyafikia malengo yake ya maendeleo.
Lengo ni kuizuia isijitutumue lakini kwa sasa wahafidhina wamekwama. Umma wa Zanzibar haudanganyiki tena na propaganda za kitoto za Uhizbu na kumrudisha Sultani. Kizazi kipya Zanzibar kinataka mamlaka kamili ya nchi yao kitaifa na kimataifa ili
kujipangia na kujiamualia mustakbali wao utakaopelekea ujenzi wa uchumi imara utakaotoa ajira na kipato cha maana kwa watu wake. Wanaoumizwa na hili watafute pain killers mapema.
— with Ismail Jussa.

No comments:

Post a Comment