SIMO katika wananchi wanaolaumu ubaya wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK). Hapana. Mimi nishatoka hapo, ninavoisema serikali, wewe msomaji ujuwe ninamlaumu Shein kama kiongozi mkuu wa Maskani ya Kisonge.
Kwa hivyo, mwanzo kabisa wa mjadala huu leo, nifahamike namtupia lawama Shein kwa sababu ni Rais wa Maskani ya Kisonge na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyeapa kutumikia nchi ya Zanzibar. Na kwa sababu ninamlaumu. Shein kwa sababu ndiye kiongozi mwenye dhamana kuu ya umma kuiongoza hapa nchini Zanzibar, yenye mchanganyiko wa wananchi, na mchanganyiko wa fikra na misimamo vilevile, basi nawatoa lawamani na shutumani viongozi waliomo Baraza la Mawaziri, wanaotoka Civic United Front (CUF) Chama cha Wananchi. Viongozi wa CUF walioko ndani ya safu ya mawaziri wa Shein, nataasaf kwamba hawahusiki na ujinga mkubwa wa kiuongozi huyu Shein unaofanywa na serikali anayoiongoza.
Ni kweli Shein anaongoza SUK. Lakini kwa mambo yanayofanywa na serikali, si rahisi kuwajumuisha mawaziri aliowateua kutokea CUF. Viongozi hawa hawahusiki kwa kweli na uovu unaodhoofisha umoja wa kitaifa wa nchi ya Zanzibar. Hicho sicho walichoahidi kukitekeleza kwa umma. Waliahidi neema chini ya misingi ya uongozi ulio mwema. CUF haijapata kuahidi ujinga wala upuzii. Haijaahidi watu ukandamizaji na kuuwauwa kisiri siri. Ni CCM wanaostawisha ukandamizaji na kuuwa watu kila wanavyopata nafasi. Hili si jambo la ajabu na uongo. Hili lipo kwenye rekodi wazi. Serikali zao zote mbili, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar au SMZ Wauwaji, zinaua raia, achilia mbali kuwanyima haki zao za msingi. Kuwatesa na kuwadhalilisha.
Kwa sababu hiyo basi, nataka ieleweke vizuri, Shein anaingia lawamani kwa sababu kwa muda mwingi anakaa zaidi na mawaziri wanaotokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Mkoloni Mweusi Tanganyika. CCM ndio chama atokacho yeye. Ni chama hichi kilichomteua Shein agombee urais mwaka 2010. Ni viongozi wa chama hichi waliopanga kwa namna mbalimbali na wapuuzi katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar – Zanzibar Electoral Commission (ZEC) – kupika matokeo ya urais na hatimaye Shein akatangazwa mshindi japokuwa yeye mwenyewe anajuwa kuwa hakushinda na watu wote wanajuwa kuwa hakushinda. Jambo hili lilikuwa likiwahangaisha Wazanzibari wengi kwamba ni kweli ndivo ilivyokuwa pale wakati umma wa wananchi wakisubiri matokeo yatangazwe kupitia hadhara iliyokutanishwa ndani ya ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani.
Mwenyeezi Mungu ameleta kudra yake na kuwatoa hofu wananchi juu ya utata wa matokeo yale yaliyotangazwa na Tume. Amelisema hili kwa uwazi muasisi wa Mapinduzi, Muungano na CCM, mzee Hassan Nassor Moyo – Shein “alitangazwa tuuuuuu rais.” Mzee Moyo, memba wa CCM anayeshika Kadi Na.07 ya uanachama, anasema yeye ndiye aliyeongoza ujumbe wa kwenda kumshawishi Maalim Seif Shariff Hamad akubali matokeo ya kushindwa. Maana yake aliyetangazwa mshindi, hakushinda kweli fatheha juu ya fetheha kwa anaye jinata kuwa ni rais hali anajuwa kuwa sio rais ni kidampa tu kimewekwa. Watu wanakumbuka hali iliyotangulia utangazaji wa matokeo yale yaliyompa ushindi batil Shein. Wanakumbuka umma ulivoshtadi kwenye geti la kuingilia Bwawani. Pale viongozi wakubwa walipopeleka salamu kwa viongozi wa CUF, eti wakawatulize na kuwapa matumaini kuwa hakuna lililoharibika.
