Zanzibar na Mauritius — kisa cha nchi mbili katika bahari moja.
Habu tujaribu kuvilinganisha visiwa vya Mauritius na vya kwetu Zanzibar na kuonyesha jinsi Mauritius ilivyotupita kwa maendeleo na kwa sababu gani.
Kwa hakika kilichonihamasisha kufanya hivyo ni mtazamo wa sahibu yangu mmoja wa Sweden mwenye mahusiano makubwa na visiwa vya Bahari Kuu ya Hindi — Comoro, Mauritius, Réunion, Bukini (Madagascar), Shelisheli (Seychelles) na Zanzibar. Kila mwaka huikimbia baridi ya Ulaya na huvizuru baadhi ya visiwa hivyo.
Ana mazoea mengine pia: haimpiti wiki moja au mbili bila kuniletea baruapepe anayoiambatanisha na makala yaliyochapishwa na moja ya magazeti ya visiwa hivyo.
Siku zote makala ayaletayo yanakuwa yanasifu maendeleo fulani katika moja ya nchi hizo au mambo yenye kumfurahisha katika jamii za nchi hizo. Jambo lenye kumkuna kuhusu Comoro, kwa mfano, ni jinsi wananchi wa huko wanavyoishi kwa amani bila ya kubaguana ingawa ni watu wa asili tofauti.
Mara nyingi lakini huwa ananiletea makala yanayohusu maendeleo ya kiuchumi ya visiwa hivyo vya Bahari Kuu ya Hindi isipokuwa Zanzibar. Kwa mfano, mapema mwezi Aprili aliniletea makala yaliyoarifu kwamba uwanja wa ndege wa Roland Garros ulio kisiwani Réunion umeorodheshwa kuwa wanne kwa ubora miongoni mwa viwanja vya ndege vya kimataifa vilivyo katika eneo la Bahari Kuu ya Hindi. Wa tatu ni uwanja wa ndege wa Shelisheli. Uwanja wa ndege wa Mauritius ni wa pili na wa kwanza ni wa Male Ibrahim Nasir ulio kwenye visiwa vya Maldive.
Viwanja bora vya ndege vilitajwa katika sherehe ya Tuzo za Viwanja vya Ndege vya Dunia iliyofanywa Barcelona, Hispania.
Aliponiletea makala hayo huyo sahib yangu alinikumbusha kwamba wakati wa kilele cha msimu wa watalii mashini ya kukagua mizigo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Karume huko Unguja ilikuwa imeharibika kwa muda wa miezi mitatu. Kwa hivyo, mizigo ilibidi ikaguliwe na wafanyakazi wa uwanja wa ndege jambo lililosababisha misururu mirefu ya wasafiri na kucheleweshwa kupanda ndege zao.
Mei 10 aliniletea makala yenye picha ya kituo kimoja cha mabasi huko Victoria, mji mkuu wa Shelisheli. Makala ya gazeti yalisema kwamba Shirika la Usafiri wa Umma la Shelisheli (SPTC) linawaarifu wananchi kuhusu kubadilika kwa mahala pa kuondokea mabasi kulikosababishwa na kazi ya kuezeka mapaa ya kituo hicho hichi ni kimoja cha vituwo walivyojengewa rai ili wasipingwe na mvuwa au juwaa.
seysheli kituo cha basi
Sahibu yangu alinieleza kwamba visiwa vya Shelisheli vilipopata uhuru 1976 taifa hilo lenye wakaazi 90, 000 lilikuwa na magari ya usafiri kama ya Zanzibar yaliyotengenezwa kwa mbao. Mfano wake ni kama yale tuyaitayo magari ya “matwana” au ya “mbavu za mbwa”. Miaka 15 tu baadaye kikajengwa hicho kituo cha kisasa cha mabasi ambacho hufanyiwa ukarabati mara baada ya mara.
