Friday, December 6, 2013

KONGAMANO LA KUMBUKUMBU ZA MIAKA 50 YA UHRURU WA NCHI YETU YA ZANZIBAR: DESEMBA ,10 ,1963 NDIO UHURU WA KWELI WA NCHI YETU YA ZANZIBARUMOJA wa Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (MUWAZA) wanaandaa KONGAMANO kubwa la aina yake, kwa lengo la kuifanya HISTORIA ya Zanzibar, iweze kufuata mkondo wake.
Mada muhimu katika Kongamano hilo pamoja na mambo mengine ni kueleza Historia ya kweli ya Visiwa vya Unguja na Pemba, na ufafanuzi wa UHURU wa Zanzibar wa Desemba 10, 1963.
Kongamano hilo ambalo limepangwa kufanyika siku ya Jumamosi Desemba 14, mwaka huu mjini London, limepewa jina ‘KONGAMANO LA KUMBUKUMBU ZA MIAKA 50 YA UHURU WA ZANZIBAR’ pia litachambua hali halisi ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika wa Aprili 26, 1964.
Mwenyekiti wa CHADEMA Tawi  la Uingereza, Salim Amar ambaye ni mmoja wa wataarishaji wa Kongamano hilo, amesema wanalenga katika Kongamano hilo kuweka ufafanuzi wa wazi katika Historia ya Zanzibar, kwa faida ya vijana wa sasa na vizazi vijavyo.
Amesema lengo lao hilo litaweza kusaidia kuvunja nguvu za baadhi ya watu hasa viongozi wa Tanganyika wanaodai kuwa Zanzibar si nchi, huku inajuilikana wazi kuwa Zanzibar, ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza, siku mbili kabla ya uhuru wa Kenya.
Salim Amar, anasema kutokea kwa  Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 isiwe sababu ya kuificha Historia ya kweli ya Zanzibar, na kufanya hivyo ni kupotosha kwa makusudi:
“Mapinduzi yametokea yameshapita sote tunayakubali…lakini hatukubali kupoteza ukweli wa nchi yetu na bila Uhuru yasingeweza kutokea Mapinduzi,” anasema Salim Amar na kuongeza:
“Tunayajua Mapinduzi kwa sababu yamekuwa yakitokea katika mataifa ya Afrika na mengine Ulimwenguni…lakini hakuna nchi hata moja iliyofanya Mapinduzi ikadharau siku yake halisi ya Uhuru kwa sababu ni siku ya Historia,”.
“Lakushangaza hadi leo hii bado tunakumbushwa utumwa pengine ulitokea zaidi ya miaka mia tano (500) nyuma…Uhuru wa raia wa miaka 50 unafichwa na kupotoshwa,” anasema Salim Amar na kufafanua:
“Serikali ya Tanganyika ndiyo iliyowachukuwa viongozi…Mawaziri na viongozi wengine wa serikali ‘Huru ya Zanzibar’ na kuwafunga katika magereza yake…Hivyo Mohamed Shamte Hamad alikuwa muwarabu au mzungu?,” anauliza Salim Amar.
Mohamed Shamte Hamad, alikuwa Waziri Mkuu wa Zanzibar katika Serikali ya MSETO ya Uhuru ya Muungano wa Vyama vya ZNP na ZPPP, chini ya maridhiano yalisimamiwa na Serikali ya Uingereza.
Kuhusu wazungumzaji katika Kongamano hilo ambalo Mwenyekiti wake atakuwa Dk Mohamed Zahran, watoaji mada ni kutoka Canada, Sweden, Denmark, Germany, France na nchi za UAE. Ni watu wanaoijuwa vizuri Historia ya kisiasa ya Zanzibar.
Kuhusu faida ya Kongamano hilo kwa sasa, Salim Amar anasema: “Faida moja kubwa ni kujenga mustakabali wa Zanzibar, Kihistoria, Utamaduni wake, Mila na Silka za watu wa Zanzibar, ili hayo yabaki kuwa urithi wa vizazi vyetu vijavyo,”.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA Uingereza, anasema katika Kongamano hilo ambalo litakuwa wazi kwa watu wote, wataangalia kwa kiasi gani wataweza kutoa michango yao ya fikra katika kuboresha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyo katika muudo wa Kitaifa, ili kuwa na ufanisi kwa wananchi wake wote.
Anasema kwamba wanakusudia sherehe kubwa za kumbukumbu ya Uhuru wa Zanzibar, zitafanyika rasmi hapo Desemba 10, mwaka ujao wa 2014 kwa sherehe itayoshirikisha watu wengi:
“Kwa sasa ni mapema kusema sherehe hizo zitafanyika wapi…nia ya kufanya sherehe kubwa za Uhuru wa Zanzibar…tunayo ili kuiweka Historia ya nchi yetu sawa,” anasema Salim Amar.
Anasema bila ya kufanya kitu kama hicho kila mwaka, kutaweza kutoa mwanya kwa watu waliyo na dhamira mbaya ya kupotosha ukweli kuhusu ‘Historia na Uhuru wa Zanziabr’, kwa maslahi yao binafsi.
Aliyewahi kuwa Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Elimu wa Zanzibar, Omar Ramadhan Mapuri alitunga kitabu kuhusu ‘Historia ya Zanzibar’, kilichoonekana kujaa upotoshaji na uongo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Wananchi (CUF) sasa ni  Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Machano Khamis Ali kwa kushirikiana na baadhi ya Vijana wa CUF, walikichoma moto kitabu hicho katika mkutano mmoja wa hadhara, uliyofanyika Kiwanja cha Malindi, mwaka 1994.
Katika hotuba yake, Machano alisema kuwa kitabu hicho kimejaa uzushi na upotoshaji kuhusu ‘Historia ya Zanzibar’, na hatua ya kukichoma moto hadhari ni kutokana na kukerwa na upotoshaji wa ‘Historia ya Zanzibar’, ndani ya kitabu cha Mapuri.
Mapuri, tayari alikuwa amependekeza kwa taasisi zinazohusika na elimu (Mitaala) kwamba kitabu hicho kifundishwe katika Skuli zote za msingi za Pemba na Unguja.
Wakati huo huo, wanaarifiwa watu wote waliyo ndani na nje ya Uingereza, wanaombwa wahudhurie kwa wingi bila kukosa katika Kongamano hilo ambalo litaanza saa 6:00 kamili adhuhuri hadi saa 11:00 magharibi (12:01pm - 5:00pm) kwa Anwani ifuatayo:-
Durning Hall Community Centre,
Earlham Grove, Forest Gate
London, E7 9AB

No comments:

Post a Comment