Thursday, July 14, 2016

SHEIN, JE HAYA YATOSHA KUWA THAMANI YA URAIS WAKO ?

WANAJESHI WA MKOLONI MWEUSI TANGANYIKA WALIPO PEWA AMRI NA KIKWETE KUKIZUNGUKA KITUO CHA KUTANGAZIA KURA HALALI CHA NCHINI ZANZIBAR UCHAGUZI WA 2015 HUU UKAWA MWANZO NA MWISHO KURA HALALI ZILIZOPIGWA NA WAZANZIBARI KUPINDULIWA NA JESHI LA MKOLONI MWEUSI TANGANYIKA KWA AMRI YA KIKWETE.
UCHAGUZI WA ZANZIBAR 2010 SHEIN ALIPO SHINDWA
UCHAGUZI WA ZANZIBAR 2015 SHEIN ALIPO SHINDWA
Maswali yangu hasa kwa Shein nitayaweka mwisho wa makala hii, lakini nitatanguliza kwanza kile kilichonisukuma kuyauliza maswali yenyewe, nacho ni hali ngumu inayopitia nchi yangu, Zanzibar, kwa sasa, ili tu kuhalalisha urais wa Shein. Jamii ya Kizanzibari ipo kwenye madhila makubwa wakati huu kwenye kila nyanja iyagusayo maisha yake. Kila jambo takribani limeharibika na sasa imegeuka jamii iishio kwa kutegemea zaidi kudra. Si ajira, si biashara, si ujasiriamali. Si elimu, si tiba. Kote kuko hoi-bin-taabani. Hakuna kitizamikacho tena, bali vyote vimevurugwa vururu vururu! Kwa miezi kadhaa nimekuwa nikifanya uchunguzi ili niandike makala zinazohusiana na huduma za kijamii hapa kisiwani Pemba. Katika uchunguzi huu, nimefika maeneo 
mbalimbali kulingana na kile nilichokuwa ninakichunguza. Kutoka mahospitalini hadi maskulini, kutoka maofisi ya ustawi wa jamii hadi taasisi za fedha. Leo nitazungumzia eneo mojawapo kati ya hayo, yaani huduma za afya kwenye mahospitali ya umma.
Nimebahatika kufika takribani zote tatu kati ya nne kubwa – ya Chake Chake, ya Wete na ya Micheweni – pamoja na vituo vidogo vidogo vya afya kwenye kisiwa hiki. Picha ya jumla kwa mote humo ni hali ni mbaya yenye viashiria vyote vya jamii kupoteza nguvukazi kubwa kutokana na uhaba mkubwa wa madawa na vifaa tiba muhimu kwa maisha ya mwanadamu. Kuna siku nilitembelea Hospitali Kuu ya Chake Chake. Hii ni hospitali kubwa na muhimu kwa maisha ya wananchi wa mikoa yote miwili – kusini iliko na kaskazini ninakoishi mimi. Siku hiyo nilimuona mzee aliyetoka masafa ya mbali akiwa na cheti kinachoonesha orodha ya vifaa tiba, yakiwemo mabomba ya sindano, glavu na madawa, kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake aliyekuwa amelazwa hapo. Kwa kumuangalia usoni na mwilini mwake, nilimuona yule mzee akiwa na dalili zote za umasikini wa kupitiliza. Aliniambia kuwa alikuwa amekipokea cheti cha orodha ile ya madawa siku mbili nyuma. Ilipofika siku ya tatu, ambayo ndiyo niliokutana naye, tayari alikuwa ameshachanganyikiwa. Hakuwa na vifaa na mtoto wake aliendelea kuteseka, akiwa hajatibiwa. Nilimkuta amekaa kando ya kitanda cha mgonjwa wake na watoto wake wengine wawili waliokuwa wamefika pale kumjulia hali ndugu yao. Walikuwa wanajadili namna ya kuzipata dawa zile ambazo ziligharimu takribani shilingi 45,000. Mungu bariki, akatokea kaka mkubwa wa mzee huyu, ambaye hatimaye alifanikisha upatikanaji madawa na vifaa vile kwa njia ya mkopo, kwani hadi anawasili hospitalini zilikuwa zimechangwa shilingi 14,000 tu.
