Monday, December 5, 2016

MAMA FAUZIA WAZANZIBARI WAMEKUSIKIA NA ULIMWENGU PIA UNAKUSIKIA

Afbeeldingsresultaat voor balozi seif ali iddi mgonjwa
Part-1
Assalam Aleykum
Jina langu naitwa Fauzia Abdullah Saif Al Bahry. Mimi ni mjane wa Said Iddi BAVUAI, na nimeishi nae si chini ya miaka thalathini. Nimezaa nae nimejukuu nae, na nimemkalia mpaka EDA. Na mpaka leo naendelea kuwa mjane wa mzee BAVUAI. Ambae jana nimeshtushwa kusikia katika vyombo vya habari tunatangaziwa kwa jina la mdogo wangu Fadya. Na sijui kwa nini wasinitangaze mimi mkubwa wakamtangaza Fadya ambae ni mdogo na sisi tuko watatu Fauzia, Fadya na Firdaus lakini wametumia jina la mtu mmoja kuwa sisi wabadhirifu.
Hii lugha mimi ngeni kwangu kwa hakika siijui na hata sijui nini maana ya ubadhirifu nauliza nini maana ya ubadhirifu ? Sijui. Lakini nimefahamishwa kuwa ni wizi, kwaivo nakataa ile habari ilosema jana ambayo rikodi yake ipo na watu wamerikodi. Mimi nakataa si mwizi, siibi, sitoiba na sijamuibia mtu yeyote shamba la Kazole. Ni haki yetu tumerithi kwa wazee wetu, babaangu Abdallah bin Saif amefariki, Nassor bin Saif amefariki, na ami yangu Hemed bin Saif amefariki, na mali hii yetu. Mali tumerithi kwa wazee wetu.
Babaangu na ami zangu wamerithi kwa baba yao ambae amefariki toka 1930 na makaburi yake yapo pale pale kazole Muembe Amari, makaburi yapo ya mababu na ndugu na wazee walio tangulia mbele ya haki. Sijui ubadhirifu huu nimeufanya kwenye kitu gani ? Kazole ni kwetu kazole nimeishi kazole nimekaa kazole naijua kwetu pakiitwa Muembe Amari. Tena mie mtu wa Kazole jirani yangu Kitope, jirani yangu Mahonda, jirani yangu Matetema. Shamba letu limepakana mpaka njia ya Mbaleni.
Hao walozuka leo wakasema lile ni shamba lao au sisi tumefanya ubadhirifu. Mh kama unataka kuchukua shamba chukua na kama unataka kuvunja kuta vunja lakini nakataa mimi na aila (familia) yangu sio wabadhirifu.
Mimi nimeolewa na mwanamme ambae ni kiongozi katika nchi sikumuona kufanya ubadhirifu, wala hajanifundisha ubadhirifu, wala kwetu sikuuona ubadhirifu. Niliona yeye (mume wangu) akifanya haki wizarani, maofisini, watu, makazini sijasikia yeye akifanya ubadhirifu wa aina yoyote. Yeye akisuluhisha na kutengeneza ndio hii siasa nilio ikuta wakati huo kwa hao waume walotuoa.
Huyo alochukua na kutoa amri ni Mh yuko katika ngazi ya juu na kajitangaza rasmi na maredio yote yanajua, TV pia. Hajasema siri. Zanzibar iniskie na Tanzania iniskie viongozi wa zamani wake zao wana nyanyaswa katika nchi hii. Wamesahau kila kitu.
NB: SALAMU KWA BALOZI MKAAZI
Part-2
Salam kwa balozi mkaazi
Assalam alaykum Muheshimiwa. Ndio, wewe ni Muheshimiwa Saif Ali Iddi, na mimi raia Fauzia Abdullah Saif Al Bahry mjane wa Said Iddi BAVUAI. Kweli Muheshimiwa, Muheshimiwa mwenye nguvu, Muheshimiwa hodari, Muheshimiwa jeuri.
Lakini Muheshimiwa nakwambia hivi, nnavojua mimi nilivokuwa nimekaa na hao waasisi na wanamapinduzi wa nchi hii walivonifundisha kuwa likitokea jambo lolote khitilafu kwenye wilaya, mkoa, na mambo yanokhusu serekali huwa inachaguliwa tume na watu huitwa na kisikilizwa pande zote mbili.
Ikiwa unasema Waarabu wamekuja kuchukua na kuvamia shamba la Kazole, hakuna alokuja kuvamia shamba la Kazole. Shamba la Kazole ni langu mimi Fauzia Abdullah Saif Al Bahry. Umefahamu ?
Na tulijisalimisha baada ya hao waasisi kutaka kutuoa na tukakubali ili kuondoke hizi FITNA za ukabila. Kwahio Muheshimiwa unarejesha UKABILA ambao kaufuta Karume 1964. Wewe unarejesha UKABILA.
Kwahio wewe unakwenda dhidi ya siasa ya Uzanzibari. Kwahio nakwambia hiyo ni haki yangu, nimerithi kwa wazee wangu, sijabadili uraia wangu, ni Mzanzibari, na watoto wangu ni Wazanzibari, na wajukuu zangu ni Wazanzibari.
Muheshimiwa chukua, na vunja kuta, na vunja makaburi, na vunja MSIKITI, na vunja kila kilichokuwemo kwenye shamba kwa ujabari wako, na kwa uhodari wako.
Na mimi Niko tayari kwa maneno haya uje kunichukua na kunifunga, unasikia ? Nifunge Niko tayari lakini tulijisalimisha kwa kukataa hizi bughdha zenu. Tulijisalimisha kwa kukataa hizi chokochoko, na bughdha na ubaguzi wenu, na ndio tukakubali kuolewa na watu kama nyinyi.

No comments:

Post a Comment