Thursday, November 7, 2013

NCHINI TANGANYIKA KWAJENGWA BANDARI MPYA BAGAMOYO, DOLA BILLIONI 1.2 KWA JILI YA UPANUZI WA MAGATI SABA BANDARI YA DAR


Ufanisi katika ukusanyaji wa mapato huenda ukaongezeka Bandari ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanganyika baada ya Kampuni ya Uingereza kuahidi kutoa zaidi ya Dola 1 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa magati saba.
Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Justine Greening, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba alisema upanuzi huo utaleta ufanisi katika shughuli za bandari, kukuza biashara na mapato.
Tizeba alisema Kampuni ya Trade Mark East Africa, ndiyo itashughulikia upanuzi huo na kuwa muda sahihi wa kuanza mradi bado haujawekwa wazi kwa kuwa upo katika hatua za mwanzo.
“Ushirikiano huu una manufaa makubwa na sisi tunatarajia upanuzi wa bandari utakuwa wa mafanikio makubwa kiuchumi. Taifa litanufaika kimapato na ushirikiano wetu na Uingereza utaongezeka pia,” alisema Tizeba.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari za nchi ya Tanganyika (TPA), Injinia Madeni Kipande alisema bandari hiyo kwa sasa ina uwezo mdogo wa kuingiza na kutoa mizigo kutokana na kulemewa, hivyo upanuzi huo utaleta mabadiliko makubwa kiutendaji.
Alisema Kampuni ya TMEA bado inafanya upembuzi yakinifu ili kupata gharama halisi za mradi wa upanuzi wa bandari ingawa gharama zinazotarajiwa ni kiasi cha Dola 1.2 bilioni.
Injinia Kipande alisema baada ya upanuzi huo, bandari itaweza kupokea meli kubwa kutoka nchi mbalimbali.
Pia alisema meli hazitakaa kwa muda mrefu bandarini na badala yake uingizwaji na utolewaji wa mizigo utakuwa wa kasi.
“Changamoto kubwa hapa ni wingi wa meli ambazo bandari yetu haiwezi kuzifanyia kazi. Ingekuwa tuna gati nyingi ufanisi ungekuwa mkubwa zaidi na mapato yangeongezeka,” alisema Kipande.
Kwa sasa bandari hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo msongamano wa mizigo tatizo ambalo linatajwa kuchangiwa na ukosefu wa ushirikiano baina ya watendaji wakuu.
Pia imeelezwa kuwa ucheleweshwaji wa mizigo bandarini ni kiasi cha asilimia 67 jambo ambalo linatajwa kuchangia kushuka kwa mapato na ufanisi.
Changamoto nyingine inayotajwa kushusha ufanisi katika bandari hiyo ni miundombinu chakavu ambayo inasababisha kupungua kwa idadi ya mizigo kwa kiasi cha asilimia 87 kutoka nchi jirani zinazotumia bandari hiyo kama Zambia, Uganda na Zimbabwe.
Hata hivyo, TPA inatarajia kuongeza kiwango cha uingizaji na utoaji wa mizigo hadi kufikia tani milioni tano ifikapo mwaka 2015, kuimarisha ulinzi na usalama na kuwa kitovu kikuu cha utoaji wa mizigo Afrika Mashariki na Kati.

No comments:

Post a Comment