Thursday, July 7, 2016

SHEIN JE MAZOMBI.......??

Shein amesema hakuna serikali ya mpito itakayoundwa Zanzibar baada ya uchaguzi wa marudio uliyofanyika Machi 20, mwaka huu. Tamko hilo alilitoa jana, alipokuwa akihutubia Baraza Eid el Fitri, katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Zanzibar. “Kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, hakuna serikali ya mpito itakayoundwa Zanzibar. Hayo yanayosemwa mitaani ni hadithi, sadiki ukipenda,” alisema Shein. Alisema baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio na CCM kuibuka na ushindi wa asilimia 91.4, hakutakuwa na uchaguzi mwingine hadi mwaka 2020 baada ya serikali ya awamu ya saba kumaliza muda wake. “Uchaguzi umekwisha serikali iliyochaguliwa na wananchi imekwishaundwa na ipo madarakani na imeanza kutekeleza majukumu yake na wajibu wa wananchi kushirikiana na serikali yao katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” alisisitiza Shein.Shein alisema malengo ya kufikia maendeleo Zanzibar yatafikiwa iwapo wananchi wake wataongeza ushirikiano na kuishi kwa amani na kudumisha misingi ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo, alisema kuwa kumeanza kujitokeza ishara na vitendo vya kutaka kuchelewesha maendeleo ya Zanzibar, lakini serikali haitawavumilia watu wanaofanya vitendo hivyo, wakiwamo baadhi ya wanasiasa. “Natoa ilani sitamvumilia mtu yoyote au kikundi chochote kitachojaribu kuchelewesha kwa mbinu yoyote ile, katika kutekeleza majukumu ya serikali na utekelezaji wa ilani yake ya maendeleo kwa wananchi,” alionya Shein. Aidha, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kujiepusha na vitendo vya uchochezi na uvunjifu wa amani na kuonya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa watu wanaojaribu kuzorotesha misingi ya amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake. Alisema viongozi wa siasa hawapaswi kuchochea wafuasi wa vyama vyetu wafanye fujo, wahasimiane, wanuniane na wagomeane kwenye huduma za jamii na dini pamoja na kufanyiana hujuma wakati wao ni wamoja katika jamii. Shein pia alisema mambo mema yaliyotendeka wakati mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, yanahitaji kulelezwa na kutekelezwa wakati wote hata baada ya kumaliza, ikiwemo kupiga vita ubaguzi.Aliwataka viongozi wa kisiasa, dini na taasisi za kijamii, kulinda, kuenzi na kuendeleza amani kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi. Alisisitiza kuwa serikali zote mbili zitaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha amani na usalama vinakuwapo nchini. Katika hatua nyingine, Shein alisisitiza kuwa Zanzibar inaongozwa kwa misingi ya katiba na sheria na hakuna mtu au kikundi cha watu kilicho juu ya sheria na wajibu wa kila mtu ni kuhakikisha hafanyi vitendo vya kuhatarisha amani, kuharibu mali za watu au kutishia maisha ya watu wasiokuwa na hatia. “Wale wote watakaobainika kushiriki katika vitendo vya hujuma na kuhatarisha amani, waelewe kwambasheria itachukua mkondo wake bila kumwonea au kumdhulumu mtu yeyote,” alisema Shein. Pia alisema wanasiasa wana jukumu la kufanya siasa kwa kuzingatia misingi ya katiba na sheria kwa kuafuata maadili ya vyama kwa kushindana bila kudharauliana au kugombana kwa madhumuni ya kuharakisha maendeleo ya nchi. Akizungumzia mpango wa serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017, alisema serikali imeamua kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza matumizi kwa madhumuni kupunguza utegemezi katika utekelezaji wa miradi yake. Kuhusu udhalilishaji na unyanyasaji wa kijisia, Shein alisema juhudi za pamoja zinahitajika kutokana na vitendo hivyo kuendelea kuongezeka, vikiwamo vya ubakaji. Alisema ripoiti zinaonyesha matukio 873 yameripootiwa katika kipindi cha 2015/2016 na kuwataka wananchi kuwa tayari kutoa ushahidi na vyombo vya dola kuongeza nguvu katika kupambana na vitendo hivyo. Pamoja na elimu inayoendelea kutolewa, alisema unyanyasaji bado ni tatizo kubwa, hivyo muhimu wananchi na vyombo vya dola kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha lengo la kukomesha vitendo hivyo.

No comments:

Post a Comment