Thursday, July 21, 2016

PART 7 MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD ANAENDELEA NA ZIARA YAKE HUKO NCHINI UHOLANZI








Ziara ya Maalim Seif Sharif Hamad na ujumbe wake hapa nchini Uholanzi (The Netherlands) imeanza vyema leo ikiwa ndiyo siku ya kwanza kuanza kazi kwa kuwa na mikutano miwili mjini The Hague na mmoja mjini Amsterdam.
Saa 4:00 asubuhi Maalim Seif na ujumbe wake walikaribishwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi ambapo walikutana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Paul J.M. Litjens na Ofisa anayeshughulikia Sera kwa eneo la Afrika Mashariki, Bibi Elin Hilwig, ambaye anashughulikia nchi za Tanzania, Mozambique, Madagascar, Mauritius na Comoros.
Mkutano ulikwenda vizuri sana na ulikuwa na maelewano makubwa ambapo Maalim Seif na timu yake walimueleza kwa undani Kaimu Mkurugenzi huyo na maofisa wake nini kilochotokea Oktoba 28, 2015 pale uchaguzi mkuu ulipotangazwa kufutwa na pia matukio yanayoendelea sasa, athari zake na pia kuwasilisha mapendekezo yake ya njia za kuitoa Zanzibar katika mkwamo iliomo sasa.
Maalim Seif pia aliwaeleza wenyeji wake fursa za kunyanyua uchumi wa Zanzibar ambapo kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Uholanzi zinaweza kuwaondolea Wazanzibari umasikini, kuzalisha ajira na kuweza kunyanyua maisha ya watu wake hasa vijana na hivyo kuondosha sababu zinazoweza kuwapelekea kukata tamaa na kutumiwa katika vitendo viovu.
Pichani ni Maalim Seif na ujumbe wake wakiwa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, mjini The Hague pamoja na Bw. Paul J.M. Litjens, Bibi Elin Hilwig na msaidizi wake.

No comments:

Post a Comment