Thursday, March 1, 2012

UDIKTETA UNAENDELEYA NCHINI ZANZIBAR.MBONA ALIYE UZAA MIPAKA YA BAHARI SHAMHUNA MPAKA LEO HAULIZWI KITU....?HAKUNA GNU WALA SUKARI UNAFIKI MTUPU


Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillahi Jihadi Hassan na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ali Saleh Mwinyikai wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa baraza la wawakilishi la zamani hapo Maisara Mjini Unguja
SERIKALI ya Zanzibar imekiri kuwawaondoa Wahariri wawili wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa madai ya kuwagonganisha vichwa (fitna) Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuumpa muda zaidi Maalim Seif kwenye ZBC TV.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mjini Zanzibar,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari  Utamaduni Utalii na Michezo,  Ali Saleh Mwinyikai alisema wahariri hao waliondolewa katika nyadhifa hizo kwa kukiuka taratibu na mwongozo wa shirika hilo ambapo walionekana watasababisha fitna kwa viongozi hao.
Wahariri walioondolewa ni pamoja na aliyekuwa Mhariri Mkuu, wa Televisheni, Juma Mohammed Salum na Msaidizi wake, Ramadhan Ali ambao wamehamishiwa Idara ya Habari(MAELEZO).
Mwinyikai aliyasema hayo kufuatia masuali ya waandishi wa habari waliotaka kujua nini chanzo cha wahariri hao kuondoshwa katika nyadhifa zao hizo na kuhamishiwa Idara ya Habari Maelezo.
Katika mkutano huo baadhi ya waandishi wa habari walilalamikia hatua zinazochukuliwa na wizara kwa kuwapa adabu wahariri na pia kuwasumbua waandishi wa habari ambao wanafanya kazi zao kwa kufuata maadili.
Aidha walisema dhana ya uhuru wa habari inaonekana haipo kwani serikali imekuwa ikiingiza mkono wake kwa vyombo vya habari na kutoa mfano wa wahariri wa ZBC kuondolewa katika nyadhifa zao kwa madai chombo hicho kinampa nafasi kubwa zaidi Maalim Seif kuliko Dk Shein.
Akifafanua Dk Mwinyikai alisema kuondolewa kwa Juma Mohamed katika wadhifa wa Mhariri Mkuu wa ZBC na Ramadhan Ali katika nafasi zao, Naibu Mhariri Mkuu wa chombo hicho kulisababishwa na utendaji wao kuwagonganisha viongozi hao ambapo Maalim Seif alipewa nafasi kubwa katika hafla kuliko Dk Shein.
“Walioondolewa sio kwa sababu ya kumtangaza zaidi Maalim Seif kuliko Rais Shein, walikwenda kinyume na taratibu na mwongozo wa shirika, zaidi ya habari tatu za Maalim Seif zinapewa dakika tano mfululizo huku za Rais Shein zikipewa dakika moja,” alisema Dk Mwinyikai.
Dk Mwinyikai alisema ZBC haliendeshwi kwa misingi ya itikadi za kisiasa kwa sababu ni mali ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoundwa na vyama viwili vikuu vya siasa vya CCM na CUF kwa mfumo wa kugawana madaraka.
Mkurugenzi Mkuu wa ZBC, Hassan Abdallah Mitawi kwa upande wake alisema kuondolewa kwa wahariri hao katika nafasi hizo ni utaratibu wa kawaida na sio jambo kubwa kwa kuwa wlaikuwa katika kipindi cha kuangaliwa utendaji wao wa kazi.
“Hilo sio jambo kubwa ni utaratibu wa kawaida kuwahamisha watendaji sehemu moja na kuwapeleka sehemu nyengine lakini walikuwa na makosa mengine sio hayo tu” alisema Mitawi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba katika habari ambayo inalalamikiwa kwa siku hiyo, habari kuu katika ZBC Televisheni ilikuwa ni ya Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akimwapisha DPP na Naibu Mufti Mkuu na kuondoka nchini kwenda Uingereza iliyotumia muda wa dakika 3:56.
Habari ya pili kwa uzito ilikuwa ya Makamu wa kwanza wa Rais,Maalim Seif Shariff Hamad akizungumza katika kongamano la jumuiya ya wanawake ya CUF alitumia muda wa dakika 2:42. Habari nyengine ya Rais kwa siku hiyo ilikuwa ni ya upande wa michezo ambayo ndio iliyokuwa habari kuu alizungumza na kamati ya kombe la mapinduzi iliyotumia muda wa dakika 2:32 huku ya CUF ya michezo ikitumia dakika 1:30.
Habari zaidi zinaeleza kuwa taarifa ya habari ya shirika hilo la ZBC TV ni dakika 30 tu.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu Mhariri aliyeondoshwa, Juma Mohamed iwapo alipewa nafasi ya kujitetea kutokana na kadhia hiyo alijibu kwa ufupi kwamba hawajapewa nafasi ya kujitetea bali walihamishwa baada ya kutakiwa kutoa maelezo kwa nini walimpa muda mrefu Maalim Seif na sio Dk Shein.
Hadi sasa utendaji kazi wa serikali unaendelea ambapo vyombo vya vya habari vinatakiwa kuipa uzito taarifa au tukio lolote lililofanywa na Rais wa Zanzibar, akifuatiwa na Makamu wa kwanza na baadae kamamu wa pili na kisha mawaziri jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa sana na wadau wa habari nchini wakisema ifike wakati utaratibu huo uondoshwe kwani kuna mambo na matukio muhimu yanakosa kupewa uzito unaostahiki.
Katika mkutano huo, uliandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Waziri wa wizara hiyo Abdillahi Jihadi Hassan alisema wizara yake imepata mafanikio katika mambo mbali mbali ikiwemo michezo na utamaduni.

No comments:

Post a Comment