Wednesday, March 23, 2016

MFALME SHEIN KESHO NDIO SIKU YAKE YA KWENDA KUJIAPIZA KWA KUSHIKA MSAHAFU NAKUJIMALIZA MWENYEWE

Kesho kwa furaha isio kifani vifijo na nderemo kwa wana wa CCM, mfalme wao atajivisha lile joho lisiloonekana na kujiapiza kwa kuapa huku akiwa ameshika msahafu kwamba atawatumikia mahuluku wote katika ufalme wake huo bila kujali kwamba wote, akiwemo yeye mwenyewe wanamuona kwamba yeye hajavaa joho la ufalme huo bali yuko uchi. Wana giningi hao ambao watafurika katika uwanja wa Imani, wengi kwa hiari yao kwa matamanio ya kuendelea kula nyama za bure na wengine kwa kulazimishwa kimisukule, ama nguvu ya Dola, wataingia uwanjani hapo kwa mbwembwe wakiwa na mabango ya kushajiisha mapenzi katika jamii na vibwagizo kama vile “machotara, mahizbu warudi kwao, Zanzibar ni nchi ya Waafrika” huku wakiwa wamependeza kwa sare zao za kijani na njano. Uwanja utazizima kwa wafuasi ambao wataletwa kwa magari ya bure yaliyoandaliwa maalum kwa siku hii adhimu na wengine kutoka upande wa Mrimani kuletwa kuja kujumuika pamoja kushereheka na kushuhudia mfalme akiapishwa. Nyimbo maalum za mapenzi kwa majirani na maswahiba kama zile za “waso haya wana mji wao!” zitaimbwa kutumbuiza halaiki na kuuaminisha ulimwengu pia mapenzi waliyonayo mahuluku tabu hawa kwa mfalme huyu na chama chake.
Vikundi mbali mbali vya ngoma na maigizo vitakuwepo kutoa burudani na kusifu mafanikio makubwa na maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya utawala wa mfalme, mafanikio yaliyopelekea nchi kung’ara na hali za wananchi kunawiri bila ya kusahau Amani na utulivu ulivyotamalaki kila kipembe cha visiwa hivi vya marashi ya karafuu.”Tumpongeze kwa makofi mengi basi mpendwa wetu kwa hayo,” atasikikika mshereheshaji akitamba kauli itayopelekea Mkulu Makomeo kukenua pamoja na wafalme wastaafu wapendwa. Uwanja utalipuka kwa chereko na nderemo pale ambapo mfalme ataposhuka na kuanza kukagua vikosi vyake vya ulinzi, na vile vya Baba Mkubwa, gwaride na mizinga itapopigwa huku akipita juu ya zulia jekundu kwa staili ya aina yake, kimoyo moyo akijiaminisha na kujisemeza “mimi ndie mfalme wa watu wote hawa, wananipenda na ulimwengu unashuhudia namna joho langu lilivyonipendeza.” Wakati wa kupanda kilinge utawadia na mfalme atavishwa joho lake la utawala kwa kuapa na kujiapiza kwa kushika msahafu kwamba yeye ndiye mfalme wa Wazenji na atawatumikia kwa bidii wote wanaotaka na wasiotaka. Kiapo chake kitakwenda kama hivi, “ Mimi mfalme wenu naahidi kuendelea kuivunja katiba hii ninayoiapia na kuwaadhibu katika kipindi hichi cha miaka mitano ijayo, na ikiwezekana maisha na kuimarisha na kuyalinda mapinduzi matukufu bila kuusahau muungano ambao umeniweka hapa nilipo, ewe roho yangu nisaidie”
Hapo viongozi wa dini zote wakiongozwa na jaji mkuu wa Zanzibar walionunuliwa kwa ahadi za mkate mnono watampatia Baraka za kuongoza mfalme wetu na shangwe, nderemo, vifijo na vigelegele vitatawala uwanja wa Imani, mshereheshaji alie na akili na kipaji cha kuzaliwa kwa jina la Bora Afya atasikikia akinguruma kwa maneno “CCM oyee…” kwa kila matusi mawili atayokuwa akiyamwaga uwanjani hapo. “Mara hii hamtokula zabibu za maboksi, mara hii mtachuma halua kwa mikono yenu…”ahadi nono zitatolewa na mfalme wetu kukumbushia kipindi cha neema kilichopita cha Komandoo. Zanzibar itaiingia katika kipindi cha neema na ujenzi wa Zanzibar mpya utaanza mara moja. huku kauli mbiu ikiwa “ Kidumu chama cha Kifalme, Zidumu fikra za mfalme, Ufalme Daima” Sauti itasikika ikiwaambia wambea wanaosikiza redioni “haya basi mlie tu kama bado machozi hayajakauka, sisi wenye nchi hii tunawarudisha katika studio zetu huru za ZBC na televisheni yenu pendwa ya TVZ kuendelea kusherehekea ushindi wa mfalme wenu,kwani tunajua mnampenda mfalme wenu, pongezi zote ziende kwa Jecha kwa kazi nzuri aliyoifanya. Mapinduzi Daima.” Kweli kuna wataodunguka roho kwa kuona safari ya matumaini imekufa, na kuna wataolia kwa kuhisi safari ya matumaini imefikia ukingoni, lakini kuna wenye roho ngumu wataojibu kwa kusimama imara kuitetea Zanzibar hadi mwisho, katika hao ndio wanaosema safari ndio kwanza inaanza. Zanzibar Daima.
KISHA NYINYI MUNAYAITA MAPINDUZI MATUKUFU HIVI KWELI NYINYI MUNAJUWA UTUKUFU NI NINI AU DUNIA IMEWAVA KISAWA SAWA MPAKA MNAKUFURU

KILA MZANZIBARI ALIYE IPIGIA KURA CCM AU MPAKA WAKATI HUU BADO ANAISAPOTI CCM ILI IBAKI MADARAKANI JAPO KUWA CCM IMESHINDWA UCHAGUZI AJUWE NA YEYE ANACHANGIA KUENDELEZA DHULMA NA KUFUNGWA KWA MASHEIKH NA KUTHALILISHWA KWAO NA KUENDELEZA DHULMA KATIKA NCHI YA ZANZIBAR UKAE UKIJUWA UTAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA,KUDHULUMIWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.

No comments:

Post a Comment