Haikupita muda vifaa na madawa yakaletwa na kukabidhiwa nesi, ambaye naye hapo hapo akavifungua na kumpa tiba yule mgonjwa niliyesikia akiitwa kwa jina la Bakari. Hata hivyo, kitambo cha dakika saba baadaye, Bakari akakata roho, huku macho yangu yakimshuhudia. Nikaiona maiti ya Bakari ikinyooshwa viungo na kuzibwa mdomo na baadaye kufunikwa shuka, ambalo dakika chache zilizopita alikuwa amefunikwa hadi kifuani. Hili lilifanyika baada ya daktari wa zamu kuthibitisha kwamba kweli Bakari alishafariki dunia. Muda mchache akaingia bwana mmoja niliyesikia akiitwa kwa jina la Ali, ambaye ni mtoto wa yule kaka mkubwa wa baba yake marehemu Bakari aliyekuwa amejitolea kubeba dhamana ya deni ili kunusuru maisha ya mtoto wa mdogo wake. Ali alikumbwa na fadhaa alipoelezwa mkasa mzima uliotawala kifo cha mdogo wake, binami yake. Kinyume na waliokuwapo kabla yake, yeye hakuweza kuyameza machungu yale. Akaripuka kwa hasira na malalamiko, akiuonesha hisia za wazi za mtu aliyechoshwa na hali inayowakabili wanyonge wengi pindi wakiugua. Mbele ya maiti ya ndugu yake, ndugu na jamaa zake na mbele ya madaktari na manesi ambao muda huu walikuwa chini ya kitanda cha marehemu Bakari, Ali alisema: “Sisi bwana twauliwa ni serikali yetu. Huyu mtoto yuko hapa leo ya tatu, hajaulizwa chochote. Madaktari waja wakirudi tu, hakuna wanachomfanyia. Eti leo baada ya kumuona anakata roho, ndio wanatowa kikaratasi watu wakanunue dawa! Mzee kaingia deni. Dawa zimefunguliwa kabla hazijatumika mtu anakata roho! Sisi bwana twauliwa ni serikali yetu!”
Kauli ya Ali ikamfanya daktari wa zamu akanushe. Nadhani alihisi kuwa mimi ni mwandishi wa habari, na hivyo akataka kuweka rikodi sawa. Daktari huyo, ambaye sitamtaja jina kwa leo, alisema wao hawahusiki na mauti ya Bakari. “Sisi hapa tuna kazi ya kutibu na kutoa usimamizi kwa wagonjwa mara wanapofikishwa kwetu. Kwa vile madawa hatuna, huwa tunachunguza tatizo la mgonjwa na kisha kuandika aina za madawa ambayo anapaswa kutumia kulingana na tatizo lake na kuikabidhisha orodha ya madawa stahiki kwa ndugu wa mgonjwa husika. Huyu mtoto alifika hapa juzi jioni na jana ndugu zake nikawakabidhi orodha hiyo, kwa vile hapa hospitalini hatuna madawa hayo. Jana jioni nilipita hapa, lakini dawa hazikuwa zimeshanunuliwa na leo nimefika asubuhi pia dawa hazikuwepo. Muda mfupi ndio dawa zimefika, nasi tumetimiza wajibu wetu wa kumtibu, ingawa haikusaidia. Lakini pamoja na yote, sisi kama wahudumu wa wagonjwa, hatuna pesa mifukoni mwetu za kuwanunulia wagonjwa madawa. Usitushutumu kaka, hatuhusiki na hili.” Alimaliza kujitetea daktari huyu wa kike, aliyekuwa kavalia suruali ya jinzi chini na kishati cha buluu iliyopayuka juu yake. Mimi nilinyamaza kimya, ingawa ni kama kwamba yote yale alikuwa akinieleza mimi badala ya Ali na ndugu zake. Sikutaka kumuhoji wala kumuhukumu yeyote kati yao. Nilijuwa wote ni wahanga wa nguvu zilizo juu yao – tena nguvu zenyewe si Mungu Muumba, bali umasikini ulioumbwa na watawala dhidi yao. Lililotokea baada ya tukio hili ndilo lililothibitisha hukumu yangu.
