Friday, March 20, 2015

HAJI OMAR SHARII ANAJENGA UFALME TUMBATU KWA MAMBO YASIYO WAFAA WANANCHI ILI WAPIGIE KURA KWA LAZIMA


KAZI anayoifanya Haji Omar Kheri jimboni Tumbatu, haitamfalia kitu. Sanasana atakachovuna hatimaye, itakuwa ni fedheha. Anajenga ufalme Tumbatu. Kila ukifika mwaka wa uchaguzi, anapanga mambo yasiyowafaa wananchi anaotaka wampigie kura. Ndio maana kila uchaguzi anatangazwa mshindi hata kama hakustahili. Ni mambo ya kawaida nchini petu ambako mfumo wa uchaguzi bado unabeba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachoishi kwa fikra za viongozi waliofaulu mtihani wa visa na udanganyifu. Hapo nyuma nilijadili kadhia yake huyu jimboni. Nikachapisha hata malalamiko ya wazee wa kijiji cha Chwaka, ya Tumbatu, waliyoyapeleka kwa IGP Omari Mahita, wakati wa Rais Benjamin Mkapa. Walimjulisha IGP matatizo ya kijijini pao. Wakamwambia hawana kosa isipokuwa kutumia uhuru wao tu kuchagua upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF). Wanajua ni halali kwao kuchagua watakacho, lakini uhalali huohuo ndio unatumiwa na wakubwa wa CCM kuwadhalilisha kwa vipigo na kuchoma nyumba zao pamoja na kuharibu Msikiti wao. Sasa wakataka serikali izuie vitendo vya kuwadhalilisha. Ila wakasema si kwamba wanalalamika tu hawana nguvu ya kujitetea, hapana. Wana nguvu zao wangepambana, lakini hawataki mapambano kwa siasa wanataka wahuni wazuiwe kuwasumbua.
Hata hawakujibiwa ingawa hali ilitulia na wakaendelea na maisha yao. Waliwataja wabaya wao, wale wanasiasa wanaowahujumu. Ni hapa wakamtaja Kheri huyu.
Sasa Kheri anataka kura maana msimu uko karibu. Anajua hazipati bila vitisho na kudhalilisha wananchi. Anajifanya jogoo la mtaa asiruke mwingine. Ajitawale atakavyo. Kumezuka visa Uvivini. Walioanza ambao ndio wangekamatwa na kushitakiwa kwa kuanzisha vurugu, wanachekelea. Vitisho vimebaki kwa waliodhalilishwa. Wahuni wameteremsha bendera za CUF. Wakapiga mbio kulalamika maskani zao zimechomwa moto. Upuuzi mtupu mahayawani hawa wanaolindwa na dola. Visa waanze wao, lawama watoe wao. Kumetulia lakini mbinu za uchokozi zimewashwa. Anayejitia ujogoo anatamba kwa kuapa CUF marufuku Tumbatu. Kheri akibaki mwanasiasa peke yake, ndio atatulia? Labda amesahau. Namkumbusha mtu aliyetamba Zanzibar lakini leo anamrudia muumba. Hasogei panapopangwa upuuzi. Ali Juma Shamhuna amemzidi umri, uwezo wa kufikiri, uzoefu katika siasa na uongozi. Ni mwingi wa mbinu za kupigana kisiasa. Shamhuna ni waziri kama Kheri. Bali mwenzake amepea kila kitu. Hapendi tena siasa za nguvu na ghamidha. Shamhuna amepoa.
Baada ya miaka mingi ya kukurukakara na panda-shuka madongo kuporomoka, akisema na kutema cheche, akivinjari na kutisha madui, leo kama si yeye; mtulivu. Alipokuwa na nguvu, si tu hakutamani upinzani kupenya Donge hata iweje, bali alipanga mbinu za medani hasa zilizolenga kuhakikisha kiongozi mpendwa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, hagusi Donge. Shamhuna alisimamia, tena kwa kutumia gari na watumishi wa serikali, njama zilizokusudiwa kumzuia Maalim Seif na CUF, asihutubie Donge. Vyombo vya dola, Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, vilimkubali na kumtii. Alitumia ipasavyo wadhifa wa Naibu Waziri Kiongozi wakati wa uongozi wa Amani Abeid Karume. Vi 999, gari za polisi, vilishaamini Donge ndio nyumbani. Barabara ya Mahonda-Donge ilishazoea, ikifika jioni, kukabili msafara wa mfalme Shamhuna. Misafara yake ilikuwa jambo la kawaida karibu kila siku. Wakati mwingine akirudi usiku kama mpango wa siku hiyo haukuwa wa kulala kijijini. Mipango ya siasa chafu ikipangwa mjini, baadhi ya muda ofisini kwake, lakini utekelezaji hulazimu watekelezaji waende Donge.
