Dar es Salaam nchini Tanganyika. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema hakuna jambo lolote litakalomfanya amkumbuke Rais Jakaya Kikwete wa nchi yao ya Tanganyika baada ya uongozi wake mwakani, akisema anachofanya sasa kiongozi huyo ni kuzindua miradi iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tatu.
“Sina la kumkumbuka Kikwete,” alisema Dk Slaa katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika makao makuu ya Chadema, kabla ya kuorodhesha mlolongo wa matatizo yaliyoibuka katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne kuelezea sababu za kutomkumbuka kiongozi huyo wa nchi.
“Kipindi anaingia madarakani alikuwa na kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanganyika, Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya, lakini leo mmemsikia anaizungumza kauli hiyo..??? Yeye mwenyewe ameikimbia, sasa unataka nimsifu kwa lipi,” alisema Dk Slaa baada ya kuulizwa kama kuna jambo ambalo linaweza kumfanya amkumbuke Rais Kikwete katika kipindi chake kinachokaribia miaka 10 akiwa Ikulu.
Dk Slaa, aliyegombea urais wa nchi ya Tanganyika pamoja na Rais Kikwete mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, alifafanua kuwa tangu rais huyo aingie madarakani mwaka 2005 hajafanya kitu chochote kitakachomfanya amkumbuke, zaidi ya kuwasababishia Watanganyika maumivu kwa ugumu wa maisha na kuanzisha miradi isiyokuwa na tija. “Elimu inaanguka, tunaweka rekodi ya dunia nzima kwa watoto 5,000 kumaliza shule wakiwa hawajui kusoma na kuandika; wananchi wanakula mlo mmoja; huduma za afya bado ni duni; maji nayo ni tatizo halafu nimsifu Kikwete, kwa lipi hasa...??
“Hata barabara anazozindua ni miradi ya muda mrefu ya Serikali ambayo chama chochote kikiingia madarakani ni lazima kiitekeleze. Mimi nimekuwa bungeni kwa miaka 15, sasa nawaeleza miradi hiyo ambayo leo Kikwete anaizindua na kujisifu ni mwendelezo wa mipango aliyoiacha (Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa,” alisema Dk Slaa.
Wakati wa kampeni za urais za mwaka 2005, Kikwete alijinadi kwa kaulimbiu ya Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya sambamba na Maisha Bora kwa Kila Mtanganyika na kushinda kwa kishindo na baadaye aliongeza neno ‘zaidi’ kwenye kampeni za mwaka 2010 huku akiibuka na miradi kama Kilimo Kwanza na sasa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),
“Kikwete ameanzisha miradi mingi, ikiwamo Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini haina jipya linaloweza kubadili maisha ya Watanzania,” alisema Dk Slaa ambaye aliacha kugombea ubunge mwaka 2010 ili awanie urais kwa tiketi ya Chadema.
Katibu mkuu huyo alipinga kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani aliyeshauri Bunge Maalumu la Katiba liahirishe mjadala wa muundo wa serikali hadi baadaye, akisema kutokufanya hivyo ni sawa na kujenga nyumba bila msingi.
“Nimeshangaa kidogo Jaji Bomani akisema tusijadili muundo wa Muungano. Huwezi kwenda kujadili haki za binadamu wakati haki hizo hujui zitatolewa na nani; huwezi kujadili afya, maji, elimu, matatizo ya wafugaji na wavuvi wakati hujui mambo hayo yatatolewa na nani. Ni lazima sura ya kwanza na sita zikajadiliwa kwanza.
“Wakati unajadili muundo wa serikali ambao ndiyo utatumika kutoa huduma muhimu kwa wananchi, ni lazima kwanza ukubaliane na sura hizo ndipo uanze vipengele vingine vilivyopo katika Rasimu ya Katiba,” alisema Dk Slaa.
Aliongeza: “Sisi Ukawa tuko tayari hata usiku wa manane kurudi bungeni, lakini tukihakikishiwa kwamba maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu hiyo yataheshimika, tofauti na hivyo hatutarudi bungeni.”
Kauli hiyo ilikuwa inajibu hoja za Jaji Bomani alizozitoa alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, alilishauri Bunge Maalumu la Katiba kuweka kando suala la muundo wa Serikali kwa kuwa ndiyo chanzo cha mgawanyiko baina ya wajumbe.
Pia aliwashauri wajumbe wa kundi la Ukawa linaloundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kurejea bungeni ili mchakato huo uweze kuendelea.
Alisema suala la muundo wa Serikali licha ya kusababisha mgawanyiko limesababisha hoja nyingine muhimu kusahaulika.
Maandamano hayaepukiki
Alisema akiwa Katibu Mkuu wa Chadema anafurahishwa jinsi anavyoona kwamba Watanganyika sasa wamefunguka wanajua haki zao, njia ya kuzidai, pia kuzipigania.
“Kwa hali hii uhuru unakaribia kufika wakati wake, kiongozi yeyote anafurahia kuona fikra na tabia za wananchi zikiimarika. Kwa hali hii ukiona vinaelea, ujue vimeundwa.
“Hayo hayakuja hivi hivi. Ilifanyika kazi kubwa kwani watu walipigwa, walipoteza mali zao, walipigwa mabomu, wamefilisika na wengine wamepoteza maisha yao. Hivyo leo hii maandamano yamekuwa sumu kwa wabunge na viongozi wa CCM kutokana na uzito wake.
“Leo hii nawashukuru Watanganyika kwani maandamano yamefanikiwa na lengo lilikuwa kuionyesha Serikali kwamba tunaungwa mkono na wananchi, lakini wabunge wengi wa CCM hawayapendi, ndiyo maana wanayapinga kwa nguvu nyingi bungeni,” alisema Dk Slaa wakati akijibu swali aliloulizwa ni kitu gani ambacho anakifurahia katika uongozi wake wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment