Friday, October 2, 2015

NCHINI TANGANYIKA LOWASSA ANGURUMA JIJINI DAR ASEMA SIKU 100 ATAFANYA MAMBO 13


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Edward Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika viwanja vya TP Sinza Uzuri, jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis
Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa ametaja mambo 13 atakayoyafanya ndani ya siku 100 iwapo atachaguliwa kuwa Rais, huku akisema “atawakata kilimilimi” wanaombeza kuwa hawezi kuondoa umaskini wa wananchi. Lowassa alikuwa akihitimisha mikutano minne aliyofanya kwenye wilaya tatu za Jiji la Dar es Salaam jana kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe. Wakati Lowassa akieleza hayo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alitangaza azimio la Kawe lililobeba ajenda kuu tatu, ikiwamo ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa mwongozo wa jinsi Serikali yake itakavyokabidhi madaraka kwa Ukawa kutokana na suala hilo kutokuwapo kikatiba. Wakati huo huo: Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akitangaza mkesha kwa wananchi siku ya kuamkia tarehe ya kupigakura na kutaka wanaume wabakie kulinda kura zisiibiwe. Akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya watu na viongozi wakuu wa Ukawa, Lowassa alisema mambo hayo atayatekeleza kwa kasi ya kilometa 120 kwa saa. Lowassa alitaja jambo la kwanza atakaloanza nalo kuwa ni uhakika wa dawa na vifaa vya uzazi wa akinamama. Alitaja mambo mengine kuwa ni umeme wa uhakika nchi nzima, kupunguza foleni jijini Dar es Salaam, kuondoa kero kwa wafanyabiashara wadogowadogo na waendesha bodaboda, kumaliza tatizo la maji nchi nzima, mfumo bora na rafiki wa wafanyabishara wakubwa na wadogo.
Kufuta ada na michango kwa wanafunzi, kupunguza kodi ya mshahara kwa wafanyakazi, kufuta kodi zote za mazao ya wakulima, mkakati wa kukuza michezo na sanaa, kuunda tume ya kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima, kuanzisha kituo kila wilaya kwa ajili ya kutoa huduma za serikali na kuboresha maslahi ya polisi, wanajeshi na walimu. Mbali na mambo hayo 13, aliahidi kumaliza kilio cha wananchi cha kupata Katiba mpya inayotokana na maoni yao, akisema ni suala linalohitaji kutuliza kichwa kulipatia ufumbuzi. “Umaskini si mpango wa Mungu,” alisema Lowassa ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu. “Nina hasira ya kupambana nao na kuwaondoa Watanzania katika umaskini.” Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyeihama CCM mwishoni mwa mwezi Julai, aligoma kushuka jukwaani akitaka awekewe muziki acheze na maelfu ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza na kumkumbatia mkewe, Regina ambaye alifika uwanjani hapo wakati mkutano huo ukikaribia kumalizika, kisha akambusu. Awali, Lowassa alisema idadi ya kura anazohitaji ili ashinde urais ni milioni 14. Akiwa Mafinga mkoani Iringa, Lowassa aliomba wananchi wampigie kura milioni 10 ili awe Rais lakini jana alisema kuna haja ya kupata kura nyingi iwezekanavyo ili ushindi wake usiathiriwe. “Kilichonileta hapa ni kuomba kura,” alisema Lowassa. “Naomba mnipigie kura milioni 14 na ushee ili ziweze kutosha kuwa Rais. Baada ya kupiga kura, wananchi mnatakiwa kuzilinda ili zisiibwe.”
Lissu
Kabla ya Lowassa kupanda jukwaani, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alitoa ufafanuzi wa alichoita “tamko la Kawe” ambalo ni kutaka ufafanuzi wa jinsi ya kukabidhiwa madaraka kwa upinzani, kitu ambacho alisema hakijaelezwa kwenye katiba. Alisema jambo jingine ni kumtaka Rais Kikwete ajibu kauli iliyotolewa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo kuwa CCM haitatoka Ikulu. “Kikwete atueleze kama hili ni tamko ni la chama au Bulembo,” alisema Lissu, ambaye pia anatetea kiti chake cha ubunge cha Jimbo la Singida Mashariki.