Hilo ni pale familia ya marehemu ilipolazimika kulipia shilingi 25,000 kwa ajili ya mafuta ya gari la wagonjwa la hospitali hiyo kuurejesha mwili wa mtoto wao kijijini kwao. Nilijisikia vibaya kulingana na mazingira ya kadhia hii vile nilivyoishuhudia hadi kufikia pale. Nilitegemea kwamba mara baada ya Bakari kufariki, uongozi wa hospitali ungetowa usafiri kuisafirisha maiti yake hadi kijijini kwao. Lakini badala yake nikashuhudia familia ikikamuliwa tena kugharamikia mafuta ya gari, ambayo mwenyewe nimewahi kuishuhudia mitaani mara kadhaa ikipiga misere! Kuna siku nyengine nilifika hospitali ya Wete. Pale nilishuhudia ndugu wa mgonjwa mmoja wameishiwa nguvu na hawana tena namna. Hawa walilazimika kununua damu zaidi ya chupa tano ili kuokoa maisha ya ndugu yao. Hali hii ilishawachosha kwani ilishawakausha kila aina ya akiba waliyokuwa nayo. Walikaa wakisubiri kudra ya Mungu itakapowapeleka, kwani wao kama wao hawakuwa tena na namna. Hivi makaribuni mzee wangu aliugua ghafla na tukalazimika tumkimbize hospitali ya Micheweni. Tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua ilikuwa presha na tukawa hatuna jinsi bali tumkimbizie huko kuokoa maisha yake. Hata hivyo, licha ya madaktari wenyewe kutueleza kwamba kweli presha yake ilikuwa juu, ilishindikana kupatikana tiba ya kurekebisha tatizo hilo na tukalazimika kurudi naye nyumbani. Tulifanya hivyo kwa ushauri wa madaktari hao wenyewe waliotueleza waziwazi kwamba kumuacha pale kungelikuwa ni kumuongezea mateso yeye mgonjwa na sisi wauguzaji, kwani kama kilichotupeleka pale ilikuwa tiba, basi tiba haikuwepo! Daktari mmoja nilimuona akajisikia huzuni kutokana na hali ya mzee wangu na akachakua kwenye mfuko wake wa koti, akapata kidonge kimoja tu, ambacho mimi sikujua kinatibu nini, akampa mzee wetu. Tukarudi nyumbani na usiku huo mzima sikulala nikifikiria namna mimi na watoto wangu tusivyo salama!
Asubuhi na mapema ya Jumatatu ya tarehe 11 Julai 2016, mke wangu aliamkia hospitalini kwa lengo la kumpigisha chanjo mtoto wetu wa siku 54. Kitoto hiki tangu kimezaliwa hadi siku hiyo, kilikuwa hakijafanikiwa kupata chanjo ya aina yoyote, jambo ambalo si sawa. Kilizaliwa kisiwani Unguja siku kadhaa zilizopita na kukaa huko kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kunifuata huku kisiwani Pemba. Kwa mujibu wa maelezo ya mama yake, alipata kufika hospitali ya serikali pale Mwembeladu, lakini nako alishindwa kupata chanjo kwa maelezo kwamba: “Chanjo hakuna!” Ndipo Jumatatu hiyo akarudi tena hospitalini kufatilia, lakini alielezwa lugha hiyo hiyo kwamba chanjo hakuna, bali akaongezewa jengine linalotisha zaidi: “Haiijulikani zitakuwepo mwaka gani!” Hili la kukosekana chanjo si la kuhadithiwa, bali nimelisikia kwa masikio yangu mwenyewe. Siku moja nikiwa hospitalini, nilishuhudia watoto waliofikisha miezi tisa wakikosa chanjo kwa maelezo kwamba wanatakiwa wawepo watoto kumi ndipo wachanjwe na kwa vile siku hiyo kumi hawakuwepo bali walikuwa watatu tu, ikawalazimu wazazi wao kuondoka na watoto wao kurejea makwao kutokana na kutokidhi masharti ya chanjo hiyo. Hii ndiyo hali ya hospitali za Pemba. Pengine haijaanza jana na leo, lakini imeshamiri zaidi baada ya wafadhili kukata misaada kwa serikali za Zanzibar na Tanganyika Mkoloni Mweusi kwa ujumla, baada ya chama cha Mkoloni Mweusi Tanganyika, CCM, kunga’nga’nia madaraka kuendelea kuitawala nchi ya Zanzibar kimabavu na guvu za jeshi na kutoheshimu maamuzi ya umma, ambao ulikuwa umeamua kubadilisha utawala wa nchi kwa njia halali ya kura ya tarehe 25 Oktoba 2015. Ni hili la maamuzi ya umma kupinduliwa ndilo lililowapelekea wafadhili kujitoa kuendelea kufadhili serikali ambayo inaendeshwa bila ya ridhaa ya wananchi.