Hali ilikuwa mbaya. Ilikuwa mbaya kwa sababu wapigakura waliokusanyika Bwawani, asilimia kubwa walikuwa ni wafuasi wa CUF na wapenda mabadiliko. Walitumaini mgombea wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, atakuwa rais wao. Walikuwa wanayo sababu ya kutumaini hivo. Walizipiga kura nyingi kumuelekea yeye. Waliamini, na bado wanaamini,nawataendelea kuamini kwamba yeye ndiye rais wao. Wanamuamini Maalim Seif kuwa ndiye mwanasiasa anayewafaa kuiongoza nchi yao wanayo ipenda ya Zanzibar. Ukweli huu unajulikana zamani. Maalim mwenyewe alichangia kuchukuliwa mwanasiasa anayeaminika. Alijichunga kiuongozi akijipambanua na viongozi asi kwa wananchi. Alijiweka kiongozi kioo cha jamii katika dhana ya uongozi mwema na mpenda nchi kweli kweli. Ni mtizamo huo aliouchukua, na kuukomaza kwa wananchi alipotoa ahadi kwamba atakuwa pamoja na Wazanzibari, tena wote wa asili ya Unguja na wote wa asili ya Pemba, akiwa ndani au nje ya serikali. Maalim Seif amekuwa akienena na ahadi hii aliyoitoa tangu miaka ya 1980 pale utawala ulipoanza kumfanyia visa asiinuke kiuongozi.
Sasa kwa kuwa wananchi wamempa imani Maalim Seif, wanamuamini kuwa ni kiongozi bora anayependa watu, anayezijali raslimali za nchi hii ya visiwa iliyozungukwa na bahari kubwa ya Hindi kwenye pande zote, kila unapokuja wakati wakaipata nafasi ya kupiga kura ya kuchagua viongozi, wanamtilia yeye. Kwa hili, wala Wazanzibari hawapapasi kalamu. Wao wakiishika tu karatasi ya kura, kwa sababu dhahiri shahir wanajua kitu wanachokitaka, hawababaiki. Wao taratibu wanatia NDIO penye nafasi ya picha ya Maalim Seif. Wao wanashuhudisha imani yao kwake. Wanamchagua. Basi Wazanzibari walio wengi walimchagua Maalim Seif hata siku ile ya uchaguzi mkuu tarehe 31 Oktoba, 2010. Kila mtu anajua hamu ya Wazanzibari, ni mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi yao. Akishakaa pale kiongozi wanayempenda, watatumaini mengi ya kheri kuliko kinyume chake. Wazanzibari wanauhakika Maalim Seif akiongoza nchi, atajitahidi kuondoa shari miongoni mwao. Atajitahidi kushamirisha uongozi mwema, ambao ameuahidi kila wakati wa uchaguzi. Wanaamini atalinda haki zao na kutumia vizuri raslimali zao katika nchi yao.
Wazanzibari wanaamini Maalim Seif ataongoza nchi ya Zanzibar kwa kuzingatia sheria, imani ya dini yake na mapenzi makubwa kwa watu. Atalinda heshma zao, utu wao, ubinaadamu wao, mali zao, aila zao, matumaini yao. Katu haiwapitikii akilini mwao kuwa Maalim Seif amekuwa adui wa Wazanzibari leo. Asilan abadan. Wanamuamini angali anakumbuka fadhila za kuaminiwa. Hawezi kuwa kiongozi mpuuzi asiyejitambua. Huyo si Maalim Seif wanayemfaham. Chini ya uongozi wake Maalim Seif, hakuna mwananchi anayetarajia atakamatwa usiku wa manane nyumbani kwake na kusafirishwa nje yao ya Zanzibar akatungiwe mashitaka. Hili halitatokea kwa sababu mwenyewe anakemea hadharani ujinga huu. Akiwa yeye Rais, Maalim Seif hata mara moja hatarajiwi kuagiza serikali yake ikapambane na bendera ambazo ni vitambaa tu walivyochagua wenye asasi yao iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi yao ya Zanzibar. Leo nchi ya Zanzibar ipo kwenye nakama. Inayo serikali inayopambana na bendera za asasi ya UAMSHO – Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam – ambayo ni taasisi iliyopatiwa usajili wa Sheria ya Usajili wa Vyama/Mashirika ya Hiari ya nchi ya Zanzibar.
Ni hivi: Msaidizi mkuu wa Shein anayeitwa Seif Ali Iddi, ambaye kabla ya jina lake hilo anatangulizwa kwa jina la Balozi – utafikiri ni balozi wa maana sana –kumbe dude debe tupu limo limo tu ametoa amri kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja nchini Zanzibar, asimamie askari wa serikali waondoe bendera zote za Uamsho mkoani kwake. Kwa hivyo, baada ya amri hii, Mkuu wa Mkoa, Juma Kassim Tindwa juha jengine nalo likaanza kutimiza amri msaka tonge, amepita akataka wananchi wote wa mkoani anakoongoza, Kaskazini, waziondoe bendera za jumuiya hii ambayo kwa ukweli hasa wanaoifuata ni watu je kuna ubaya gani...? wanaoongozwa na watu wenye upeo mkubwa katika Uislam na asili zake zote hasa hapo kosa liko wapi....?? Wananchi hawakujali amri hiyo. Kwanza, hawaoni kama ni kosa kisheria mtu kuchomeka bendera ya kitu au chama anachokipenda, cha aina yoyote ile hata kama si chama cha siasa. Pili, hawaoni kama bendera tu inaweza kumkosesha mtu usingizi au amani katika nchi yao. Kwamba eti bendera ile nyeupe yenye maandishi tu ambayo si kwamba yanapinga lolote lile la serikali, imnyime raha Shein, au Makamo wake, Balozi Seif, au mawaziri wa CCM katika serikali ya Shein, au ikinyime raha chama cha mapinduzi ni jambo la jabu kabisa.
