Monday, September 23, 2013

NCHINI TANGANYIKA HAKUKALIKI FAMILIA YAUWAWA NA KITOTO KICHANGA PIA

mauaji
Mwanza. Familia ya watu watatu akiwamo baba, mama na mtoto wa miezi saba, wameuawa kikatili usiku wa kuamkia jana Kata ya Buhongwa, Kijiji cha Ihila,Wilaya ya Nyamagana, mkoani huko nchini Tanganyika.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia miili ya marehemu hao ikiwa sakafuni, huku imetapaaka damu. Hadi sasa haijafahamika sababu ya watu hao kuuawa.
Waliouawa ni Jonas Luhinga, Rusia Jonas na mtoto Eliud Jonas.
Akisimulia tukio hilo, mtoto wa marehemu, Debora Jonas (12), alisema tofauti na baba, mama yake na mdogo wake ambao wameuawa, kulikuwa na mgeni nyumbani kwao kwa muda siku tatu ambaye asubuhi ya tukio alitoweka.
Debora alisem saa 10:00 usiku, akiwa amelala na mdogo wake ghafla alianza kulia sana na kumbembeleza, baada ya muda mgeni huyo aliingia chumbani kwake na kumwomba mtoto huyo ili ampeleke chumbani kwa mama yake.
Alisema alimpatia mtoto huyo na yeye kulala mpaka asubuhi na kwamba, aliamka kwenda kufungua mlango wa chumbani kwake na kukuta umefungwa kwa nje ndipo alipoanza kuomba msaada kwa kupiga kelele na majirani walikwenda kufungulia.
“Nilipofika mlangoni nilijaribu kuufungua bila mafanikio, baadaye niligundua umefungwa kwa nje,” alisema Debora.
Alisema baada ya kufunguliwa aliona maiti ya baba yake ikiwa sebuleni, huku ikiwa imechinjwa na alikimbia chumbani kwa mama yake na alimkuta amekufa na mdogo wake huyo wa miezi saba.
Pia, tukio hilo lilishuhudiwa na majirani waliokwenda kumfungulia mlango.
Debora alisema alikimbia chumbani kwa wazazi wake moja kwa moja akiwa na majirani hao na kukuta miili ya mama na mdogo wake ikiwa chini, hakukuwa na damu bali waliona kamba ikiwa pembeni yao na kuhisi huenda ndiyo ilitumika kumnyongea mama na mtoto wake.
Kuhusu mgeni ambaye alikaa nyumbani kwao kwa siku tatu, alisema alikuwa hamfahamu zaidi ya kumtambua kwa jina moja la Lameck na kwamba, muda mwingi alikuwa akimwona anaongea na baba yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Erenst Mangu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, polisi wanafuatilia waliohusika na mauaji hayo.
Akizungumza eneo la tukio, Ofisa Upelelezi Makosa ya Jina Mkoa Mwanza, Joseph Konyo, alisema waliouawa ni familia ya Jonas Luhinga.
Konyo alisema ni mapema kwa polisi kuzungumzia mauaji hayo kwamba, watakapokuwa tayari watatoa taarifa.
Baadhi ya wananchi walisema hivi sasa upokeaji wa wageni unatakiwa kuratibiwa kama ilivyokuwa zamani, mwenyeji akitakiwa kutoa taarifa kwa mjumbe wa nyumba kumi.
Walidai inawezekana mgeni huyo akawa amehusika na muda aliokaa hapo alikuwa anasoma mazingira ya nyumbani.
Pia, walitaka ulinzi shirikishi kuimarishwa kwa sababu inawezekana wakati mauaji hayo yalipokuwa yanafanyika, kungekuwa na doria ingeweza kusaidia. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakipinga kushiriki ulinzi shirikishi, huku wakidai kazi hiyo inatakiwa kufanywa na polisi.

No comments:

Post a Comment