Hali hii inamaanisha kuwa tunaishi kwenye nchi iliyododa na kwa hivyo hatuko salama. Ndio maana, wengine tunaamini kuwa sasa panahitajika tafakuri na maamuzi mapya ya kutukwamua ili tusonge mbele. Huu si muda wa kutowa kauli za kibabe, wakati watu wanakufa kwa kukosa madawa hospitalini. Huu si muda wa kujinata kwamba tuna vifaru, lakini kumbe hatuna hata kichupa cha chanjo kwenye mahospitali na zahanati zetu. Huu si muda wa kurusha vijembe na kejeli kwamba hakuna serikali ya mpito wala ya kurudi wakati hatuna hata pamba na glavzi. Huu ni muda wa kukaa chini na kufanya tafakuri jadidi, tukijiuliza kwa nini yakatufika haya na kukubali majibu ya swali hilo. Dhana na fikra ya khofu imetanda kwenye mioyo ya wengi kiasi cha kuathiri maisha ya wafanyakazi wengi wa serikali hapa kisiwani Pemba. Wamiliki wengi wa biashara wametanda khofu ya kupoteza vyao kutokana na uvumi uliozagaa kwamba serikali ya Zanzibar kwa sasa inaendeshwa kwa njia ya kubebwa na matajiri wakubwa. Hivyo wengi wanaamini upo uwezekano mkubwa kwa matajiri hao kubwaga manyanga na serikali kukosa mishahara ya kulipa wafanyakazi wake. Usahihi wa khofu hii ya wafanyabiashara inapata nguvu ya kilio cha mmoja wa wawakilishi wa uchaguzi wa Machi 20, ambaye alinieleza jinsi wanavyolipwa shilingi milioni mbili badala ya milioni nane wanazostahili kulipwa kama mshahara wao wa kila mwezi. “Kweli hali ni mbaya kiasi cha sisi wawakilishi kulipwa 2,000,000 na nyingine haijulikani tutalipwa lini.”
Hivi karibuni nilimsikia Shein akilizungumza hili kwenye kiriri, nami nikajawa na maswali ambayo nilitamani kumuuliza mbele ya uso wake. Akiwa mmoja wa wa wazee wa nchi hii, nilitaka kumuuliza ikiwa kweli ameshindwa kuiona busara ambayo itaivuusha na kuipeleka mbele Zanzibar. Akiwa mmoja wa wasomi wa nchi hii, nilitaka kumuuliza ikiwa kweli amekubali nchi izame ili tu yeye aendelee kukalia kiti ambacho wananchi walishampoka kwa njia ya kura halali! Akiwa kiongozi ambaye kwa miaka mitano aliionja hasa ladha ya urais wa Zanzibar anayeheshimiwa na hata wale wasiomkubali, nilitaka kumuuliza ilipo ile ladha na ule utamu wa uraisi wake, ikiwa raia wanateseka kwa sababu tu ya uraisi huo!
Akiwa kiongozi aliyewahi kushika nafasi ya makamu wa rais wa ((Jamhuri ya Muungano wa Tanzania)) na hivyo anayejuwa na aliyewahi kushiriki shughuli za kimataifa, nilitaka kumuuliza ilipo raha ya yeye kuitwa rais, ikiwa dunia imempiga pande na sasa haimpi tena misaada ya kuwasaidia raia wake! Na mwisho, nilitamani kumuuliza ana haja gani na uraisi ambao hapewi mashirikiano na raia wake na sasa analazimika kuvitawala visiwa hivi kwa mkono wa chuma!

No comments:

Post a Comment