Serikali ya Saudi Arabia imesema inakusudia kukuza ushirikiano wake na Zanzibar sambamba na kuongeza misaada yake hasa katika Nyanja za taaluma.Mshauri wa Mfalme wa Saudi Arabia Sheikh Abdallah Omar Nasif ameeleza hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni.
Sheikh Nasif amesema Saudi Arabia na Zanzibar zina uhusiano wa kindugu wa muda mrefu, na kwamba hata tamaduni zao zinafanana, hivyo kuna kila sababu ya kukuza uhusiano huo.Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amekaribisha ujio wa kiongozi huyo, na kwamba kitendo hicho kitakuza mashirikiano baina ya pande hizo mbili.Ameiomba Saudi Arabia kuangalia uwezekano wa kusaidia shughuli za madrasa, ikizingatiwa kuwa madrasa nyingi hazina mazingira mazuri ya kusomea.
Kiongozi huyo ameambatana na ujumbe wa serikali na dini ya kiislamu wakiwemo Waziri wa Katiba Mhe. Abubakar Khamis Bakari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej, Mufti Mkuu Sheikh Saleh Omar Kabi na Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji.
Wakati huo huo Maalim Seif amewataka wafanyakazi kuendeleza nidhamu na ushirikiano katika sehemu zao za kazi ili kuongeza ufanisi.Ameeleza hayo katika hafla fupi ya kuwaaga na kuwazawadia wastaafu watano wa ofisi yake, hafla iliyofanyika ofisini kwake Migombani.
Amewataka wafanyakazi wengine wa ofisni kufuata nyayo za wenzao waliostaafu, ili nao waweze kufanya kazi vizuri hadi kustaafu kwao.Mapema akizungumza kwa niaba ya wastaafu wenzake, muhasibu mkuu mstaafu wa ofis hiyo bwana Duchi Mussa, amesema siri kubwa ya mafanikio yao ni mashirikiano pamoja na mashauriano kutoka kwa wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment