SIKU moja mwanasiasa mmoja wa Uganda aliyekuwa akiishi London alikuwa amejimwaga kwenye sofa sebuleni mwake akipiga soga na shemeji yake huku akiangua vicheko na kujifaragua.
Mara simu ikalia; akanyosha mkono kuichukuwa kwenye meza iliyokuwa pembezoni mwa sofa. Alipoisikia sauti ya aliyepiga simu ghafla akanyanyuka, simu mkononi, akasimama kwa ukakamavu.
Akaanza kutetemeka akimwitikia mpiga simu kwa heshima na taadhima utadhani aliyepiga simu alikuwa mbele yake, ilhali alikuwa kilomita elfu sita ushey kutoka sebuleni mwake.
Alifanya aliyoyafanya kwa sababu sauti ya mpiga simu ilimtisha. Ilimtia woga. Kiasi imtishe kwani ilikuwa ya Rais wa siku hizo wa Uganda, Jenerali Idi Amin Dada aliyejibandika cheo cha U-Field Marshal (Jemadari Mkuu) na vyeo vingine vya ajabu ajabu kama kile cha ‘Mshindi wa Milki ya Uingereza’.
Mkasa huo nilihadithiwa na shemejiye huyo mwanasiasa. Ingawa mwanasiasa mwenyewe ni rafiki yangu wa miaka mingi sikuthubutu kumuuliza iwapo kadhia hiyo ilikuwa ya kweli au ya kubuni. Sikutaka, na hadi sasa sitaki, kumtahayarisha.
Mwanasiasa huyo alikuwa mfuasi mkubwa wa Milton Obote ambaye Idi Amin alimpindua. Amin alikuwa ni hasimu yao na wakila njama za kutaka kumbwaga. Ndiyo maana nikashangaa nilipohadithiwa namna alivyoipokea simu ya Idi Amin huku akiwa anamtetemekea.
Amin alikuwa dikteta aliyekuwa nayo hiyo sifa ya kupenda kutetemekewa. Kuna baadhi ya madikteta wenye kutaka hata picha zao ziwe zinaenziwa na kutetemekewa. Mtu anaweza akakamatwa na kupandishwa mahakamani kwa kosa la kuiharibu au kutoiheshimu picha ya Rais.
Hiyo ni moja ya sababu zinazowafanya mawaziri wawe wanashindana kuweka mapicha ya viongozi wao ofisini mwao na majumbani mwao. Si ajabu ikiwa kuna wenye kuzipigia saluti picha hizo.
Hufanya hivyo si kwa kutaka lakini kwa sababu ya woga kwani woga ukidekezwa unaweza ukamfanya mtu mwenye akili zake afanye mambo yasiyoingia akilini.
Madikteta wengine hujipa majina yenye kutisha. Mfano ni wa Marais wa Syria baba na mwana, Hafez na Bashar Al Assad. Babu wa Hafez alikuwa pandikizi la mtu aliyekuwa na miguvu hata watu wakawa wanamwita kwa jina la Al Wahhish yaani “Mnyama Mwitu”.
Inaonyesha kwamba alilipenda jina hilo la utani kwani alikuwa akilitumia kuwa ndilo jina rasmi la ukoo wake mpaka babake Hafez alipoligeuza. Badala ya kulitumia jina la Al Wahhish akawa anatumia jina la Al Assad yaani “Simba”. Na simba ni simba, lazima aogopwe.
Madikteta hupendelea sana kutumia maguvu na vitisho. Na kila wakati hukumbusha kwamba watayang’ang’ania madaraka. Mfano mzuri ni wa Mohammed Siyad Barre, Rais wa mwisho wa Somalia kabla ya nchi hiyo kusambaratika.
Alipokuwa Rais alikuwa hachoki kukumbusha kwamba aliposhika madaraka mji wa Mogadishu ulikuwa na barabara moja tu iliyojengwa na Wataliana.
“Mkijaribu kunilazimisha nijiuzulu, nitauacha mji huu kama nilivyoukuta. Nimenyakua madaraka kwa bunduki; na ni bunduki tu itayoniondosha,” akisema Barre. Alichokusudia ni kwamba alikuwa radhi kuutwanga mji mzima wa Mogadishu kwa mabomu na kuufanya urejelee hali yake ya zamani.
Jingine alilokusudia ni kwamba ni bunduki tu itayomg’oa madarakani. Na hayo ndiyo yaliyotokea Januari 26, 1991.
Madikteta na watawala wa mabavu, kwa jumla, mambo yao huwa yanafananafanana. Matamshi hayo ya Siyad Barre, kwa mfano, yanalingana na yaliyotamkwa na mjumbe mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka Zanzibar katika Bunge Maalumu la Katiba aliyesema kwamba kwao Zanzibar serikali ya CCM katu haitobadilishwa kwa karatasi (yaani kwa upigaji wa kura).
Siyad Barre pia alikuwa na mambo mawili matatu yaliyofanana na yale ya dikteta Adolf Hitler wa Ujerumani. La kwanza ni sharubu; Siyad Barre akipenda kuweka sharubu kama zile za Hitler.
La pili, kama Hitler alikuwa na umahiri wa kuhutubu na uhodari wa balagha. Siyad Barre akiweza kuhutubu kwa muda wa saa nyingi, akiwapumbaza wasikilizaji wake wasibanduke walipo.
Dikteta akijuwa namna ya kuitumia lugha. Nimeambiwa kwamba siku zote hotuba zake zilikuwa za kutungwa papo kwa papo.
Alikuwa haziandiki kabla ya kuzitoa na wala hakuwa akizitayarisha na mapema. Lakini akijuwa namna ya kuzungumza na ndiyo maana alikuwa akiwavutia maelfu ya Wasomali wenzake.
Pengine haikuwa sadfa kwamba utotoni mwake alipokuwa akichunga mbuzi na ng’ombe akiitwa kwa utani “Afweyne”, yaani “Domo kubwa”. Jina hilo lilimganda mpaka kufa kwake ijapokuwa vibaraka waliokuwa wakijipendekeza kwake walijaribu kumbandika majina mengine yenye heshima kama vile “Baba wa Hekima” au “Jalle Siyad” (Comrade Siyad).
Japokuwa kiwango chake cha elimu kilikuwa cha chini Siyad Barre alikuwa mtu mwenye akili. Na mwenyewe akijiona kuwa ni mwenye akili sana kiasi cha kuwafikiria Wasomali wenzake wote kuwa ni wendawazimu.
Ndiyo maana siku moja alisema: “Kinyume na wanavyofikiri watu wengi mimi si Rais wa taifa. Mimi ni mkurugenzi wa hospitali ya wendawazimu.”
Kwa kuyasema hayo akimaanisha kwamba Somalia ni hospitali ya wendawazimu na Wasomali ndio wendawazimu wenyewe. Yeye, akiwa pekee mwenye akili, ndiye aliyekuwa akiwasimamia na kuwashughulikia.
Hivyo ndivyo walivyo madikteta. Wanajiona watakavyo. Na mara nyingi huwaona wananchi wenzao kuwa ni wendawazimu au mende au watoto. Rais wa zamani wa Kenya, Daniel arap Moi, akipenda kusema kuwa Wakenya wote ni watoto wake, hata ajuza waliokuwa wamempita kwa umri. Yeye ndiye aliyekuwa baba yao.
Siyad Barre alikuwa mtu wa vituko. Akipenda, kwa mfano, kufanya mikutano ya usiku wa manane na mawaziri wake na mabalozi wa nchi za nje. Alikuwa na andasa za kuwaita wende Villa Somalia, Ikulu ya Mogadishu, ambako akiwaweka macho usiku kucha kwa mikutano isiyokuwa na kichwa wala miguu.
Hakuna aliyekuwa akimweza Barre ingawa kuna wasemao kwamba akisuguliwa roho na mkewe mkubwa, Mama Khadija Maallin.
Udikteta wa Siyad Barre ulisababisha mengi yaliyo maovu huko Somalia. Athari zake ziko bayana hadi leo ambapo inaonyesha magaidi wa Al Shabaab wameazimia kuwalenga wabunge pamoja na jengo la bunge.
Serikali ya Somalia inasisitiza kwamba imeidhibiti hali ya mambo Mogadishu na kwamba kwa msaada wa majeshi ya Muungano wa Afrika imewashinda nguvu magaidi wa Al Shabaab. Lakini matukio ya hivi karibuni yanaonyesha hali nyingine. Yanaonyesha kwamba mji wa Mogadishu haukutulia asilani.
Mji huo umekaa kama ulioingia wazimu. Haujijui haujitambui. Na ukenda kuuzuru huenda ukakufanya nawe uingiwe na kichaa. Hujui ukalale hoteli gani; hujui ukatarazaki wapi.
Hujui bomu litaripuka wakati gani; hujui washambulizi waliojitolea mhanga watashambulia wakiwa wamepanda motokaa au wamepanda punda. Ilimradi unakuwa na wasiwasi moto mmoja.
Ukaidi wa Siyad Barre wa kung’ang’ania madaraka ndio chanzo cha hii hali ya sasa ya Somalia. Mtawala huyo aliifisidi Somalia akiifanya kama milki yake binafsi pamoja na jamaa zake.
Wanawe walikuwa na vyeo vya juu katika serikali: Maslah, mtoto wake wa kiume, alikuwa Katibu Mkuu wa Serikali;Ayanle alikuwa Mkuu wa Utawala katika Ofisi ya Rais; Abdullahi alikuwa naibu waziri wa afya; Hassan alikuwa Msimamizi wa kikosi kimoja cha kijeshi mjini Mogadishu.
Mtoto wake mwiengine wa kiume Dirrie alikuwa Mshauri wa Rais kuhusu mambo ya fedha.
Siyad Barre aliwapachika pia mabinti zake katika uongozi wa serikali: Hawa alikuwa Waziri wa Utalii na Maendeleo na Anab alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Bajeti ya Taifa.
Jamaa zake wengine waliokuwa na vyeo vikubwa ni pamoja na nduguye, Abdirahman Jama, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje,na wakweze watatu: Ahmed Suleiman Abdulle alimpa uwaziri wa Mambo ya Ndani na uenyekiti wa kamati ya usalama; Abdirahman Hassan alikuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi na Mohamed Said ‘Morgan’ alikuwa waziri mdogo wa ulinzi.
Inasemekana kwamba mkewe Mama Khadija Maallin alikuwa Mkurugenzi wa Hangash, Idara ya Ujasusi wa Kijeshi.
Hivyo ndivyo madikteta wetu wapendavyo kufanya, kuzifisidi nchi zetu. Uroho wao huwafanya viongozi wengine watamani nao wawe madikteta ijapokuwa wenyewe wanajitambua kwamba ni dhaifu kwa kila hali. Ndipo wanapoanza kutoa vitisho kutaka watu wawaogope.
Na wanapoona kuwa watu hawatishiki tena huanza kupanga njama hata ikiwa zitasababisha vifo. Ngoma, tunaambiwa, hailazwi basi wacha niwape niliyonong’onezwa Jumamosi.
Nasikia katika kikao kimoja cha ndani cha viongozi wa CCM/Zanzibar hivi majuzi mmoja wao (jina ninalihifadhi) alisimama na kwa hamasa akasema: “Lazima tushinde uchaguzi wa 2015 hata kama tutaua.”
Ni matamshi yaliyowashtua wengi kwenye kikao hicho. Bahati nzuri ingawa aliyeyatamka ni kiongozi mzito alikemewa vikali. Kuna aliyekuwa na busara, uzalendo na ujasiri aliyemuuliza atawaua kina nani? Kimya kikatanda katika ukumbi wa mkutano.
Huyo kiongozi mzito alikuwa na hisia zile zile kama za Siyad Barre za ukaidi wa kung’ang’ania madaraka kinyume cha matakwa ya wananchi. Anatamani awe dikteta kama Siyad Barre au Idi Amin. Anataka wenzake waliokuwa wakimsikiliza wamuone yuko imara na ni mtu kuogopwa.
Roho za watu hazina maana kwake. Yenye maana ni roho ya chama chake na jinsi uhai wa chama hicho utavyomnufaisha yeye na wenzake. Potelea mbali nchi ife, potelea mbali watu wafe.
Kiongozi huyu mzito na aukumbuke mwisho wa Siyad Barre. Haukuwa mwema kwake, kwa wenzake na wala kwa nchi yake ambayo kila uchao inaendelea kusononeka.
No comments:
Post a Comment