Siku hizi badala ya mbavu za mbwa nchi hiyo ina mabasi 300 ya kisasa ikiwa na vyombo vya GPS. Huduma yote hiyo inatolewa na shirika la umma la SPTC. Huko si kama kwetu; hakuna matwana, hakuna mbavu za mbwa, hakuna matatu, hakuna daladala, hakuna bodaboda, hakuna bajaji.
Alichokuwa akinambia hasa ni kwamba wenzetu, majirani zetu katika Bahari Kuu ya Hindi, wanakwenda mbio na sisi hatuna letu jambo ila balaa na bla bla bla nyingi.
Kabla ya kuingia zama za siasa katika miaka ya 1950 Zanzibar ikijivunia kwa mengi licha ya kutawaliwa na Waingereza. Ubora wa maisha na jinsi watu walivyokuwa wakiishi mitaani ni miongoni mwa mengi yaliyowavutia Watanganyika na wengineo waje kuishi nchi kwetu Zanzibar.
Wengi wakiikimbia kodi ya kichwa ambayo wakoloni wakiwatoza Waafrika katika baadhi ya nchi ikiwemo nchi ya Tanganyika. Kodi ya kichwa ilikuwa haitozwi katika nchi yetu ya Zanzibar. Wengine wakija kuchuma karafuu au kijitafutia riziki kwa njia nyingine kama walivyo wafrika wa bara zima wanavyo kwenda nchi za marekani,canada,ulaya na hata uwarabuni kutafuta maisha basi ndivyo ulivyokuwa kwa Watanganyika kukimbilia nchini kwetu Zanzibar kutafuta maisha na mpaka leo bado wanakuja halikuwa sisi wenyewe tumaji hahe hohe.
Jambo moja ambalo watu hulisahau ni kwamba katika siku hizo za neema nchi ya Zanzibar ilikuwa ikifuata sera mahsusi ya kiuchumi. Ilikuwa sera ya bandari huru. Dhana ya bandari huru ni kwamba bidhaa zinazoingizwa nchini huwa hazitozwi ushuru wa forodha.
Bandari Huru ni bandari, eneo la bandari au eneo lolote lile jengine ambalo sheria zake za utozaji kodi wa forodha hulegezwa na serikali inayohusika. Maeneo huru ya kiuchumi nayo pia huitwa bandari huru.
Kuna nchi nyingi zilizojitangaza kuwa ni bandari huru au zilizoyafanya maeneo yao fulani yawe na sifa za bandari huru. Miongoni mwao ni
hii ndio singapore leo iko hivi Zanzibar inanuka
Bahrain,Singapori, China, Misri, Liberia, Uturuki, Urusi, Hispania, Mauritius,Libya, Eritrea, Morocco, Nigeria na Muungano wa Tawala za Kifalme za Kiarabu (UAE).
Aghalabu bandari huru ni eneo mahsusi la forodha ambalo sheria zake za utozaji kodi za forodha hulegezwa sana au kodi za forodha huwa zinafutwa kabisa.
Sera hiyo iliifaa sana nchi yetu ya Zanzibar kwa vile Zanzibar ni visiwa vya wafanyabiashara wenye kusafirisha bidhaa zao nchi za nje na wenye kuingiza bidhaa nyingi kutoka ng’ambo. Visiwa hivi havikubarikiwa madini wala maeneo makubwa ya ardhi kwa kilimo au ufugaji wa wanyama kama walivyobarikiwa ndugu zetu wa Tanganyika wakoloni weusi.
Watanganyika nchi lote hili haliwatoshi tu....??
Kuyadhukuru haya kunanikumbusha Rasimu ya Katiba kwamba ingawa imewatetea wakulima, wafugaji na wavuvi lakini haikuwatetea ipasavyo wafanyabiashara ambao ni kiungo muhimu katika uti wa mgongo wa shughuli za kiuchumi za nchi yetu ya Zanzibar.