Mbowe
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Lowassa, Mbowe aliwataka wafuasi na wanachama wa Chadema na Ukawa kuhakikisha wanakesha Oktoba 24, kujiandaa kupiga kura siku inayofuata: “Bado siku 24 tufanya uamuzi wa hatma ya maisha yetu na kuonyesha hasira kwa kutoichagua CCM,” alisema Mbowe. “Tunakwenda kuanza safari ya uhakika ya kutoa mwanga kwa taifa letu na kuonyesha heshima ya nchi na watu wake…“Oktoba 24 ni siku ya nini?…Ni siku ya kukesha kusubiri kupiga kura…Tunakubaliana tutakesha...?” Wananchi walimjibu kwa kelele kuwa watakesha na ndipo alipotoa maelekezo. “Akinamama mkishapiga kura rudini nyumbani mkaandae chakula, ila wanaume watabaki vituoni kulinda kura. Lakini hesabu hatua ya kwanza, ya pili… hadi zifike mia na hapo pigeni kambi kulinda kura,” alisema Mbowe. Kwenye mkutano wa Liwiti, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye aliendeleza kampeni zake za kumnadi Lowassa huku akirusha tuhuma dhidi ya CCM na Serikali.
Sumaye alisema ni aibu kwa meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi kugombea ubunge wakati jiji analoongoza limekithiri kwa kipindupindu. “Ni lazima tuwe na aibu. Masaburi, jiji ni chafu limekushinda kipindupindu `kinatamba’ sasa unataka ubunge wa Ubungo, unadhani wananchi hawana akili za kupima,” alisema. Akiwa Kawe, Sumaye alimshangaa mgombea wa CCM, Dk John Magufuli akisema kuwa huwa ana maamuzi ya kukurupuka hadi ashikwe shati na kwamba akiwa Rais hakutakuwa na mtu wa kumzuia. Alisema alitaka kuvunja jengo la Tanesco la Ubungo ambalo limejengwa kwa kodi za wananchi, lakini akazuiwa. Pia aliamua kujenga barabara bila ya kuwa na fedha za kuwalipa makandarasi na kusababisha Serikali idaiwe Sh900 bilioni za riba, huku uamuzi wake wa kukamata meli ya uvuvi ukiigharimu Serikali mabilioni ya fedha.
Mbatia
Naye mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alikitaka Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuitisha mkutano utakaovishirikisha vyama vya siasa ili Ukawa na CCM wakubaliane kuyakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu ikiwa tu utakuwa wa uhuru na haki. Mbatia, ambaye anagombea ubunge jimbo la Vunjo, alidai kuwa Serikali imeuza hisa zake katika kampuni ya bia ya TBL kwa Sh176 bilioni na kuzipeleka fedha hizo katika uchaguzi, huku akikitaka CCM kuibuka na kujibu jambo hilo akisema anao ushahidi.
Mnyika na Lubuva
Akizungumza kwenye mkutano huo wa Kawe, mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika alimtaka mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva kuwapa jibu kabla ya Oktoba 4, mwaka huu kuhusu kupeleka wataalamu wao wa Tehama kwenda kuhakiki mfumo wa utakaotumika kupokea na kujumlisha kura za urais kwa lengo la kujua kama uko salama ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Awanadi Kubenea, Mdee, Mnyika
Akimnadi Saed Kubenea, ambaye anagombea ubunge wa Jimbo la Ubungo, Lowassa alisema sekta ya habari itapoteza mwandishi mahiri katika kazi yake, lakini wana Ubungo watakuwa wamepata mtetezi wa haki za wananchi. “Kubenea ni jembe mchagueni ili akafanye kazi bungeni na kusimamia maendeleo ya jimbo lenu,” alisema Lowassa. Pia alimnadi mgombea ubunge wa Kawe, Halima Mdee akimuelezea kuwa ni sururu badala ya jembe.
KILA MZANZIBARI ATAKAE IPIGIA KURA CCM ILI IBAKI MADARAKANI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.

No comments:

Post a Comment