TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kesho, tarehe 27 Januari, 2016 tutakuwa tunatimiza miaka 15 tokea yalipofanyika mauaji ya kinyama ya watu wasiopungua 65 visiwani Zanzibar waliouliwa na vyombo vya dola wakati maelfu ya wananchi walipofanya maandamano ya amani kudai haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka mwaka 2001. Mamia ya watu wengine walijeruhiwa vibaya na wengine kupoteza viungo hadi leo huku Tanzania kwa mara ya kwanza ikizalisha wakimbizi wa kisiasa wapatao 2,000 waliokimbilia Shimoni, Mombasa, nchini Kenya.
Kila mwaka tumekuwa tukiadhimisha siku hii kwa njia mbali mbali ikiwemo kufanya maandamano, mikutano ya hadhara, visomo vya kuwaombea marehemu na bendera za Chama kupepea nusu mlingoti.
Kwa mwaka huu, Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Wananchi (JUVICUF), waliiandikia Polisi Wilaya ya Mjini Unguja barua rasmi na kutoa taarifa ya kufanya matembezi ya amani yatakayofuatiwa na mkutano wa hadhara. Polisi wamejibu barua kwa kukataza kufanyika matembezi hayo na mkutano huo wa hadhara.
Kutokana na hali ya nchi ilivyo, na hasa kwa kujali usalama wa wananchi, uongozi wa CUF ngazi ya Taifa, umetoa agizo rasmi la Chama kwa Jumuiya ya Vijana wa CUF kuwataka WASIFANYE matembezi hayo na mkutano huo wa hadhara.
Badala yake, uongozi wa Chama Makao Makuu unaagiza kwamba tuadhimishe siku hiyo kwa kupeperusha bendera za Chama nusu mlingoti kwenye ofisi zote za Chama nchi nzima.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO
26 JANUARI, 2016
Mkapa aliyeamrisha mauaji hayo bado yuko hai na yeye bado anaiandama Zanzibar kuhakikisha haipati mamlaka yake kamili. Ni jambo la maana kama yeye angewashitaki Wazanzibari kwa Mungu wake kuliko sisi kwenda kumshitaki. Mkapa usome ujumbe huo vizuri sisi tuna chuki na wewe na kwa sababu hukuomba radhi kwako kisasi ni halali kama lisemavyo bibilia
ReplyDelete