Na kama bendera tu ile ya Uamsho inaweza kuwa kero kwa CCM chama cha Mkoloni na viongozi wake hao Wasaka Tonge kwa mpangilio huo au hata akiwa ni Katibu Mkuu wao, Abdulrahman Kinana, au Makamo wao wa huko nchini Tanganyika, Philip Mangula, au hata Mwenyekiti wao, Jakaya Mrisho Kikwete, basi Watanganyika hao wasaka tonge walio nchini Zanzibar basi wana shida kubwa na viongozi wao. Viongozi wanaokasirikia wananchi kwa sababu wamepachika bendera kwenye maeneo yao, lazima waonekane wamefilisika kisiasa. Hao ni viongozi waliochoka kufikiri. Ni viongozi muflis ambao wamejitoa katika kuwa watu wanaowaza ni vipi wataondosha shida tele zinazowakabili wananchi walioapa kuwatumikia. Ni ujinga mtupu viongozi watu wazima kuacha mambo ya maana katika kuwatumikia wananchi, wakatoa matamko na amri kwa wasaidizi wao washughulike na bendera. Hivi bendera ndiyo inayopambana na umasikini...?? Hivi bendera ndiyo inayosaidia serikali kujua kama inapendwa na wananchi wake...?? Hivi bendera ndiyo inayoizuia serikali kuhudumia wananchi kwa elimu, tiba, maji,umeme,nyumba nzuri za kuishi na tuseme kufikia malengo ya milenia..??? Siamini hata kidogo. Bendera haiwezi kuwa jambo la maana sana kwa viongozi wa serikali isipokuwa kama wameishiwa busara kwa kuwa wameshindwa kufikiria njia za kuondoa shida za wananchi basi ndio hubaki kupigana na bendera.
Viongozi hawa ambao ndio maana nikasema mwanzoni kabisa mwa mjadala huu, kwamba simo katika kuamini kuwa mawaziri waliotoka CUF wanaweza kuwa sehemu ya ushetani huu wa kupambana na bendera. Simo mimi. Ujinga huu wa kuituma dola ishughulike na bendera ni wa aina yake ambao watu wenye akili nzuri ya maendeleo ya wanadamu hawawezi kushiriki. Viongozi wa CUF waliomo katika SUK pamoja na Maalim Seif hawawezi kushiriki kuagiza upuuzi kama huo. Shein yeye anaweza. Kwanini asiweze...?? Anaweza kwa sababu anayajua yote yanayofanywa na msaidizi wake mkuu, Balozi Seif, wanayetoka pamoja CCM chama cha Mkoloni Mweusi Tanganyika, chama kinachoshika udhibiti wa uongozi wa nchi ya Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Anajua kwamba serikali yake ndiyo inayohusika kushughulika na bendera, kitambaa, tu cheupe.badala ya kushughulikia hospitali,madawa,barabara,maji,umeme,ajira kwa vijana,kuhimili kodi ya vyakula ili masini nao wale mara tatu na sio mlo moja au hawana kabisa nyumba nzuri za kuishi n.k. Lipo tatizo kubwa katika nchi ya Tanganyika maana sio nchi ya Zanzibar peke yake. CCM chama cha Mkoloni Mweusi Tanganyika ambayo ndiyo inaongoza dola, imechoka sana sana na wala haijuwi tena ni vipi ilete maendeleo kwa wananchi walio wengi tabani bin hoehe. Haina tena nguvu ya kuongoza bali ina nguvu ya kukandamiza rai wake kuuwa rai wake kunyanyasa rai wake na kuendele kujitajirisha wao kwa wao viongozi na kuwasahau kabisa rai wao.
KILA MZANZIBARI ATAULIZWA SIKU YA KIYAMA NA MWENYEZI MUNGU ULIPOSIKIA WAZANZIBARI WENZIO WANADHALILISHWA NA KULAWITIWA NA HAWA JE ULIFANYA NINI TAFUTA JIBU LAKO MAPEMA KWA SIKU HIYO YA KIYAMA SIKU AMBAYO MALI NA WATOTO WAKO WALA CHEO CHAKO HAVITAKUFAA SIKU HIYO.