Wakati fulani rafiki yangu ambaye ni mwakilishi sasa katika jimbo Kaskazini Unguja, aliniambia Shamhuna akiwaita maofisa wa serikalini wa wilayani au mkoani, kuwatisha wamtii. Kwa kuwa mambo ya kijitu kizima hapewi mtoto, ndio maana mwenyewe akilazimika kwenda jimboni. Sina hakika kama alienda sambamba na mfalme mwenzake jimboni, Ali Ameir Mohamed. Yawezekana ndio CUF walipotaka kutafuta kura za Donge kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa inayoelekeza chama kwenda kwa wananchi kutafuta ufuasi. Wafalme leo kila mmoja tuli. Ali Ameir aliyekuwa mbunge kwa enzi, amestaafu na kwa hali yake ya afya sasa, muda mwingi amepakata miguu barazani. Shamhuna, mwakilishi, yungali serikalini ambako ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali. Ninaamini anamaliza muda astaafu siasa. Sijawahi kukutana naye karibu siku nyingi; sidhani kama anahamu ya kugombea tena Oktoba 2015. Nataka kuamini ule urais alioupania 2010, hautamani tena. Hana kasi ile aloanzia ujanani akisakata gozi na vijana wenzake kama sahibu, kaka na mwalimu wangu Salim Said Salim, Suleiman Othman Nyanga, Yussuf Omar Chunda na Mzee Mkweche.
Walikuwa wafalme jeuri Donge. Wawapi leo? Magharibi imeingia; tena wakati tayari Donge ina matawi hai ya CUF. Umma wa jimboni umeipokea CUF kama vile imezaliwa jana. Wananchi wamejitoa na wanajiamini. Wamevua ujinga wa kuangalia misafara ya CUF kwa dirishani kwa kuwa wamekatazwa kutoka nje kushangiria. Wakinyimwa haki na uhuru wa kikatiba na kibinadamu. Mwaka 2013, viongozi wa CUF Donge Muwanda, walifanikiwa kushawishi chama kumpeleka Maalim Seif kuhutubia. Kabla haikuwa rahisi. Ulikuwa mkutano uliotangazwa sana. Asia, Ulaya na Marekani. Nilihudhuria maana yapo mambo kwa fani yetu huruhusiwi kusubiri simulizi. Unakwenda kushuhudia. Mwalimu mmoja alipopewa nafasi ya kuhutubia umma, alitoboa siri ya alivyotumikishwa na CCM kila uchaguzi. Wacha avunje mbavu huku akisononesha umma kwa visa. Akasimulia alivyozoea kupiga kura hata mia katika vituo tofauti jimboni na majimbo mengine Unguja. Alitekeleza hayo chini ya walinzi wa serikali. Siku hiyo akatangaza rasmi amehama CCM na amehamia CUF. Alipokuwa anakabidhiwa kadi ya CUF na Maalim Seif, karibu apinduke kwa furaha. Kama vile akiota lini atakutana naye uso kwa uso, mwalimu alimtaka amsamehe binafsi duniani na akhera, kwa kutumia mkono wake kumdhulumu kura za urais walizotumwa kuziharibu masandukuni.
Akasema amechoka kutumwa kuhujumu ikiwemo kutakiwa kudhuru ndugu na jamaa wa Donge na kule alikopata kuagizwa kufanya kazi chafu. “Tafadhalini ndugu zangu nipokeeni. Nimeamua kuachana na mipango ya dhulma, fitna na uchonganishi wa sisi kwa sisi. Walipopata basi, nataka nguvu na akili niitumie kuijenga CUF na Muwanda yetu. Nipeni kazi nifanye,” alisema akisihi wana-CUF wamsamehe na kumridhia kuwa ndugu yao katika kundi. Leo Donge ni nyingine si ile ya wakati wafalme wana nguvu na pesa za kifisadi. Uharibifu hawauwezi tena zaidi ya kuhesabu tasbihi. Wakati umewapita. Tunaambiwa dhulma haidumu siku zote, wanaodhulumu nao ni binadamu – watachoka. Kwa bahati, baadhi ya dhulumati hufika mahala wakajitambua na kujirudi. Wakaamini hawawezi kubakia wakidhulumu tu, ilhali iko siku watakufa. Bahati yao. Uzuri wa mtu ni kuacha mabaya akiwa na nguvu. Basi akijisahau angalau awache anajiweza kusema, “Ewe Allah nisamehe mja wako nilikosea na kukukosea, nilidhulumu viumbe wako, ninatubu yailahi.” 
Kheri anasumbuliwa na jeuri tu. Anadhani haitakwisha? Tusubiri.
KILA MZANZIBARI ATAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.

No comments:

Post a Comment