Nadhani wajumbe wa Zanzibar iwapo watarudi katika Bunge la Katiba litapokutana tena Agosti, wanapaswa wahakikishe kwamba vifungu maalumu vinaingizwa katika Rasimu ya Katiba vitavyovifanya visiwa vya Unguja na Pemba viwe ni bandari huru na bandari zisizotoza ushuru ili nasi tuwe na maendeleo.
Vikiwa na sifa hizo Visiwa hivyo vitaweza kuvutia uwekezaji na rasilimali kutoka nje, vitaanzisha ajira mpya na vitawapa wananchi fursa za ajira. Lengo ni kuvifanya visiwa vya Unguja na Pemba ving’are, viwe mfano wa kuigwa katika kanda hii ya Afrika kwa maendeleo yao.
pemba hiyoo
Zanzibar haitotendewa haki endapo Rasimu ya Katiba haitokuwa na vifungu hivyo. Kwa kutokuwa na vifungu hivyo kunaweza kumaanisha kuwa Rasimu ya Katiba itayazingatia maslahi ya wakulima, wafugaji na wavuvi wa Tanganyika peke yao. Kufanya hivyo itakuwa ni kuziendeleza sera za Muungano ambazo zimezoea kuyapuuza maslahi ya nchi ya Zanzibar na kudidimiza nchi yetu isipige hatuwa.
Kuna swali moja ambalo sahibu wangu wa Sweden heshi kuniuliza: kwa nini Zanzibar si mwanachama wa ile jumuiya ya Mataifa ya Visiwa Vidogo Vyenye Kuendelea (Sids)? Mwaka huu alichagiza kuniuliza swali hilo kwa sababu huu ni Mwaka wa Kimataifa wa Sids. Jibu la swali lake bila ya shaka ni kuwa Zanzibar haiwezi kuwa miongoni mwa Sids kwa sababu Serikali ya Muungano haitoiruhusu wakolini weusi Tanganyika.
Mataifa haya ya Sids yalitambuliwa na Mkutano Mkuu wa Ardhi uliofanywa Rio 1992 kuwa ni kundi tofauti la nchi zenye kukabiliwa na vitisho vinavyofanana vya kijamii, kimazingira na vya kiuchumi. Kwa sababu hizo za kimazingira na kimaendeleo nchi hizo zinaonekana kuwa ni zenye kustahili kupewa umuhimu maalumu.
Tangu 1992 nchi za Sids zimekuwa zikishirikiana kuhakikisha kwamba kunapatikana maendeleo endelevu duniani ili mahitaji ya vizazi vijavyo nayo yakidhiwe. Zanzibar ni nchi pekee iliyo katika Bahari Kuu ya Hindi ambayo si mwanachama wa jumuiya hiyo na inayokosa faida zake.
Hii leo nchi ya Zanzibar inahitaji kila msaada inaoweza kuupata ili kuunyanyua uchumi wake. Lakini kubwa linalohitajika ni mageuzi ya kimsingi katika uendeshaji wa serikali na namna viongozi wetu wanavyofikiri na wanavyozipanga na kuzitekeleza sera zao.
Wazanzibari wanatamani nchi yao izipate tena sifa zake za zamani za kuwa kituo cha ubora na bandari huru. Yote hayo mawili yanawezekana lakini lazima kwanza pawepo mageuzi makubwa.
Kweli nchi ya Zanzibar imeanza kupiga hatua katika miaka ya karibuni ukilinganisha na awamu za mwanzo tangu Mapinduzi ya 1964. Siku hizi, kwa mfano, watu wana uhuru wa kusema na wa kukusanyika (ingawa kuna nyakati ambapo wanabanwa banwa).
Hata hivyo, haionyeshi kama Serikali inakisikiliza kilio chao cha kutaka pawepo mageuzi makubwa. Kinachotia moyo ni ile imani waliyo nayo wananchi kwamba siku za nchi ya Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili haziko mbali.
No comments:
Post a Comment