Wafuasi wa CUF wakiingia Donge na kubeba ujumbe wa kumkaribisha Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad.
Wafuasi wa CUF wakiwa wakibeba ujumbe mzito katika eneo la Donge.
Vijana wa CUF Donge, wakighani utenzi katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Muwanda Donge.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Muwanda Jimbo la Donge.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akipandisha bendera katika moja ya matawi mapya ya chama hicho katika eneo la Donge.
Wafuasi wa CUF wakiwa tayari kumsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi kadi kwa mmoja wa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho katika Jimbo la Donge.
Picha na Salmin Said, OMKR
Na Hassan Hamad, OMKR
Hatimaye Chama Cha Wananchi (CUF) kimeingia katika kijiji cha Donge kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Muwanda na kuhutubiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad.
Maelfu ya wafuasi wa Chama hicho kutoka maeneo mbali mbali ya Mjini na Vijijini walijitokeza katika mkutano huo ili kushuhudia kile kilichokosekana kwa muda mrefu kuingia katika eneo hilo la Donge kwa ajili ya Mkutano wa hadhara.
Akizungumza katika mkutano huo, Maalim Seif amesema anajisikia fahari kuzungumza na wananchi wa Donge katika eneo la ndani la jimbo hilo.
Amesema Donge ni kijiji chenye historia ndefu na ambacho kimejipatia umaarufu mkubwa Zanzibar baada ya kutoa wanazuoni kadhaa, pamoja na kutajwa kwao kushiriki kikamilifu katika Mapinduzi ya mwaka 1964.
Kuhusu mamlaka kamili amesema suala hilo limeanza kudaiwa tangu wakati wa marehemu mzee Karume, na kwamba wanaobeza kudai mamlaka ya Zanzibar wanabeza kauli za Mzee Karume ambapo katika mkutano huo pia iliwekwa sauti ya Mzee Karume alipokuwa akitaja malengo ya Mapinduzi.
Maalim Seif aliingia Donge mapema asubuhi ambapo kabla ya mkutano huo alifanya shughuli za kuimarisha chama ikiwa ni pamoja na kufungua matawi ya Chama hicho, barza pamoja na kuweka jiwe la msingi katika tawi la CUF Donge Muwanda.
Katika Mkutano huo Maalim Seif pia alikabidhi kadi kwa wanachama wapya 234, baadhi yao wakiwa wanachama na viongozi waliokihama Chama cha Mapinduzi kwa sababu tofauti, mmoja wao nd. Salim Khamis Nassor akiwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya (CCM).
No comments:
Post a Comment